Posted Alhamisi,Juni26 2014 saa 14:42 PM
Kwa ufupi
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na uelewa wa biashara
anayoifanya kwani uelewa au weledi wa jambo ni kivuko kimojawapo kati ya
vivuko vingi ambavyo humvusha mwanadamu kutoka katika hali duni kwenda
katika hali nzuri.
Wataalamu mbalimbali wa uchumi duniani wamefanya utafiti na
kubaini kuwa biashara zinazoanza zinakabiliana na changamoto mbalimbali
kwani takriban asilimia 64 ya biashara hushindwa kuendelea ndani ya
miaka mitano tangu zimeanzishwa. Hii ina maana kuwa kiasi cha biashara
zinazokua ni kidogo sana ukilinganisha na kile kinachoishia njiani.
Kufa kwa biashara nyingi zinazoanza ndani ya miaka mitano kunatokana na sababu mbalimbali hasa zinazohusu mjasiriamali mwenyewe.
Sababu nyingine ni mazingira, mfumo mzima wa nchi
katika uandaaji wa mazingira mazuri ya kukuza biashara na matatizo ya
asili ambayo yanakuwa nje ya uwezo wa mwanadamu katika kukabiliana nayo.
Kwa vile lengo la kufanya biashara ni kutaka kuona
kuwa biashara husika inakua na kuwa kampuni kama biashara husika
haikuanzishwa kama kampuni, zifuatazo ni mbinu zinazoweza kutumiwa na
mjasiriamali katika kuhakikisha biashara anayoianzisha haiishii njiani,
bali inapiga mbizi ndani ya mawingu makubwa na ngurumo za radi kuelekea
kwenye sehemu salama na yenye mafanikio.
Mjasiriamali anatakiwa kufanya tathmini ya kina
juu ya biashara yake ili aweze kubaini fursa na changamoto zilizoko kwa
lengo la kuepukana na anguko analoweza kulipata katika safari ya
biashara yake.
Ikumbukwe kuwa, wakati mwingine mjasirimali huamua
kufanya biashara bila kufanya tathmini ya kina kwa kuwa tu ana mapenzi
na biashara hiyo na matokeo yake huwa ni anguko la kibiashara kwani kuwa
na mapenzi ya kitu fulani huweza kuwa na upofu ambao madhara yake ni
makubwa kibiashara.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na uelewa wa biashara
anayoifanya kwani uelewa au weledi wa jambo ni kivuko kimojawapo kati ya
vivuko vingi ambavyo humvusha mwanadamu kutoka katika hali duni kwenda
katika hali nzuri.
Mara nyingi wajasiriamali wengi huishia njiani
kutokana na uelewa mdogo wa biashara anayoifanya ambao husababisha
ashindwe kukabiliana na changamoto za wakati na mazingira.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na ufshsmu wa mahitaji
ya kitaalamu ya biashara yake ili kuepukana na changamoto zinazoweza
kuangusha biashara yake, kwa mfano, kama wewe ni mfanyabiashara wa
magari unatakiwa uwe unajua angalau nusu ya kila jambo linalohusiana na
magari.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na uelewa juu ya
masuala ya kifedha kama vile kutunza kumbukumbu za mauzo na manunuzi
ikiwa ni pamoja na mambo mengine ya kifedha yanayohusiana na biashara
yake.
Tafiti zinaonyesha kutokuwa na uelewa wa masuala
ya kifedha ni moja ya sababu za kushindwa kukua kwa baadhi ya biashara
duniani kote.
Mjasiriamali anatakiwa kuwa na uelewa juu ya
sheria zinazohusiana na biashara anayoifanya ili kuepukana na kero
ndogondogo zinazoweza kuangusha biashara yake kwani uzoefu unaonesha
kuwa baadhi ya sehemu hapa nchini zimekuwa na baadhi ya watendaji wa
Serikali ambao huwa na malengo ya kuwakomoa wajasiriamali kwa kutoa
vitisho kwa baadhi ya wajasiriamali ambao kwa kutoelewa sheria
ndogondogo, huamua kutelekeza biashara zao.
Ikumbukwe kuwa kuna wataalamu waliobobea katika masuala ya
biashara kama vile sheria, uongozi na usimamizi wa biashara ambao kazi
yao ni kushauri namna ya kufanya biashara kwa mafanikio kwani kazi ya
mjasiriamali inafanana na msemo wa Kichina usemao “kikombe kilichojaa,
hakina manufaa” kwa maana kuwa mjasirimali hajabobea katika kila jambo
la biashara anayoifanya bali mwenye uelewa wa jumla wa biashara
anayoifanya.
Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu wa ujasiriamali na mtunzi wa vitabu
Post a Comment