“Ni vizuri viongozi wakaandaliwa, isiwe mtu anaibuka tu anagawa hela
halafu anashinda. Anatakiwa mtu atakayeweza kushughulikia matatizo ya
Watanzania. Watanzania ni wapole na wavumilivu lakini wanazungumza.
Hivyo anahitajika kiongozi atakayesikiliza mahitaji yao na kutoa
suluhisho, si kutoa ahadi za uongo,”
Dk Salim Ahmed Salim
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Waziri Mkuu
mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim kusema kuwa hana mpango na hafikirii tena
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wasomi na wanasiasa
wamezungumzia kauli hiyo wakisema ni ya kishujaa inayofaa kuigwa na
viongozi wengine.
Wakizungumza na gazeti hili wamesema, Dk Salim
ametambua mchango alioutoa kwa taifa hivyo hana budi kuwaachia nafasi
vijana nao wakatawala.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),
Dk Benson Bana alisema Dk Salim hana anachotaka kukifanya kwani
amelitumikia taifa kwa kipindi kirefu hivyo ameona ni busara kujiweka
kando na kuwa mshauri.
“Ni kauli nzuri na inayoheshimu busara, nafasi za
uongozi alizofikia ni hakika zinatosha kulingana na umri wake na siasa
chafu za nchini ni bora akawa pembeni na akatumika kama mshauri tu,”
alisema Dk Bana.
Naye mtaalamu wa masuala ya maendeleo na siasa wa
Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd Makombe alisema Dk Salim amejifunza
kutokana na siasa za mwaka 2010 wakati wa uchaguzi mkuu
zilivyochafuliwa.
Alisema Dk Salim ameona bora ajiondoe kulinda heshima yake, kitendo kinachotakiwa kuigwa na wanasiasa wengine.
“Mimi ninaamini kuwa kama Dk Salim angesimama
katika uchaguzi uliopita au ujao na kusiwepo na siasa chafu, angeshinda
bila ubishi,” alisema Dk Makombe.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe alisema kitendo cha Dk Salim kueleza kuwa ni lazima kuwa na
sifa za ziada ndiyo ushinde, imedhihirisha jinsi CCM inavyowapata
viongozi wake kwa njia zisizostahili.
“Hata uwe na sifa za aina gani lakini lazima
ufanye ujanja ujanja ndiyo ushinde. Sasa kwa watu ambao hawawezi kutumia
mbinu hizo ndiyo kama Dk Salim, anaona bora akae kando kwani haziwezi
mbinu hizo,” alisema Nyambabe.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John
Mnyika alisema, Dk Salim anatakiwa kuandika kitabu kuelezea yaliyojiri
tangu awamu ya kwanza ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere hadi awamu ya
tatu ya Rais Benjamin Mkapa katika mchakato wa kumpata mgombea urais.
Alisema kutokana na kuwa na uzoefu wa kimataifa
alimshauri Dk Salim atumie kitabu hicho kuelezea uzoefu wa mataifa
mengine kuwapata wagombea urais unavyokuwa akifananisha na chama chake
CCM ili kiwe ngazi na tunu ya taifa kwa kizazi kijacho.
Post a Comment