Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido
Mhando akizungumza na wafanyakazi wa MCL jijini Dar es Salaam jana.
Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL), Tido Mhando amewaaga wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya
kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na nusu.
Mkataba wa Tido katika kampuni ya Mwananchi utafika kikomo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nation Media
Group (NMG), Linus Gitahi kwa wafanyakazi wote wa Afrika Mashariki
ambako kampuni hiyo inamiliki vyombo vya habari, inasema Mhando
anaondoka MCL huku akiacha mafanikio makubwa katika nyanja zote na
kwamba atakumbukwa kwa mchango wake.
MCL ni kampuni tanzu ya NMG inayochapicha magazeti
ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, The
Citizen on Saturday, Sunday Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL mwaka
2012, Mhando alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC) kati ya mwaka 2006 na 2010. Awali alikuwa Mkuu wa Idara
ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la BBC (1999-2006).
Mhando aliiwezesha MCL kukua kwa kasi kubwa katika
mapato na katika mpango wa uchapishaji wa magazeti ya MCL Kanda ya Ziwa
ambako wakazi wa mikoa hiyo sasa wamekuwa wakisoma magazeti asubuhi
tofauti na zamani.
Wafanyakazi wa MCL walimpongeza kwa kuboresha
masilahi yao kwa kipindi cha uongozi wake na kuandaa misingi bora ya
uongozi, ikiwamo kumwandaa mrithi wake.
Akiwaaga wafanyakazi jana asubuhi, Mhando
aliwashukuru kwa ushirikiano wao pia alisema amejifunza mambo mengi
mapya, ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi alikuwa kwenye sekta ya habari
ya utangazaji tofauti na uchapishaji. “Safari hii ilinipa uzoefu mpya na
wenye changamoto nyingi lakini kupitia ushirikiano wenu wa dhati
tulifanikiwa kuiweka kampuni katika hali nzuri,” alisema Mhando.
Gitahi alisema nafasi ya Mhando itachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL (COO), Francis Nanai.
Nanai alijiunga MCL , Agosti mwaka jana akitokea
Kampuni ya Saruji ya Mbeya Cement (Lafarge Tanzania) ya mkoani Mbeya
akiwa Mkurugenzi wa Biashara.
Post a Comment