Taarifa zilizopatikana kutoka wizarani zinaonyesha kuwa kati ya
wagonjwa 150 na 200 husafirishwa na Serikali kwenda nchini India, ambako
kuna uhakika wa matibabu, kila mwaka. Idadi hii haijumushi wale
wanaolipiwa na ofisi zisizo za serikali au wanaojilipia wenyewe.
Msemaji wa wizara ya afya, Nsachris Mwamaja
anaeleza kuwa serikali huwapeleka nje wagonjwa wote wenye mahitaji
japokuwa haweki wazi kiasi kinachotengwa kwa ajili hiyo.
“Mtu yeyote ambaye atathibitishwa kutoka hospitali
za serikali kama Muhimbili na Bugando hugharamiwa matibabu yake…yeye
pamoja na wanaomsindikiza. Wote hupokelewa na mwambata wa afya aliye
katika ubalozi wetu katika nchi husika ambako amependekezewa akapate
matibabu hayo,” alisema na kuongeza kuwa:
“Kiasi cha fedha kinachotengwa hubadilika kila mwaka na huweza kuongezwa kama itaonekana kuna haja katika mwaka husika.”
Kwa taarifa zilizopatikana kutoka ubalozi wa India
ni kwamba kila mgonjwa anapewa nafasi ya wasaidizi wawili wanaoruhusiwa
kuambatana naye na kila mmoja ni lazima awe na taarifa ya fedha ya
benki (bank statement) isiyopungua dola za Marekani 1,500.
“Hii ni lazima kwa wale wote wanaojilipia au wanaolipiwa na makampuni binafsi,” anasema Karki.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwepo kwa ongezeko la
maradhi ya moyo ulimwenguni. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria
kuwa takribani watu milioni 12 wanakufa kwa maradhi haya duniani kila
mwaka huku kukiwa na ongezeko la asilimia 26 kwa mwaka hapa nchini.
Pamoja na ongezeko hilo, matibabu ya maradhi hayo
bado hayakidhi mahitaji kutokana na idadi ya wagonjwa kulemea uwezo wa
vituo na hata wataalamu wa kitengo hicho waliopo. Mpaka wakati huu ni
hospitali chache zinafanya upasuaji wa moyo na kutibu magonjwa yake
nyemelezi.
Hospitali ya Aga Khan
Mkurugenzi wa tiba wa Hospitali ya Aga Khan, Dk
Jaffer Dharsee anathibitisha uwepo wa tatizo hilo na kusema kuwa
hospitali yake inajipanga kutoa huduma za uhakika za matibabu hayo hapa
nchini; kwa wananchi na hata wageni.
“Tumeanza ujenzi wa jengo litakalokuwa maalumu kwa
ajili ya maradhi ya moyo ambalo litakamilika Julai mwaka huu. Litakapo
kamilika litakuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 24 kwa wakati mmoja na
hivyo kupunguza idadi ya wanaoenda nje. Tayari tunao madaktari bingwa
watatu watakaotoa huduma hiyo,’ anasema mkurugenzi huyo.
Hospitali hiyo hupokea wagonjwa wa moyo wapatao 4,320 kwa mwaka
ambao hulazimika kuwasafirisha nje ya nchi kutokana na yenyewe kutokuwa
na uwezo wa kuwahudumia ipasavyo.
Kituo cha Moyo-Muhimbili
Mwishoni mwa mwezi Aprili Rais Kikwete alizindua
kituo cha upasuaji, tiba na mafunzo ya moyo katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili. Kituo kilichogharimu kiasi cha Sh26.6 bilioni kimejengwa na
serikali kwa ufadhiri wa Serikali ya Watu wa China iliyotoa Sh16.6
bilioni huku kilichobaki kikitolewa na Tanzania.
