Juni 18 mwaka huu, Bodi ya Pamba (TCB) ilitangaza kuanza kwa
msimu mpya wa uvunaji wa zao hilo, sambamba na kutangaza bei mpya kwa
msimu wa mwaka 2014/15 kwa wakulima kutoka Kanda ya Ziwa.
Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Kijiji cha Isole,
Wilaya ya Sengerema na kuhudhuriwa na wakulima ambao walikuwa na shauku
ya kutaka kujua wanafaidika na nini mwaka huu baada ya kulima pamba?
Nikiwa miongoni mwa watu waliohudhria sherehe za
kutangazwa kwa bei mpya ya msimu wa pamba, nilishuhudia waziwazi nyuso
za wakulima waliohudhuria sherehe hizo zikiwa na matarajio makubwa ya
kupata faida kwa msimu huu.
Lakini, baada ya makamu mwenyekiti wa TCB, George
Wassira kutangaza bei mpya ya pamba, zilisikika sauti za chinichini
kutoka kwa wakulima ambazo ziliashiria kutoridhishwa na bei hiyo.
Makamu huyo mwenyekiti wa TCB alitangaza kuwa kwa
msimu wa mwaka 2014/2015 pamba imeongezeka kwa Sh50, kutoka Sh700 kwa
kilo moja kwa msimu wa mwaka 2013/2004 hadi kufikia Sh750 kwa kilo kwa
msimu wa mwaka 2014/15.
Miongoni mwa malalamiko ya wakulima ni pamoja na
gharama kubwa wanazotumia wakati wa kuandaa mashamba na kwamba na bei
iliyotangazwa na TCB kuwa ndogo, haiwezi kufikia hata robo ya gharama
wanazotumia.
Kila msimu wa kuvuna pamba unapokaribia kumekuwa
na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wa zao hilo, hivyo kuna haja kwa
Serikali kutafuta njia mbadala ya kuwasaidia wakulima hawa ili waweze
kupata faida.
Hata hivyo, moja ya vitu ambavyo wamekuwa
wakilalamikia wakulima hao ni hatua mbalimbali ya upangaji wa bei. Mosi
wanadai kuwa hawashirikishi, hivyo kama suala hili ni vyema likatafutiwa
ufumbuzi ili kuwafuta machozi wakulima hawa ambao kila kukicha wanakuwa
na malalamiko lukuki.
Pili, wakulima wamekuwa wakidai Bodi ya Pamba
ndiyo wapangaji wa bei na hao ndiyo wanunuzi wa pamba, hivyo ni wazi
haiwezi kutoa bei zenye faida kwao. Kama jambo hilo ni kweli ni vyema
Serikali ikalitazama na kuchukua hatua stahiki. Siyo vyema kuona mtu
ambaye anategemea kilimo kama sehemu ya maisha yake, kupata hasara na
kuwanufaisha watu wachache.
Hayo ni baadhi ya malalamiko, ukiondoa mengine ya
utumiaji wa mizani ya digiti ambazo wakulima wengi wanadai kwamba
zinawaibia zaidi kwa kuwa hawafahamu jinsi ya kuzitumia.
Si jambo la busara kama hujatoa elimu sahihi ya
matumizi ya kitu halafu unawapelekea wakulima watumie wakati unafahamu
wazi kwamba wengi wao wana elimu ya kawaida.
Baadhi ya maneno ambayo wakulima wa pamba
walitamka ni pamoja na “elimu zetu ni za kawaida, leo tunaletewa mizani
ya digiti ili kupima pamba zetu. Hii kama siyo njia ya kutunyonya na
kutaka kutuibia, ni nini?” alihoji mkulima mmoja.
Ni vyema Serikali kupitia TCB kulitazama jambo hilo kwa kina ili
kuhakikisha inaondoa malalamiko ya wakulima na kuwawezesha kupata faida
kupitia kilimo chao cha pamba.
Kwa sasa wakulima wengi wa pamba ambao ni wa kawaida wanadai kutumia Sh30,000 kwa kulima na kukodi shamba ni Sh100,000.
Kwenye hatua za mwanzo jambo hili linawasababishia kutumia gharama kubwa tofauti na matarajio yao wakati bei zinapotangazwa.
Aidan Mhando ni mwandishi wa habari wa gazeti la Mwananchi.
Post a Comment