Tembo waliopo katika moja ya hifadhi nchini Tanzania. Picha na Maktaba
Kwa hali ilivyo sasa, inatabiriwa kuwa baada ya miaka saba, kama
jitihada hazitafanyika, tembo watatoweka katika ardhi ya Tanzania.
Inakadiriwa kuwa kwa siku, katika mbuga mbalimbali nchini tembo wapatao 30 huuawa kwa ajili ya kupata meno yao.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuwalinda Tembo (TEPS),
Alfred Kikoti anasema kwa kasi hii, ifikapo mwaka 2020 Tanzania
haitakuwa na tembo hata mmoja katika mbuga zake.
Biashara ya pembe za ndovu inaripotiwa kushamiri katika Bara la Afrika, hali inayohatarisha kupotea kwa viumbe hao duniani.
Inaelezwa kuwa ujangili hufanyika kwa njia
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vikundi vya waasi katika nchi zenye
machafuko, kuendesha biashara hiyo na baadhi ya watu waliopewa vibali
maalumu vya uwindaji kutumia mwanya huo kufanya ujangili.
Ujangili unaripotiwa kuwa tishio katika sekta ya
utalii, kutokana na idadi kubwa ya tembo kuuawa kila mwaka. Sekta hii
imekuwa ikichangia kiasi kikubwa katika pato la taifa na wanyamapori
pekee wamekuwa kivutio kikubwa cha utalii.
Inakadiriwa kuwa mwaka 2013, uwindaji halali
uliingizia Tanzania Dola 50 milioni za Kimarekani ambazo ni wastani wa
Sh900 bilioni). Hii inafafanuliwa kuwa, zaidi ya asilimia 90 ya mapato
ya sekta ya utalii yanatokana na wanyamapori.
Kuongezeka kwa kasi ya ujangili nchini kunaelezwa
kusababishwa na vitendo vya rushwa, matumizi mabaya ya madaraka na
kuwapo mfumo dhaifu wa usimamizi wa sheria katika Wizara ya Maliasili na
Utalii.
Ripoti hiyo linayoitwa ‘Ivory’s Curse: The
Militarization and Professionalization of Poaching in Africa’, inaeleza
kuwa tangu mwaka 2000, wizara hiyo imetawaliwa na kashfa za rushwa mpaka
kusababisha zilzosababisha mawaziri na watendaji wakuu kujivua au
kuvuliwa nyadhifa zao.
Taasisi ya Kimarekani ya Utunzaji Wanyamapori ya
Born Free USA, kwa ushirikiano na Shirika la Ripoti za Kichambuzi na
Takwimu la C4ADS, wamefafanua katika ripoti hiyo jinsi vikundi
mbalimbali vya waasi barani Afrika wanavyoendesha shughuli za ujangili.
Tanzania inaelezwa kuwa na mfumo mbaya wa
usimamizi wa sheria katika kuwasimamia watu wenye vibali vya uwindaji.
Pia, wanaangazia jinsi ujangili unavyofanywa kwa ustadi na watu wenye
mtandao mkubwa kimataifa wa kuendesha biashara ya pembe za ndovu
duniani.
Nchi nyingine zilizotajwa kuathirika zaidi na
ujangili barani Afrika ni Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Cameroon, Msumbiji, Kenya na Zimbabwe.
Hali ya ujangili nchini
Ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi ya tembo katika
Hifadhi za Selous na Mikumi kwa mwaka 1976, ilikuwa ni 109,419, lakini
mwaka 2009, idadi hiyo ilishuka mpaka kufikia tembo 38,975.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Frankfurt
Zoological Society mwishoni mwa mwaka 2013, inaeleza kuwa ni tembo
13,084 wanaokadiriwa kubakia katika hifadhi hizo, sawa na upungufu wa
asilimia 66 katika kipindi cha miaka minne.
Hii imefafanuliwa kuwa zaidi ya tembo 25,000
waliuawa katika hifadhi ya Selous ndani ya miaka minne pekee. Pia
inabainisha upungufu wa tembo katika Hifadhi ya Ruaha-Rungwa kutoka
tembo 35,461 mpaka tembo 20,090 sawa na upungufu wa asilimia 36.5
kuanzia mwaka 1990 mpaka sasa.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa mwezi huu nchini Kenya,
inaitaja Tanzania kama kitovu cha usafirisha wa pembe za ndovu katika
ukanda wa Afrika Mashariki na Bandari ya Dar es Salaam inaongoza
ikifuatiwa na Mombasa.
