Mtu chake. Siku nikikukamata unachezea amali yangu
sitakuvumilia. Baada ya kuhakikisha nimeshaikomboa amali hiyo,
nitakuburuza hadi kwenye mamlaka zilizopewa jukumu la kunilinda mimi na
mali zangu. Nitafanya hivyo ili wakakukumbushe kuwa cha mtu mavi,
ukiogope kama homa ya dengue!
Nikukute unampiga longolongo Bibi Mlevi hakyanani
ntaku... sijui nitakufanyaje. Najua kuwa akili zitanihama nisijue
ninachokifanya wakati huo. Hata kama nitaharibu, lakini nitasema ukweli
mbele ya sheria. Na iwapo ile dhana ya “mwananchi mwenye hasira kali”
itakuwa imeshaeleweka vyema, naamini nami nitakuwa salama.
Wapo watu wanaofanya mambo kwa makusudi huku
wakidai kuvurugwa. Mtu anakwiba sufuria, anapokamatwa anadai kavurugwa
na njaa! Sote tunajua tiba ya njaa ni mlo; Sasa ndiyo tuseme njaa
ilipomkamata akaona akwibe sufuria ili akapikie ugali? Kama si uongo ni
kitu gani?
Falsafa ya “tiba ya njaa ni wizi” haijapata kuwapo
duniani. Kama ingalikuwapo wezi wangeiba chakula. Ni wazi kuwa wapo
wezi wa mazao shambani, lakini bado sikubali kuwa ati walisumbuliwa na
njaa. Kama ndivyo basi wangeiba nusu kilo wakapike na kula. Lakini watu
wa aina hii huvuna shamba zima wakiamini watauza kwa bei ya fasta,
watapata hela ya kutosha na watatoka kimaisha.
Ndiyo maana mimi siwezi kumwachia mtu wa namna
hii. Zamani nilikuwa nawatetea wasivishwe matairi na kupigwa moto,
lakini waliponiibia nilitia adabu. Kila mwizi namfananisha na aliiba
kwangu. Ndiyo yaleyale; kama unachekelea mke wa mwenzio kuopolewa,
subiri umfumanie wa kwako.
Wengine wanadai kuvurugwa na Serikali zao. Hawa
hawaibi sufuria, bali wanafanya uharibifu mkubwa kwenye nchi zao ili
Serikali iliyo madarakani izomewe. Wengi ni hawa tunaowaita waasi, ambao
starehe yao ni kupora mifugo, kulipua mahospitali, kubaka wajane,
kuteka mabinti na kadhalika. Yote hayo yanalenga kuzitia madoa Serikali
zao.
Mwanzoni nilidhani kuwa watu hawa wameumbwa
tofauti na wengine. Si rahisi mtu kuchukua bunduki na kumuua mama yake
na kumbaka shangazi yake. Lakini kwenye kisingizio cha “kuvurugwa”
wengine hufanya hivyo. Hapa kunasingiziwa kuvurugwa, lakini ukweli hila
ileile ya mwizi wa mahindi anayemaliza shamba ndiyo inayotokeza. Ngoja
nikufafanulie.
Hawa ni wahuni wanaokutwa bila kazi mtaani. Kwa
sababu hawana kazi wala elimu, ni rahisi kwa mababa wa vita (War
Mongers) kuwashawishi kuwa viongozi wao wanakula haki zao bure.
Wanaambiwa iwapo watashika bunduki na kuiwezesha Serikali kusalimu amri,
wote wataishi Ikulu wakipewa huduma zote hadi ya kuogeshwa. Kila mmoja
atakwenda Ulaya kama anayekwenda msalani.
Haya ndiyo unayoyasikia huko Nigeria na Afrika ya
Kati. Mababa wa vita wanazisumbua nchi zao kisha wanapeleka taarifa kwa
“mabwana” wa vita. Hawa ndiyo watengenezaji na wauzaji wakubwa wa silaha
duniani. Kule wanapata fedha na silaha na kurudi “kuendeleza mapambano”
dhidi ya ndugu zao wa damu.
Jonas Savimbi alialikwa Ikulu ya Marekani kukutana
na Rais Ronald Reagan mwaka 1986. Akapetiwa mgongoni na kusifiwa kwa
kazi nzuri. Savimbi akarudi Angola kuendeleza zengwe lake. Miaka miwili
tu baadaye alikwenda tena Washington kupewa heshima. Mpaka mwaka 1990,
Savimbi alikuwa ndiye habari kuu duniani: hakuna cha Osama wala Mullah
wakati huo.
Akafanya kosa kubwa sana. Kwanza alikubali
mazungumzo ya amani na kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu
mwaka 1992. Lakini yeye alipata asilimia 40 dhidi ya asilimia 49 za kura
za Rais José Eduardo dos Santos. Savimbi akadai kuchakachuliwa kwa
matokeo na akaingia tena msituni. Mwaka 2002 baada ya kuwa
amesharipotiwa kufa mara 15, aliuawa zaidi ya kinyama katika mapigano.
Ndiyo mwisho wao unavyokuwa. Kazi sasa inabaki kwa
waasi wanaobaki kwa sababu hakuna anayetambulika kwa wafadhili wao.
Ndiyo mwanzo wa kuishi kama gendaheka msituni wakila mizizi na matunda
pori, na pengine hata binadamu wenzao wanaoingia humo kuwinda. Kumbuka
kuwa waasi sasa hawana baba wala bwana, zile ndoto za kuishi kifalme
zinakuwa zimeshalala mbele.
Waasi wa Kiislamu nchini Nigeria, Boko Haram nao wanadai
kuvurugwa. Wao wanaitafsiri elimu ya kimagharibi kuwa dhambi. Hivyo bila
shaka jina la Rais wa Nigeria (Goodluck Jonathan) linawatia
kichefuchefu kila walisikiapo. Lakini tazama kuvurugwa kwao kunavyokuwa
kisingizio. Wao wanapokwenda kuua wanachanganya wote: Waislamu,
Wakristu, Wa dini asilia hadi Wapagani.
Ukipiga hesabu za haraka, utakuwa na uhakika kuwa
kuna bwana anayewapa fedha na silaha. Kule msituni hakuna maduka ya
silaha, na hata mipaka ya nchi yao ikifungwa bado hawataishiwa na
silaha. Nikamsikia Obama akihuzunishwa na hali ile. Akasema
“Nitahakikisha wasichana waliotekwa wanakombolewa.”
Alas! Nilikusanya magazeti yote yaliyoandika
habari ile nikidhani kuna neno limesahaulika. Hakika nilitegemea kusikia
“Nitawakamata Boko Haram, Hakyanani nitawatia adabu!” Ebu ngoja kabla
sijaendelea nihakikishe kilichosemwa na kile nilichosikia...
Post a Comment