Kuwa na makazi ni moja ya mahitaji muhimu
ya binadamu, kwa kutambua hilo Serikali imekuwa ikifanya jitihada
mbalimbali kuwawezesha watumishi wake na wananchi kwa jumla kupitia
mashirika mbalimbali, waweze kumiliki nyumba hata kwa njia ya mkopo.
Kumekuwa na miradi mingi ya ujenzi wa nyumba
mbalimbali zikiwamo za ofisi na makazi, ikitekelezwa chini ya Mfuko wa
Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika
ya Umma (PPF) na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Mingine ni Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa
Serikali (GEPF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) pamoja na
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Miezi minne iliyopita Serikali imeanzisha kampuni
maalumu iitwayo Watumishi Housing Ltd (WHC), ambayo imepewa jukumu la
kusimamia mpango mahususi wa kujenga nyumba 50,000 ambazo itawakopesha
kwa masharti nafuu watumishi wa umma, ikiwa na lengo la kuwajengea
maisha bora.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa WHC, Dk Fred Msemwa
anazungumzia hatua hiyo ya Serikali, akisema kuwa mpango huo unaanza
kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu mkoani Dodoma katika eneo la Njedengwa.
“Serikali inatambua uhusiano wa karibu kati ya
kuwa na makazi bora kuwa na afya, kupata fursa za kiuchumi ikiwamo
mikopo, hivyo WHC inajisikia fahari kutimiza ndoto ya watumishi wa umma
kuwawezesha kumiliki makazi,” anasema Dk Msemwa.
Anafafanua kwamba WHC inajenga na kuuza nyumba za
aina mbalimbali kwa lengo la kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja,
kulingana na mahitaji kwa kuwa zipo nyumba za chumba kimoja, viwili na
vyumba vitatu.
Dk Msemwa anassema pia zipo nyumba zilizoungana au
(semi-detached), zilizo pekee (detached) na zile za ghorofa, ambazo
zote zinazojengwa kwa kuzingatia utamaduni wa Mtanzania na maendeleo
katika mtindo wa maisha ya vijana.
Anabainisha kwamba pia mpango huu wa kuwezesha
wananchi kumiliki nyumba umeanza na watumishi wa umma na baadaye
utahusisha wananchi wote kwa mkopo ambao unatofauti na aina hii iliyopo
katika soko, kwani mingi inaishia miaka 10-15 na michache sana inafika
miaka 20.
“Kampuni imepewa jukumu la kuwa mtekelezaji mkuu
wa Mpango wa Taifa wa Makazi kwa Watumishi wa Umma, kwa kuwa imebainika
watumishi wengi wa serikali, wamekuwa wakikumbana na vikwazo
wanapojitokeza kwenda kuomba kukopeshwa nyumba, kutokana na kushindwa
kumudu masharti yaaliyowekwa,” anasema.
Post a Comment