Kutoka mwaka 2008 mpaka 2013, inaelezwa zaidi ya
tani 20 za pembe za ndovu zilikamatwa zikisafirishwa au kuingizwa katika
Jiji la Dar es Salaam. Hii ni kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya C4ADS
iliyokuwa ikiripoti juu ya pembe za ndovu zilizokamatwa, Dar es Salaam
kuwa ya pili baada ya Mombasa.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa uchunguzi wa vinasaba
(DNA) ulifanywa katika tani 11 za pembe za ndovu zilizokamatwa Taiwan,
Japan na Hong Kong mwaka 2006, ilibainika kuwa pembe 1500 zilitoka
Tanzania katika Mbuga ya Selous.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa vinasaba vya pembe
hizo vilifanana, hali iliyoleta hisia kuwa baadhi ya watu wamekuwa
wakiwinda katika hifadhi hiyo mara kwa mara katika utaratibu maalumu
unaotambuliwa na Serikali.
Ripoti inaonyesha kuwa kuna udhaifu mkubwa katika
usimamizi wa uwindaji halali, kwani wawindaji wenye vibali hawasimamiwi
ipasavyo kufanya taratibu zilizowekwa kisheria, hali inayowafanya
kutumia nafasi hiyo kufanya vitendo vya ujangili.
Kuhusu vitalu vya uwindaji, ripoti inaonyesha kuwa
zoezi la utoaji vibali limekuwa likifanyika kwa usiri mkubwa, jambo
linalodhaniwa kutoa nafasi ya rushwa katika uwindaji huo. Pia taasisi za
kusimamia sheria zinatajwa kutokuwa na njia madhubuti za kusimamia
zoezi hilo, jambo inayolirudisha nyuma taifa.
Tuhuma za rushwa wizarani
Ripoti hiyo inawataja baadhi ya waliokuwa mawaziri
na wakurugenzi mbalimbali wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuhusika
katika kulisababishia taifa hasara kubwa na kushindwa kusimamia
kikamilifu udhibiti wa vitendo vya ujangili nchini.
Ripoti inasema wakurugenzi watatu kati ya watano waliokuwapo
Wizara ya Maliasili, ikiwajumuisha Wakurugenzi wa Wanyamapori na Misitu,
ama waliondolewa kazini au kushushwa vyeo kutokana na utendaji mbaya
katika idara zao.
Inaeleza kuwa wizara ilijawa kashfa za rushwa,
hali iliyosababisha Norway kuacha kutoa msaada katika Mpango wa
Mabadiliko ya Tabia ya Nchi. Ilibainika kuwa kulikuwa na ubadhirifu wa
mabilioni ya fedha za mpango huo.
Mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili ilifichua
‘madudu’ yaliyofanywa na watendaji waliotumwa kuwakamata watuhumiwa wa
ujangili nchini.
Vitendo viovu vilivyofanywa na watendaji hao,
vinatajwa kuwa kikwazo katika vita hiyo kwani vilisababisha Serikali
kusitisha zoezi hilo hali ambayo inatajwa kuchangia ongezeko la vitendo
vya ujangili nchini.
Idara ya Wanyamapori yazungumza
Akizungumzia udhaifu katika usimamizi wa wawindaji
halali, kaimu mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Paul Sarakikya
alisema siyo kweli kwamba wawindaji halali huachwa bila usimamizi
wowote, kwa sababu wana mifumo ya kusimamia zoezi hilo.
Sarakikya alisema idadi ya tembo inazidi kuongezeka katika hifadhi nchini, tofauti na upungufu unaoelezwa katika ripoti hiyo.
“Sikubaliani na ripoti hiyo, tumeshaongea sana juu
ya suala hili. Rais (Jakaya Kikwete) alishalizungumzia na waziri pia
alishaliongelea. Ufafanuzi ndio huo, hamna ukweli wowote katika ripoti
hiyo,” alisisitiza Sarakikya.
Mkurugenzi huyo alihoji kuwa kama hakuna usimamizi
madhubuti katika uwindaji halali, wamewezaje kusimamia zoezi hilo miaka
yote mpaka idadi ya tembo inaongezeka tofauti na ilivyokuwa miaka ya
nyuma?
Juhudi zinazofanywa na Serikali
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Bunge
la Bajeti la 2013/14 ilisema imeimarisha ulinzi wa rasilimali ya
wanyamapori na imefanikisha kuwakamata watuhumiwa 1,215, bunduki 85 na
risasi 215 mwaka 2013.
Ilisema kesi 670 zimefunguliwa katika mahakama
mbalimbali nchini kati ya hizo, 272 zimekwisha baada ya washtakiwa 247
kulipa faini ya jumla ya Sh175 milioni na washtakiwa 71 kupewa adhabu ya
vifungo vya jumla ya miezi 1,192. Kati ya hizo, kesi 398 zenye jumla ya washitakiwa 897 bado zinaendelea
katika mahakama mbalimbali nchini. Pia Serikali ilikamata nyara zenye
thamani ya Sh 855.1 milioni.
Post a Comment