Ajali za barabarani zimekuwa ni janga kubwa kwa taifa letu.
Ajali hizi kwa muda wa hivi karibuni zimeongezeka sana na kusababisha
watu kufariki dunia, kupotelewa mali, kupata majeraha, kupata ulemavu wa
kudumu na watu wengi wamejikuta maskini kwa sababu ya ajali za
barabarani. Wengine wanafia njiani wakihangaika kupata haki zao.
Mtu anapofariki dunia kwa ajali watu wengi huathirika, ikiwa ni pamoja na watoto na ndugu wa marehemu.
Ndugu msomaji utagundua kwamba kila anayesoma
makala haya anajua kuwa kuna watu zaidi ya watano anawafahamu
walishafariki kutokana na ajali.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2013 ya utafiti
uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, mwaka 2013 zilitokea
ajali 24,480, na kusababisha vifo vya watu 4,091.
Rekodi ya bodaboda pekee inaonyesha watu 1,106 walifariki dunia na watu 6,581 wamepata ulemavu.
Hii ina madhara mengi kiuchumi ikiwa ni pamoja na
upotevu na uharibifu wa mali, kupunguza nguvu kazi ya taifa na hivyo
kusababisha uchumi kushuka.
Sheria gani zinatumika kusimamia usalama na kulipa fidia?
Sheria juu ya usalama barabarani inasimamiwa na
Sheria ya Usalama Barabarani namba 30 ya mwaka 1973, linapokuja suala la
kudai fidia kwa dereva aliyeendesha kwa uzembe kesi mbalimbali
zilizohukumiwa juu ya hili japo ndio zitakuwa msingi wa madai yako.
Kama madhara yatasababisha kifo, sheria ya ajali sura ya 360, hutumika kutoa fidia kwa waathirika wa ajali barabarani.
Haki za kisheria kwa mwathirika
Mtu au watu waliopata ajali au ndugu zao wanaofariki kutokana na
ajali za uzembe wana haki ya kufungua shauri la madai na kufungua
shitaka la madai ili waweze kufidiwa na waliowasababishia madhara kwa
kufuata utaratibu wa sheria. Kwa mujibu wa sheria ya ukomo ya mwaka
1971, madai hayo yanatakiwa kuletwa ndani ya miaka mitatu tangu kutokea
kwa ajali.
Vitu vya kuthibitisha kuwa dereva alikuwa mzembe
Dereva wa chombo cha moto ana wajibu mbalimbali
kisheria, akivunja huo wajibu na ikathibitika kisheria, dereva au
mmiliki wa chombo hicho atakuwa na jukumu la kutoa fidia. Wajibu huu
unafahamika kwa madereva wote, polisi na watu wa kawaida, ikiwa ni
pamoja na;-
Wajibu wa kuwa mwangalifu muda wote anapoendesha
chombo cha moto na kutotumia simu; uangalifu ni pamoja na kuzingatia
alama za barabarani na mengineyo.
Wajibu wa kuendesha gari kwa mwendo unaokubalika
kisheria, kwa kuangalia mazingira husika, mfano, kukiwa na watu wengi
huwezi kuendesha kwa mwendo sawa na sehemu isiyokuwa na watu kabisa.
Wajibu wa kuweka gari katika hali nzuri, ikiwa ni pamoja na kulifanyia
matengenezo kila mara.Watu wengi wamekuwa wakiendesha magari bila
kuyafanyia matengenezo.
Dereva aliyepo barabara ndogo anayetaka kuingia
barabara kuu ana wajibu wa kusimama na kutoa njia. Madereva wengi
wamekuwa na tabia ya kutishia kama anaingia barabara kuu, hasa madereva
wa gari za abiriam na endapo utatishika na kusababisha ajali,
utawajibika kisheria.
Wajibu wa kuheshimu watumiaji wengine wa barabara ni wajibu mwingine unaotegemeana na kesi husika.
Kipi kinaweza kufidiwa?
Kisheria mahakama inaweza kutoza fidia kwa majeraha yaliyosababishwa kwa mtu, vifo vilivyotokea kutokana na ajali.
Endapo mtu amekufa, shauri lake lazima lipelekwe na msimamizi wa mirathi aliyechaguliwa kisheria kwa niaba ya wanufaika.
Aliyekumbwa na ajali kwa mazingira ya uzembe anaweza kudai fidia kwa madhara yafuatayo:
Athari za kimwili zilizosababishwa na ajali,
athari kwenye mwili ni baadhi ya madhara yanayoweza kufidiwa mfano ni
shauri la Mondo dhidi ya Jessa (1969).
Katika shauri hilo, mdai alivunjika uti wa mgongo mpaka kupooza,
mahakama ikaamuru alipwe kiasi cha Sh90,000 kwa mwaka huo wa 1969.
Machungu na maumivu pia yanaweza kufidiwa endapo
mtu atapata maumivu. Sheria haisemi maumivu ya wakati wa ajali tu, hata
maumivu ya mbeleni kama ya upasuaji.
Pia kupoteza furaha ya maisha, mfano mtu alikuwa
mwanamichezo au mwanamazoezi ajali ikasababisha akakatwa mguu atapoteza
furaha ya maisha, mahakama inaweza kutoa fidia hii pamoja na fidia ya
jumla.
Kupoteza kiungo kwa ajali kutaongeza fidia
unayotakiwa kudai kwa mhusika mfano kukatwa mkono au mguu, mfano shauri
la mwanasheria mkuu dhidi ya Vinod (1971), mtu huyu mguu wake ulipungua
urefu kutokana na ajali, mahakama ikaamuru afidiwe.
Madhara mengine ni kupoteza uwezo wa kufanya kazi,
kukosa mapato, gharama za matibabu, mapato yanayotarajiwa, upotevu wa
mali wakati wa ajali.
Katika ajali kuna uwezekano mtu aliyehusika kwenye
ajali akafariki, anaweza kuwa alikuwa baba wa familia “Bread Winner”
kifo chake kinaweza kuathiri watu wengi waliokuwa wanamtegemea.
Usikose mwendelezo wa makala haya Alhamisi ijayo.
Jebra Kambole ni mtaalamu wa Sheria kutoka Kampuni ya Law Guards ya Jijini Dar es Salaam.
Post a Comment