Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri
wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imetoa amri kwa Shirika la Usafiri Dar
es Salaam kutoza viwango sawa vya nauli kama vinavyotozwa na daladala
za kawaida.
Sumatra imetaka punguzo hilo la viwango vya nauli
kwenda sanjari na mabadiliko na tiketi za mabasi ya Uda ikielekeza
zianze kutumiwa wiki ijayo, huku Uda ikikiri kupokea agizo na kuahidi
kulitekeleza.
Akizungumza na gazeti hili, Ofisa Mfawidhi Kanda
ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shiyo alisema kuwa, kumekuwa na usumbufu
kwa abiria hasa wanaoutumia usafiri wa Uda, huku makondakta wake
wakitoza viwango vya juu vya nauli na kukatisha ruti kinyume na taratibu
akibainisha suluhu ni kufanya mabadiliko hayo.
“Tumeshapeleka mapendekekezo ya mchoro wa tiketi
mpya na viwango vya gharama za nauli makao makuu, hivyo tunasubiri
marejesho kutoka kwao ili utekelezaji uanze.Mchoro huo unaonyesha ruti
ya gari pamoja na kiwango cha nauli abiria anachotakiwa kulipa,”alisema
Shiyo na kuongeza:
“Nauli kwa ruti za mjini ambazo siyo za safari za
mbali kwa maana ya umbali wa kilomita 14 zitagharimu Sh400 hadi 450.
Kwa ruti zinazoanzia kilomita 15 hadi 25 nauli yake itakuwa Sh750…hivyo
ndivyo viwango vipya vya nauli za mabasi ya Uda zinazopaswa kuanza
kutumika wiki ijayo.”
Alisema, katika kuhakikisha hilo linakuwa endelevu
na wananchi wanaondokana na adha ya usafiri, maofisa wa Sumatra
watakuwa wanafanya operesheni endelevu kubaini madereva watakaokiuka
agizo hilo.
Shiyo alibainisha kuwa tayari utaratibu wa kutumia
vibao vinavyoonyesha ruti ambayo mabasi hayo yanatakiwa kwenda vimeanza
kutumika ili kuepusha madereva kuiba ruti.
“Pia tumeshawaambia wachore mistari au kuweka
stika zenye alama ya rangi za ruti hizo kwa sababu madereva ni
wajanja…ikifika usiku wanaweza kutoa kibao na kuiba ruti,”alisema Shiyo.
Amri hiyo imekuja wakati kukiwa na malalamiko
kutoka kwa watumiaji wa usafiri wa Uda, wakidai kutozwa gharama kubwa za
nauli tofauti na vinavyotozwa na mabasi ya daladala.
Kwa mujibu wa tiketi za sasa za Uda abiria
anatakiwa kutozwa kati ya Sh400 hadi 450 kwa umbali wa kilomita 14 na
Sh500 hadi 1,100 kwa umbali wa kilomita zaidi ya 20, lakini abiria
wamekuwa wakitozwa kinyume na kiwango hicho.
Viwango vya nauli za daladala huanzia Sh400 kwa safari ya umbali wa kilomita 14 hadi Sh750 kwa umbali wa kilomita zaidi ya 20.
Mkurugenzi wa Mafunzo Utafiti na Maendeleo wa
Kampuni ya Simon Group inayoendesha shirika hilo, Henry Bantu, alikiri
kuwapo kwa mabadiliko hayo ya viwango vya nauli.
“Tumekubaliana na Sumatra kubadilisha na kuboresha viwango vya
nauli zetu ambazo zitaanza kutumika hivi karibuni,” alisema Bantu na
kuongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kupata malalamiko kutoka wa
watumiaji wa usafiri huo.
Alisema, pia wameandaa semina kwa ajili ya
madereva wa Uda zaidi ya 500 ili kuongeza tija katika utendaji na
kuboeresha huduma za usafiri huo. Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano
wa Wizara ya Uchukuzi, Willium Budoya alisema licha ya kuwa Sumatra
ndiyo chombo teule cha kusimamia masuala ya usafiri wananchi pia
wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kwa wahusika.
“Sumatra wakiachiwa jukumu hilo peke yao haitoshi,
wananchi wanatakiwa kuhakikisha kuwa wao ndio wanaosema maovu si
kuyaendeleza…ushirikiano wao ni muhimu sana katika kutokomeza matatizo
ya aina hii,”alisema Budoya.
Mmoja wa wakazi wa jiji hili ambaye pia ni
mtumiaji wa usafiri huo, Neema Erasto alisema kuwa uamuzi huo utaleta
afueni kwa watumiaji wa usafiri wa Uda kwani umekuwa kero.
“Bora wamefanya hivyo..sisi watu wa hali ya chini
tumekuwa tunateseka kutokana na viwango vya nauli wanazotoza makondakta
wa Uda…haziendani na umbali aliosafiri abiria, lakini kwa sababu una
shida ya kusafiri unalipa,” alisema Erasto.
Takriban siku tano zimepita tangu Sumatra
ilipokamata daladala 75 katika operesheni maalumu iliyoanza mwanzoni mwa
wiki hii mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Post a Comment