Dar es Salaam. Visima vingi vya maji
vilivyochimbwa jijini Dar es Salaam na unga wa lishe kwa watoto
umeelezwa kutokuwa salama kwa afya za watumiaji, kulingana na utafiti
uliofanywa hivi karibuni na Ofisi ya Wakala wa Mkemia Mkuu wa Serikali
(GCLA).
Akizungumza wakati wa kuwatembeza katika maabara
za mkemia mkuu baada ya uzinduzi wa bodi ya wakurugenzi wa wakala huyo
jijini Dar es Salaam jana, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel
Manyele alisema sampuli zilizochukuliwa hivi karibuni zimebainisha.
Alisema maji yalichukuliwa kutoka katika visima
tofauti na kufanyiwa utafiti na maabara ya wakala huyo na kubainika kuwa
mengi si salama kwa matumizi ya binadamu na utafiti zaidi unaendelea
ili kubaini athari zaidi ambazo zinaweza kusababishwa na maji hayo.
“Tumechukua sampuli chache na zimeonyesha kuwa
maji hayo siyo salama hata kidogo na tunaendelea na utafiti kujua athari
zaidi ambazo zinasababishwa na maji hayo” alisema.
Alisema hali kama hiyo imeonekana pia katika unga wa lishe ambao unauzwa mitaani.
Alisema hali siyo nzuri kwa chakula hicho cha
watoto ambacho kimekuwa kikitumiwa na watu wengi nchini miaka ya
karibuni na walifanya uchunguzi huo wa kimaabara ikiwa ni sehemu ya
mipango ya ofisi hiyo ya mkemia kuchukua sampuli za vyakula tofauti na
bidhaa zingine kwa aili ya utafiti.
Profesa Manyele alisema wanatarajia kuwasilisha
bungeni mapendekezo ya muswada wa mabadiliko ya sheria ambayo yatatoa
mamlaka kwa wakala wa mkemia mkuu wa serikali kuchukua sampuli ya
vyakula, dawa au bidhaa zingine zozote na kuzifanyia uchunguzi katika
maabara na kutoa mapendekezo serikalini.
Post a Comment