Serikali na taasisi mbalimbali za kilimo zimekuwa zikifanya utafiti wa kilimo na mazao kwa lengo la kuboresha kilimo nchini.
Hata hivyo inaonekana kwamba wakulima hasa wadogo
wamekuwa hawashirikishwi kwenye hatua za awali za utafiti na kusababisha
kupatikana kwa majibu au taarifa ambazo siyo sahihi baada ya utafiti
kukamilika.
Matokeo ya kutoshirikishwa kwa wakulima wadogo ni kuwapo kwa upungufu wa chakula nchini na umaskini.
Utafiti uliofanywa na taasisi iitwayo Eastern
& Southern Africa Farmers’ Forum (ESAFF) kuhusu maendeleo ya kilimo
na mbegu nchini ikiwalenga wakulima wadogo, ulibaini kwamba wakulima hao
hawashirikishwi kwenye utafiti licha ya kuwa ni kundi muhimu kwenye
sekta hiyo.
Vilevile utafiti huo ulibaini idadi ya kampuni
zinazofanya biashara ya mbegu nchini, zimekuwa zikiongezeka tangu mwaka
2005, lakini wakulima wamekuwa hawafikiwi na huduma hiyo. Mwaka 2005
kulikuwa na kampuni 16, lakini sasa zimeongezeka na kufikia zaidi ya 55
wakiwamo wafanyabiashara mbegu za kilimo.
Wadau kilimo nchini, wanaamini kwamba endapo
wakulima watashirikishwa kwenye utafiti, ni rahisi watafiti kubaini
mahitaji yao na kutekeleza ushauri wa kiutaalamu unaotolewa na watafiti.
Mdau kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua),
Dk Damian Gabagambi anasema watafiti wamekuwa hawatengi muda wa kutosha
kwa ajili ya kuwashirikisha wakulima wadogo kwenye tafiti mbalimbali na
matokeo yake wamekuwa hawatekelezi ushauri wa kitaalamu unaotokana na
tafiti zao.
“Kwa mfano, wilayani Mbozi, wakulima walikataa
mbolea waliyopelekewa na Serikali kwa kuwa hawakuelimishwa umuhimu wake
ingawa utafiti ulibaini kwamba mbolea hiyo ilikuwa nzuri kwa wakulima wa
wilaya hiyo,” anasema Dk Gabagambi.
Dk Gabagambi anabainisha kuwa serikali ilipata
hasara kwa kuwa mbolea hiyo haikutumika na pia fedha zilizotumika kwa
ajili ya kuandika ripoti ya matokeo ya matumizi ya mbolea hiyo,
zilipotea.
Anasema kutokana na wakulima wadogo kutoshirikishwa kwenye tafiti za kilimo, imekuwa vigumu kutekeleza mpango wa Kilimo Kwanza.
“Tulifanya utafiti hivi karibuni kuhusu mbolea.
Moja ya mambo tuliyobaini katika bajeti ya 2012/13, ni kwamba asilimia
40 mpaka 70 ya mbolea ya ruzuku ilisambazwa kwa wakulima vijijini,”
anasema Dk Gabagambi.
“Kama wakulima wakishirikishwa ipasavyo katika
mpango wa Kilimo Kwanza wangehoji kwanini pembejeo hazikuwafikia
vijijini, anasema Dk Gabagambi. Lakini hawahoji kwa kuwa wanaamini
Kilimo Kwanza ni mpango wakulima wakubwa hasa wafanyabiashara.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Wakulima Wadogo
mkoani Morogoro, Marcelina Kibena anasema wakulima wadogo wamekuwa
hawashirikishwi katika tafiti.
“Kwa mfamo, hivi sasa wakulima wanaamini kuwa
Kilimo Kwanza kilianzishwa na wafanyabiashara kwa ajili ya kupata soko
la uhakika huku serikali ikiamini wakulima wadogo ni watekelezaji wa
matokeo ya utafiti na kusahau kwamba haikuwashirikisha katika hatua za
awali,” anaeleza Kibena.
Makamu mwenyekiti huyo anasema pia wakati wa
kutunga sera za kilimo, wakulima wadogo wamekuwa hawashirikishwi na
badala yake wamekuwa wakiambiwa watekeleze sera hizo.
Vilevile anasema serikali imekuwa ikifanya makosa kwa kuongeza bei ya pembejeo huku maisha ya wakulima yakindelea kuwa magumu.
“Mbali ya taarifa za serikali, maisha ya wakulima
hayajabadilika, maisha yetu yako palepale, naamini mambo yatabadilika
kama wakulima watashirikishwa kwenye tafiti.
“Ukitaka kujua mpango wa Kilimo Kwanza umewalenga
wafanyabiashara na siyo wakulima, angalia jinsi kampuni mbalimbali
zinavyouza pembejeo za kilimo.
“Hawa wafanyabiashara wameweka mikakati ya
kuwalazimisha wakulima kununua mbegu zao, kila mwaka huku serikali
ikisahau kwamba kuna mbegu za asili ambazo zinaweza kutumika,” anaeleza
Kibena.
Kwa mtazamo mwingine, Kibena anasema wakulima
wamekuwa hawajui umuhimu wa tafiti zonazofanyika kutokana na watafiti
kutembelea maeneo vijijini bila kuchukua maoni ya wakulima.
Taasisi ya Mbegu nchini (TASTA) ambayo
inawakilisha kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya mbegu, imekuwa
ikishindwa kudhibiti vikwazo vinavyokabili sekta ndogo za kilimo nchini,
hivyo tatizo hilo linapaswa kutatuliwa.
Post a Comment