0
Urasimishaji biashara, yaani kuifanya biashara itambulike kisheria, ni hatua muhimu sana katika maendeleo ya biashara na taifa kwa ujumla, ingawa wajasiriamali wengi hawajarasimisha biashara zao kwa kuwa baadhi yao hawajua hatua mbalimbali zinazotakiwa kufuatwa.
Kitendo cha wajasiriamali hao kutojua namna ya kurasimisha biashara zao kinaashiria mambo mengi ikiwa ni pamoja na kasoro za mfumo wetu wa elimu ya msingi hadi vyuoni katika kuwaandaa vijana kwa ajili ya maisha ya baadaye nje ya mfumo wa kuajiriwa, na kushindwa kwa mamlaka husika katika kutoa elimu na vishawishi kwa wajasiriamali juu ya urasimishaji wa biashara zao.
Kabla ya kuanza kuelezea hatua hizo hatuna budi kukiri kuwa kila mfanyabiashara huwa na malengo yake kibiashara na hatua anazochukua mara nyingi huwa zinaendana na malengo yake kibiashara.
Haiyumkiniki kuwa na wajasiriamali ambao wangependa biashara zao ziwe na majina yanayotambulika kisheria kama vile “Hope Publishers” na kuna baadhi yao wangependa biashara zao ziwe na majina yao waliyopewa na wazazi wao kama vile “Masawe Kinabo,” yasiyotambulika kama majina ya biashara kisheria.
Kwa mjasiriamali ambaye angependa kuwa na jina la biashara ambalo linatambulika na kulindwa na sheria ya nchi, anatakiwa kuanzia BRELA au katika ofisi za mabaraza/mamlaka za biashara zilizo karibu na mhusika ambako atapewa fomu maalumu na kuijaza na wao kuiwasilisha BRELA.
Ili kuhakikisha kuwa jina la biashara halifanani na majina mengine ambayo yameshatumika sharti lifanyiwe uchunguzi ama kwa mjasiriamali mwenyewe kupitia tovuti ya BRELA na kisha kupeleka BRELA kwa ajili ya uthibitisho ama kupeleka moja kwa moja BRELA ambapo hufanyiwa uchunguzi na kwa kawaida zoezi hili ambalo hugharimu kiasi cha shilingi 6,000/= hukamilika ndani ya siku saba au zaidi kulingana na hali halisi ya utendaji kazi pamoja na matatizo mengine yenye kuhusiana na mwombaji.
Baada ya kupata cheti cha jina la biashara, mjasiriamali anatakiwa kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuomba namba ya mlipa kodi (TIN), ambapo hupewa fomu mbili za kujaza; fomu maalumu ya TRA kwa ajili ya kuijaza yeye mwenyewe na barua ambayo inatakiwa kujazwa na mwenyekiti wa mtaa kama uthibitisho wa kufanya biashara katika eneo husika. Kwa wale ambao wanaona biashara yao haihitaji kuwa na jina la biashara kutoka BRELA, wanaenda moja kwa moja Mamlaka ya Mapato Tanzania ambako hupewa fomu mbili; fomu maalumu ya TRA kwa ajili ya kujazwa na mhusika mwenyewe na barua ambayo hujazwa na mwenyekiti wa mtaa kama uthibitisho wa kufanya biashara katika eneo husika, na urejeshaji wa fomu hizo huambatana na mkataba wa upangaji wa mahali anapofanyia biashara.
Kama mjasiriamali tayari ana namba ya mlipa kodi ya leseni ya gari/udereva, anatakiwa kujaza namba hiyo kwenye fomu husika akiambatanisha na cheti/leseni kivuli cha namba husika na kupeleka TRA kwa ajili ya uthibitisho na kuipa matumizi mengine ya biashara binafsi.
Baada ya kupata namba ya mlipa kodi, mjasiriamali anatakiwa kwenda mamlaka za halmashauri za wilaya/mji/manispaa/jiji kwa ajili ya kuomba leseni ya biashara akiwa na kivuli cha cheti cha mlipa kodi kutoka mamlaka ya mapato ya TRA, mkataba wa upangaji wa mahali anapofanyia biashara na nakala mojawapo ya kivuli cha kitambulisho cha uraia/kupigia kura au udereva, ambapo atapewa fomu ya kujaza yenye maelezo ya aina za biashara na masharti ya kupata leseni, na baada ya hapo maofisa biashara wa mamlaka husika hujiridhisha na kutoa leseni.
Mwandishi wa makala ni mtaalamu wa ujasiriamali.

Post a Comment

 
Top