Kituo hicho chenye vitanda 98 na uwezo wa
kuhudumia wagonjwa 400 kwa siku kina changamoto ya wataalamu wa kutoa
huduma hiyo kiasi cha kumshawishi Naibu Spika wa Bunge la China, Chen
Changzhi, kutoa ahadi ya kuleta wataalamu hao kutoka nchini kwake wakati
serikali ikiendela kuwaandaa wa kwake.
“Kituo tunachokizindua leo ni chenye vifaa vya
hali ya juu vinavyotumia teknolojia ya kisasa katika uchunguzi na tiba
ya magonjwa ya moyo. Kupatikana kwa kituo hiki, Tanzania inapiga hatua
nyingine muhimu katika kuendeleza huduma ya afya nchini,” alisema Rais
na kuongeza:
“Maradhi haya yameanza kuwa tatizo kubwa hapa kwetu, hivyo hatuna budi kuchukua hatua thabiti kukabiliana nayo.”
Kwa upande wake Changzhi, alikaririwa na vyombo
vya habari akisema kuwa katika kuendeleza mahusiano mazuri yaliyodumu
kwa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili, serikali yake italeta madaktari
wa moyo 48 ili wasaidie utoaji wa huduma hiyo hapa nchini.
Fursa
Kwa kujijengea uwezo wa ndani wa kutoa huduma za
upasuaji wa moyo siyo tu Tanzania itaokoa fedha zinazotumika kupeleka
wagonjwa nje ya nchi, lakini itajipatia fedha za kigeni kutoka nchi
jirani ambazo hazijaanza kutoa huduma hii.
Dk Dharsee anaeleza kuwa kwa sasa wanalazimika
kupeleka mgonjwa mmoja kila baada ya wiki tatu nchini Kenya, ambako wana
hospitali kubwa, kwa ajili ya huduma zaidi lakini anasisitiza kuwa
kukamilika kwa kituo cha hapa nchini kitakuwa msaada kwa watu wengi.
“Tunatarajia kuwa kituo kitatoa huduma hii kwa
wagonjwa kutoka nchi nyingine tano tunazopakana nazo kama Kongo, Rwanda,
Malawi, Msumbiji na Uganda. Tunatarajia kukiimarisha zaidi pindi
kitakapoanza kufanya kazi,” anasema Dk Dharsee.
Naye mkuu wa kituo cha tiba na mafunzo ya moyo, kilichozinduliwa
Muhimbili, Dk Robert Mvungi anasema kuwa wamejipanga kutoa huduma hiyo
kama inavyotarajiwa na kwamba hakutakuwa na ubaguzi wowote.
“Jukumu langu ni kutoa tiba bila kujali kama
mgonjwa ni kiongozi wa serikali au raia wa kawaida. Wote watahudumiwa
kwa usawa kama inavyotakiwa,” anasema Dk Mvungi.
Taarifa zinaonyesha kuwa jumla ya wagonjwa 363
wamefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo hapa nchini. Wagonjwa 330 wamefanyiwa
katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na 33 katika kituo hicho kinachotarajiwa
kufanya upasuaji mkubwa siku za mbeleni.
Wadau wa afya wanasema kuwa endapo serikali
itashirikiana na sekta binafsi kuidhatiti sekta ya afya kuna dalili zote
kuwa itajiingizia fedha nyingi za kigeni na kuondokana na madeni kama
hili la Sh21 bilioni tunazodaiwa na nchi mbili; Afrika Kusini na India
ambazo zimewekeza kiasi cha kutosha.
Pamoja na wizara ya afya kupitisha bajeti ya
takribani Sh623 bilioni kwa mwaka huu wa fedha kamati ya bunge ya huduma
za jamii iliinyooshea kidole serikali kwa kushindwa kutenga fungu la
kutosha ikiwa ni pamoja na kutotekeleza mkataba wa Abuja, uliosainiwa
mwaka 2001, unaozitaka serikali za nchi kutenga asilimia 15 ya pato la
taifa (GDP) kwa ajili ya wizara ya afya.
Post a Comment