0
Watanzania tumekuwa wepesi mno kulalamika na kutaka maendeleo wakati huohuo tunashiriki kwa kiasi kikubwa katika kukwamisha juhudi hizo za maendeleo.
Kila siku kumekuwepo kelele za matatizo na kero mbalimbali ambazo tumekuwa tukiinyooshea kidole serikali bila kujua kuwa sehemu kubwa ya matatizo hayo inasababishwa na sisi wenyewe.
Mfano mzuri katika hili ni tatizo la foleni katika barabara nyingi hususani jijini Dar es salam chanzo kimoja wapo kikiwa ni biashara ndogondogo na shughuli zinazoendelea kandokando ya barabara hizo.
Awali ilikuwa ikionekana katika baadhi ya maeneo hususani, Kariakoo lakini siku hizi biashara za kandokando ya barabara zinaonekana kukithiri katika maeneo mengi ya jiji.
Ukipita maeneo ya Buguruni, Ilala, Mbagala, Mwenge, Kigogo, Manzese, Ubungo na sehemu nyingine ni jambo la kawaida kabisa kukuta wafanyabiashara wakiwa wameingia kabisa katika hifadhi ya barabara na kuendesha shughuli zao.
Katika kituo cha daladala cha Mwenge na Ubungo tatizo hili linaonekana kuwa kubwa zaidi kwani uwingi wa biashara katika maeneo hayo huchangia msongamano mkubwa wa magari na watu, hali inayosabisha pia ongezeko la wizi na vitendo vya kihalifu.
Nyakati za usiku, hali huwa mbaya zaidi kwa kuwa wafanyabishara wengi hujitokeza nyakati hizo kuwinda wateja kwa lengo la kukwepa ushuru mchana hivyo kusababisha msongamano mkubwa.
Mbaya zaidi kuna wakati bidhaa hizo huangukia barabarani hivyo muuzaji kulazimika kuziokota wakati huohuo magari yakiendelea kupita, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kusababisha foleni.
Pamoja na kusababisha foleni, hali hii inaweza pia kuhatarisha maisha ya wafanyabiashara na hata wateja wanaofika katika maeneo hayo kununua bidhaa.
Suala hili linaweza kuonekana la kawaida, lakini kwa kiasi kikubwa linaweza kusababisha madhara makubwa kiuchumi na hata kupoteza nguvu kazi ya taifa kutokana na ajali ambazo zinaweza kusababishwa na biashara hizo.
Licha ya mara kadhaa serikali kupiga marufuku ufanyaji wa biashara katika maeneo hayo bado zimekuwa zikiendelea na kushamiri kwa kasi kana kwamba zinaruhusiwa kisheria.
Hata inapojaribu kuchukua hatua zaidi na kuwaondoa katika maeneo hayo wamekuwa wakipotea kwa siku chache lakini baadaye hurudi na kuendelea na shughuli zao kama kawaida.
Inawezekana kabisa wahusika wakawa wanafanya hivi wakidhani wanaikomoa serikali lakini ukweli ni kwamba hata wao wanahatarisha maisha yao na biashara zao kwa ujumla.
Endapo gari litapita kwa mwendo kasi na kuharibu biashara au mfanyabiashara sidhani kama serikali itakuwa inahusika kwa namna yoyote ile hivyo mhusika atakuwa ameingia katika hasara ambayo ingeweza kuzuilika.
Tumekuwa tukisifu nchi za watu wapo makini katika miji yao ndiyo maana inaonekana vizuri tunapoona kwenye runinga au wale waliopata bahati za kwenda huko lakini hatuwezi kufanikiwa kufikia hali hiyo kama hata tunashindwa kukomesha biashara katika maeneo yasiyostahili.
Nasema hivyo kwa kuwa tumekuwa tukitamani kwa kiasi kikubwa kupata maendeleo bila kushiriki kwa namna yoyote ile katika kufanikisha hilo.
Lakini tukishirikiana kwa pamoja tunaweza kulimaliza kabisa tatizo hili na kulifanya Jiji la Dar es salaam kuwepo katika mazingira yanayostahili ukilinganisha na miji mingine mikubwa Afrika na duniani kwa jumla.

Post a Comment

 
Top