Rufiji ni wilaya tajiri sana. Sidhani kama wananchi na viongozi
wanalielewa hilo. Kuwa mto mkubwa kuliko yote nchini, unapita wilayani
hapo na kuachia tani za maji baharini na kutapanya mbolea asili huko na
huko ardhini. Ni utajiri ambao unahitaji watu wenye kufikiri kwa makini,
na wanaotaka maendeleo ya wananchi wao. Na kuwa Rufiji inaweza pia kuwa
sehemu ya utalii wa wanyama kama viongozi na wananchi wangekubali hilo.
Nilikuwa Rufiji Delta hivi karibuni. Awali sikuwa nina picha kamili ya
delta hiyo ikoje. Na kwa kweli siwezi kuielezea ikoje kwani ninachoweza
kusema tu ni kuwa mto Rufiji umezaa mito mikubwa, baadhi ikiwa na upana
wa nusu kilomita ikitengeneza visiwa vingi ambako watu wanaishi.
Na kuwa hata utumie mtumbwi wenye injini, huwezi
ukatembelea kila mahali kwa siku moja. Unahitaji siku mbili. Delta hii
ina utajiri mwingi.
Kwanza ni utajiri wa maji ambayo ndani yake
unaweza kufanya uvuvi wa samaki na uvuvi wa dagaa. Katika pitapita yangu
na mtumbwi katika delta hiyo tuliona uwezekano wa kuwekeza katika
uvuvi. Wavuvi walioko ni wale wa kutumia mitumbwi ya makasia, ambayo
huwezi kutegemea kuwa na tija kubwa.
Lakini tukakutana na wavuvi wawili wa samaki aina
ya kamba ambao mtumbwi wao ulijaa samaki hao wakiwa hai, sijui walikuwa
wakienda nao wapi? Tulipowauliza bei walisema kuwa ni Sh1,000 kwa fungu
la kupima kwa mkono.
Nilinunua fungu tatu,na wenzangu wakanunua mengi
zaidi, ni kama kilo sita kwa jumla;, kwa ukubwa wa Kamba wale, tena
wakiwa hai, hotelini tungenunua kama kwa Sh50,000. Nina uhakika kabisa
kwa kuwa na uratibu mzuri sana wa kimazingira, na wa kibiashara, wavuvi
wale wanaweza kupata faida kubwa kwa biashara hii ya Kamba. Lakini sijui
kama viongozi wanajua kama huu ni utajiri mkubwa sana. Ukiachia mbali
hilo, kuna utajiri wa samaki wa kawaida ndani ya mito mingi inayopishana
eneo hili.
Delta hiyo ina utajiri wa kihistoria! Hapo ndipo
palipojengwa boma la kwanza, mwaka 1906 la Mjerumani kabla ya lile la
Utete. Boma hilo liko hadi leo, likitumika kama zahanati ya kata ya
Salali.
Na jirani na hapo, kama mita miambili ndipo ilipo
meli ya kivita ya Kijerumani ya Konisberg ambayo ilipigwa mabomu na
majeshi ya Waingereza.
Ndiyo niliyoilalamikia katika makala iliyopita; na
kuwa hapo vita vilipiganwa sana kwa vile sio tu koloni la mjerumani
lilikuwa likitetea, bali pia kulikuwa na ofisi ya serikali ya kikoloni.
Lakini utajiri huu wa kihistoria, kama nilivyosema, umetelekezwa na
kuachwa wawindaji wa skrepa waivamie na kuimaliza kwa kuikatakata.
Kabla ya watu kuongezeka eneo hilo, lilikuwa sehemu ya hifadhi ya wanyama ya Selous.
Na si miaka mingi iliyopita tembo, simba na
wanyama wengine walikuwa wakionekana katika msitu unaopakana na delta
hii. Msitu huu uko chini ya hifadhi.
Kumbe kama serikali ya Wilaya ya Rufiji ingeamua,
ingeweza kuufanya msitu huu kuwa zoo (hifadhi ya kutembelea wanyama kwa
burudani), au mbuga kamili ya wanyama , ambayo ingefanya tuwe na mbuga
ya pili nchini inayopakana na Bahari ya Hindi baada ya Saadani.
Inanishangaza kuwa tunataka kuwa na utalii wa
ndani, lakini kivutio kama hiki cha Rufiji Delta kinapuuzwa. Delta hii
ingeweza kuvutia watalii wa kimazingira (eco-tourists), ambao wangetaka
kupata burudani ndani ya mito hii mikubwa ya delta, na kutembelea
hifadhi ya mikoko na kujua maisha ya watu.Kwa kuwa na kambi za muda kwenye eneo hilo, ingeweza kuwafanya watalii
kufika na kutoka, na hivyo kuongezea wananchi kipato kutokana na utalii.
Badala yake, tunaruhusu wananchi kufanya kilimo ambacho kinaharibu uoto
na mifumo mingine ya bionuwai. Rufiji iamke usingizini.
Post a Comment