Siku hizi ukipita mitaani katika mikoa mbalimbali si jambo la
ajabu kusikia na kusoma matangazo yanayoelekeza mahali fedha chakavu
zinaponunuliwa.
Tangazo moja linalotoka katika kipaza sauti
kilichopo stendi ya mabasi ya daladala ya Mbagala Rangi Tatu, wilayani
Temeke linasema: “Tunauza dawa ya kuua panya, inzi na mende, pia
tunanunua hela mbovu, mia tano, elfu moja na dola, tunanunua”.
Ingawa tangazo hilo linataja bidhaa aina tofauti,
linanivutia kusogea karibu na kuzungumza na mnunuzi wa fedha hizo, John
Kiduko anayesema watu wengi wana fedha zilizochakaa, wanaziweka nyumbani
wakidhani thamani yake imekwisha.
Anaeleza kuwa tangu aanze kununua fedha chakavu
watu wengi wamejitokeza na kushukuru kuwa kumbe kuna watu wanaonunua
fedha zilizochakaa.
Huku akiamini mimi ni mmoja wa wateja wake,
anavuta droo yenye fedha alizozinunua na kunionyesha, kisha anatoa
maelezo ya namna kila moja ilivyochakaa.
“Hela zenyewe ziko hivi, nyingine bado mpya kabisa lakini zimechanika,” anasema.
Mfanyabiashara mwingine, Victor Asenga anasema kwa
siku ananunua noti za Sh500 nyingi zaidi ikilinganishwa na aina
nyingine za fedha.
Ananionyesha fedha alizonunua, na nabaini kuwa
pamoja na kuchakaa pia zipo ambazo zimepakwa rangi, mafuta na nyingine
zikiwa na mabaki ya damu.
“Tunanunua hela mbovu kama hizi (ananionyesha
Sh500 iliyochakaa lakini haijachanika). Sharti letu sisi tunanunua noti
ambayo bado namba zake zinaonekana, kama imefutika sana basi hiyo
haitufai,” anasema.
Ninapomuuliza kwa nini noti za Sh500 zilizochakaa
ndiyo nyingi zaidi, anasema: “Sina jibu kamili, nadhani ndizo zilizo
nyingi mikononi mwa watu, kama siyo hivyo basi kutakuwa na sababu
nyingine.”
Mtandao wa biashara
Naye, Elia Lyimo anayefanya biashara hiyo na ya
kuuza chenji kwa makondakta wa daladala, anasema kazi hiyo wamepewa na
mtu anayemtambulisha kwa jina la ‘bosi’ wao ambaye hupita kila baada ya
wiki moja kukusanya fedha hizo na kuzipeleka Benki Kuu ya Tanzania
(BoT).
“Kuna jamaa mmoja anayefanya kazi Benki Kuu ndiye aliyetupa kazi
ya kununua fedha mbovu, huwa anakuja kuzikusanya na kuondoka nazo,”
anasema Lyimo.
Waziri alonga
Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya anasema
kuwa wafanyabiashara kupita mitaani na kukusanya fedha chakavu siyo
kosa, tatizo ni kuzinunua noti hizo kwa punguzo la asilimia hamsini.
Pia anasema wafanyabiashara hao siyo mawakala wa
Benki Kuu, hivyo anawataka wananchi wenye fedha zilizochakaa kuzipeleka
wenyewe benki.
“Ingekuwa busara zaidi kama wananchi wenyewe
wakafika Benki Kuu au kwenye benki za biashara kubadilisha hizo fedha.
Kimsingi hizo zina thamani sawa na zile zilizochakaa,” anasema.
Tamko la Benki Kuu
Katika taarifa yake kwa gazeti hili, Benki Kuu ya
Tanzania (BOT) inasema kuwa huduma ya kubadilisha noti chakavu hutolewa
bure na benki hiyo kwa sharti kuwa anayepeleka noti anarudishiwa fedha
kwa thamani ile ile.
Mkurugenzi wa huduma za kibenki wa benki hiyo,
Emmanuel Boaz anasema hawana madalali wa kununua noti chakavu na
kusisitiza kwamba biashara hiyo kimsingi siyo halali.
“Wananchi walio na taarifa za biashara
inayoendelea kinyume na utaratibu huo ni vyema wazitaarifu ofisi za
Benki Kuu au kuzipeleka kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria
zichukuliwe,” anaeleza.
Pia anasema kuwa ubadilishaji wa noti chakavu
hufanyika makao makuu Dar es Salaam na katika matawi yake yaliyoko
Mwanza, Mbeya, Arusha na Zanzibar.
Sababu za noti kuchakaa
Mfanyabiashara wa muda mrefu katika Soko Kuu la
Kariakoo, Uswege Mwambambe anasema moja ya sababu zinazofanya noti
nyingi kuchakaa haraka ni pamoja na tabia ya baadhi ya watu kupenda
kuzifunga kwenye nguo na kuzishika kwa mikono michafu.
“Nimekuwa nikipokea noti ambazo zimekunjwa vibaya sana, nyingine
hazijachanika lakini zimechafuka kwa mafuta au hata damu, hasa
zinazotoka buchani kwa wauza nyama,” anasema na kuongeza:
“Baadhi ya watu hawana nidhamu kabisa ya kutunza
fedha, fikiria kwamba kila siku unapokea noti moja iliyochorwa au
kuchanwa kwenye pembe, kuna noti ngapi za aina hiyo nchi nzima?”
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitivo cha Biashara cha
Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Deogratius Massawe anasema baadhi
ya watumiaji wa dawa za kulevya wanachangia kuharibu noti kwa kuchomoa
uzi wa usalama kwa minajili ya kwenda kuutumia katika uvutaji wa unga.
“Mateja huchomoa ule uzi unaowekwa kwenye noti na
kuuchanganya na vitu vingine kwa ajili ya kuvutia unga. Hii ni tabia ya
muda mrefu na inaharibu sana fedha,” anasema.
Anaongeza kuwa hali hiyo inapaswa kukomeshwa mara moja kwani inaharibu mwelekeo wa kiuchumi wa Taifa.
Post a Comment