Waziri wa Fedha Saada Mkuya.PHOTO|FILE
Kwa ufupi
Tukipitia bajeti hizo na ya mwaka ujao wa fedha,
tunagundua kwamba kinachofanywa na watayarishaji wa bajeti hizo ni
kubadilisha tu takwimu za mwaka hadi mwaka na kuishia na bajeti
zinazotegemea mapato yatokanayo na pombe, sigara na soda.
Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha ilipitishwa
bungeni juzi baada ya wabunge kuijadili kwa siku saba. Kama wananchi
wengi walivyoshuhudia, Bajeti hiyo iliibua mijadala mikali, huku wabunge
wengi wakitishia kutoiunga mkono kutokana na Serikali kushindwa kubuni
vyanzo vipya vya mapato, huku misamaha ya kodi ikiendelea kuikosesha
fedha nyingi na kusababisha nakisi kubwa katika Bajeti hiyo.
Haishangazi hata kidogo kuona kwamba Bajeti hiyo
ilipitishwa kwa idadi kubwa ya ‘kura za ndiyo’ 234, huku wabunge 66 wa
vyama vya upinzani waliopiga kura wakiikataa. Kinachoshangaza ni pale
wabunge wengi wa chama tawala waliokuwa wametishia kuikwamisha
waliipitisha kwa misingi ya kiitikadi na msukumo wa kile kinachotajwa
kuwa ni kutunza nidhamu ya chama. Hivyo, pamoja na upungufu mkubwa
uliomo, wabunge hao waliona bora kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Majumuisho ya Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya
kuhusu mapendekezo ya wabunge waliochangia mjadala wa Bajeti hiyo
hayakuonyesha kama Serikali imeyapa mapendekezo ya wabunge uzito wa
kutosha, isipokuwa katika maeneo machache kama misamaha ya kodi.
Serikali ililiomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh19.9 trilioni kwa
matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo. Lakini katika kuthibitisha
kwamba bajeti hiyo siyo endelevu, fedha za maendeleo zilizokuwa
zimetengwa ni Sh6.44 trilioni sawa na asilimia 32.4 tu ya bajeti, huku
fedha zilizoombwa kwa matumizi ya kawaida ni Sh13.4 trilioni sawa na
asilimia 67.4 ya bajeti hiyo.
Wabunge walitaka kipaumbele kiwekwe kwenye sekta
za elimu, afya, maji, miundombinu na nyingine kadhaa zilizoainishwa
katika mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), badala ya fedha
nyingi kutengwa kwa ajili ya matumizi yasiyo muhimu kama semina, safari
za viongozi, posho, magari ya kifahari na matumizi mengine ya anasa.
Kwa mfano, safari za Rais zilitengewa Sh50 bilioni, wakati Kilimo
kilitengewa Sh51 bilioni. Hata hivyo, pamoja na Kamati ya Bunge ya
Bajeti kuibana Serikali, ni Sh165.8 bilioni tu zilizopunguzwa kwenye
matumizi yasiyo na tija kwa taifa.
Katika majumuisho ya Waziri Mkuya, jambo
lililojitokeza bayana ni kwamba Serikali haijawa tayari kubadilika na
kutumia ubunifu katika kutayarisha bajeti za Serikali, badala ya
kuendelea na bajeti za mazoea. Katika utayarishaji wa Bajeti, lazima
Wizara ya Fedha iwahusishe wadau, kama Repoa, Twaweza, TGNP na ESAURP
ili ichote fikra mpya na kuleta mabadiliko yanayoweza kuliwezesha taifa
kuondokana na Bajeti tegemezi. Tumekuwa tukisema bajeti za Serikali
zinarudufiwa, kwa maana ya kubeba maneno, maelezo na maudhui
yanayofanana sana na ya bajeti za miaka iliyopita. Tukipitia bajeti hizo
na ya mwaka ujao wa fedha, tunagundua kwamba kinachofanywa na
watayarishaji wa bajeti hizo ni kubadilisha tu takwimu za mwaka hadi
mwaka na kuishia na bajeti zinazotegemea mapato yatokanayo na pombe,
sigara na soda.
Inasikitisha kuona kwamba Waziri Mkuya hakutoa
sababu za Serikali kushindwa kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Bunge
ya Bajeti kuhusu vyanzo vipya vya mapato, ambavyo vingemaliza tatizo la
nakisi katika bajeti za Serikali kama mapendekezo hayo yangetekelezwa.
Pamoja na kusema Serikali inahitaji muda zaidi kufanya utafiti wa kuona
utekelezaji wa mapendekezo hayo, hakusema hatua ambazo Serikali
imechukua hadi sasa kutokana na wabunge kupigia kelele suala hilo mwaka
hadi mwaka.
Post a Comment