Moja ya biashara zinazovutia watu wengi ni biashara ya vipodozi.
Hata hivyo wafanyabiashara wa vipodozi wamekuwa wakikabiliana na
changamoto mbalimbali. Baadhi ya changamoto hizi ni baadhi ya
wafanyabiashara kutofahamu taratibu za kufanya biashara hii.
Katika makala ya leo nitaeleza namna ya
kujihusisha na biashara ya vipodozi kuanzia kusajili jengo, kuagiza
bidhaa za vipodozi kutoka nje ya nchi na kusajili vipodozi.
Vipodozi ni wingi wa bidhaa kipodozi. Kipodozi ni
kitu chochote kinachoweza kutumika kwenye mwili au sehemu ya mwili kwa
njia ya kujipaka, kuosha, kunyunyuzia, kujipulizia, kwa ajili ya
kusafisha, kujiremba, kujipamba, kuongeza uzuri wa ngozi au muonekano wa
sura.
Kwa mujibu wa sheria ya chakula, Dawa na Vipodozi
ya mwaka 2003, TFDA ndiyo yenye kudhibiti ubora na usalama wa bidhaa za
vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya ya jamii.
Sheria hii pia inakataza kuuza, kuhifadhi au
kutengeneza chakula, dawa na vifaa vya tiba isipokuwa katika maeneo
yaliyosajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na
mtengenezaji bidhaa awe na leseni ya bidhaa iliyotolewa na mamlaka.
Ni marufuku mtu kutengeneza kwa kuuza, kusambaza
au kuhifadhi bidhaa zinazosimamiwa kwa mujibu wa Fungu la 18 la sheria
ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya Mwaka 2003, isipokuwa kwenye maeneo
yaliyosajiliwa na TFDA.
Ili uweze kufanya biashara ya vipodozi unapaswa
kuhakikisha kuwa vipodozi unavyotaka kuuza vimesajiliwa na Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA). TFDA imeweka utaratibu unaomwezesha mtu yeyote
kusajili bidhaa za vipodozi. Tangu mwaka 2003 mpaka Juni 2013 TFDA
imesajili jumla ya vipodozi 3,968.
Usajili wa vipodozi unajumuisha utathimini wa
taarifa za ubora na usalama wa viambata vilivyotumika, uchunguzi wa
kimaabara wa sampuli za vipodozi husika na tathimini ya taarifa za
kwenye lebo.
Taratibu za kusajili vipodozi
Kama unataka kusajili vipodozi unatakiwa kuomba Usajili wa Vipodozi TFDA.
Wasilisha maombi yako kwa kujaza Fomu ya Maombi
ukamilifu pamoja na sampuli mbili za bidhaa. Fomu hizi zinapatikana
katika ofisi za TFDA na tovuti ya mamlaka. Wasilisha nakala ya kawaida
na ya kielektroni kwenye CD-ROM kwa muundo wa PDF, fonti 12 mtindo wa
zamani wa “bookman”. Kama unasajili bidhaa zaidi ya moja, wasilisha fomu
ya maombi iliyojazwa kwa ukamilifu tofauti kwa kila bidhaa au bidhaa
mbadala.
Katika maombi ya usajili wa vipodozi lipa pia ada
ya tathmini na usajili ya dola za Marekani 75.00 kwa kipodozi cha
kilichotengenezwa nje ya nchi au dola za marekani 45.00 kwa kipodozi
kilichotengenezwa nchini. Iwapo mamlaka itaridhika, itatoa usajili wa
kipodozi. TFDA itakataa kusajili wa vipodozi kama itakugundua kama kuna
ukiukwaji wa utaratibu katika usajili au bidhaa inayotarajiwa kusajiliwa
ina viambato vyenye sumu ambavyo ni hatari kwa matumizi ya binadamu.
Baadhi ya viambata hivi ni Hydroquinone, Mercury na steroids.
Masharti ya kusajili vipodozi
Anayesajili vipodozi anatakiwa kuwa mkazi wa
Tanzania au kampuni iliyoandikishwa/kusajiliwa nchini Tanzania. Nyaraka
zote za maombi zinatakiwa kuwa zimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza au
Kiswahili. Muombaji wa usajili wa vipodozi anatakiwa kuwasilisha
sampuli, nyaraka na taarifa nyingine kadri atakavyoelekezwa au kutoa
ufafanuzi kutegemea hali halisi ya bidhaa anayotaka kusajili. Martin
Malima ni mtaalamu wa masoko kutoka TFDA
Post a Comment