Zanzibar.Mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar,
Mohamed Raza Dharamsi anadaiwa kodi inayotokana na gawio la faida kwa
muda wa miaka 16 na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia
Kampuni ya ZAT inayotoa huduma za viwanja vya ndege visiwani Zanzibar,
imefahamika.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Fedha, Omar Yussuf
Mzee katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akichangia Bajeti ya
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano baada ya baadhi ya wajumbe kutaka
kujua kwa nini kampuni ya ZAT hailipi kodi kwa wakati mwafaka ikiwamo
gawio la faida ya Serikali la asilimia 5 kutokana na mapato na faida.
Waziri Mzee alisema tayari amekwishaagiza
watendaji wa Wizara ya Fedha kwenda kupitia hesabu za kampuni ya ZAT ili
kujua faida waliyoipata kwa muda wa miaka 16, ili SMZ ijue inaidai
kampuni hiyo kiasi gani cha fedha itokanayo na faida ya utoaji wa huduma
katika viwanja vya ndege.
Hata hivyo, waziri huyo alisema viongozi dhamana
wa Fedha waliopita ndiyo waliochangia kwa kiasi kikubwa kwa kampuni ya
ZAT kutolipa kodi kwa wakati kwa vile walishindwa kusimamia ipasavyo
majukumu yao.
Alisema baada ya kukabidhiwa Wizara ya Fedha mwaka
2010 alilazimika kumwita Mwenyekiti wa Kampuni ya ZAT, Mohamed Raza
Dharamsi ambaye pia Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Mkoa wa Kusini Unguja,
na kumtaka aeleze ni kwa nini kampuni yake imekuwa haiilipi serikali
gawio la asilimia 5 na kuikosesha mapato SMZ.
Aidha, alisema baada ya kuanza kufuatilia, SMZ
imefanikiwa kukusanya Sh890 milioni kutokana na kumpa siku tano Raza
kuhakikisha analipa gawio la Serikali na awamu ya kwanza ZAT ililipa
Sh400milioni na baadaye Sh450 milioni na kuwataka watendaji kuangalia ni
kiasi gani bado kinadaiwa katika miaka 16 mbali na kiwango
kilicholipwa.
Waziri Mzee alisema kati ya fedha hizo gawio la
Serilali alilipa Sh440 milioni ikiwa ni kuanzia mwaka 2012 hadi 2013 na
kodi nyinginezo Sh450 milioni huku akiwahimiza watendaji kupitia kwa
umakini hesabu zote za miaka ya nyuma bila kungoja.
Post a Comment