0
Dar es Salaam.Watumiaji wa huduma za kibenki wametakiwa kujiepusha na wimbi kubwa la utapeli kwa njia ya mtandao linaonekana kushika kasi siku za hivi karibuni.
Wametakiwa pia kutokubali kutoa taarifa zao kwa watu wasiowafahamu kutokana na wengi wao kutumia fursa hiyo kufanya uhalifu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei kuhusu  huduma ya kutuma na kutoa pesa kupitia simu za mkononi (Simbanking) na changamoto ya uhalifu kwa njia ya mtandao aliwataka wateja wa benki kutunza taarifa za akaunti zao ikiwemo kadi na  namba za siri.
 “Wote tunafahamu kuwa kumeibuka matapeli kwenye mitandao ya kijamii wanaojaribu kuwalaghai wateja wetu kwa kuwaomba taarifa za akaunti zao ili kufanya uhalifu,”alisema na kuongeza:
“Tunawaomba wateja wetu kuwa makini na matapeli wanaopiga simu kujitambulisha kuwa ni wafanyakazi wa CRDB wakiwataka watoe maelezo ya akaunti zao ikiwemo namba za siri,  vilevile niwasihi wasitumie mwaka wa kuzaliwa kama namba ya siri na kuepuka kutunza namba hizo kwenye simu au anuani zao za mtandao.”
Hata hivyo, Dk Kimei aliwaondoa hofu wateja wa benki hiyo wanaotumia huduma ya Simbanking akisema kuwa imehakikiwa na imepitia viwango vyote vya usalama.

Post a Comment

 
Top