0
Ama kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Yaani dunia ilivyokuwa ikisubiri kusikia au kushuhudia ugomvi wa Beyonce na mumewe Jay Z, leo hii unakuwa wa mtu na shemeji yake…makubwa haya!
Sitaamini ukiniambia hujalisikia sekeseke hili la mdogo wa Beyonce, Solange kumshambulia kwa mangumi na mateke shemeji yake baada ya kutoka katika tuzo za Met Galla.
Kinachoacha maswali siyo Solange kumpiga ngumi shemeji yake, kwa sababu mtu anapopandwa na hasira anaweza kufanya jambo lolote na huenda hiki kilimkuta mwanamuziki huyu.
Kinachoshangaza katika sekeseke hili ni kitendo cha Beyonce kutoingilia katika ugomvi huo, kama vile alipendezwa na sinema iliyokuwa inaonekana mbele yake.
Beyonce anajulikana kwa kujifanya mwanamke shupavu, anayempenda na kumthamini mumewe kupita kiasi, sasa suala la kusimama kama sanamu wakati mumewe akishambuliwa na mdogo wake, linaacha maswali mengi kichwani.
Wapo wanaosema Beyonce alitulia kwa sababu mdogo wake alikuwa akimshambulia Jay Z kwa kosa ambalo amemfanyia yeye.
Wazungu wanasema ‘family over everything’, yaani familia yako inakuja kwanza kabla ya kitu chochote na ndicho kilimchomsukuma Solange kumshambulia shemejiye.
Inavyoonekana Solange hawezi kukasirishwa na Jay Z kiasi cha kumshambulia kwa ngumi, isipokuwa kama amemuumiza dada yake.
Kama hiyo haitoshi, baada ya Solange kuamuliwa na mlinzi, aliondoka katika gari tofauti na aliloingia Jay Z, lakini na dada yake akamfuata na kupanda gari hilo.
Kwa maana hiyo Jay Z alikwenda peke yake nyumbani na Beyonce haifahamiki kama alirudi kwake au alilala kwa mdogo wake.
Tukirudi kwenye vitabu vya dini vinatuambia siku mnayofunga ndoa mnaungana kuwa mwili mmoja. Tafsiri yake ni kwamba katika maisha yenu mnakuwa kwanza nyinyi, watoto wenu halafu familia zenu zinafuata.
Sasa kilichomkuta Beyonce ni nini hata aache kumsaidia mumewe au kumkanya mdogo wake asiendelee na kitendo hicho?
Inawezekana Jay Z amefanya kosa kubwa sana hadi kustahili kupata adhabu hiyo, kwani hata sasa tunamwona Beyonce akitupia picha mtandaoni zinazomwonyesha akiwa na mdogo wake katika matukio mbalimbali.
Nadharia nyingine ambayo inawezekana imechangia Beyonce kusimama pembeni ni kivazi zlichokuwa amepigilia usiku ule. Huenda angeamua kwa namna yoyote kuingilia basi kigauni kile cha wavu kingefunguka halafu mapaparazi wapate stori nyingine za kuuzia magazeti mwaka mzima.
Yote kwa yote hatujasahau kilichomkuta Chris Brown alipomtwanga Rihanna, mpaka leo kuna watu hawajamsamehe kijana wa watu kwa kuwa tu alinyanyua mkono kumpiga mwanamke.
Kwa hili la Jay Z kuamua kusimama tu kupokea ngumi, mateke na matusi ambayo kwa bahati nzuri kamera za CCTV haziwezi kuyanyaka ni la kumpongeza.
Ubaya wa hadithi hii tutasubiri sana majibu bila mafanikio, kwasababu mwanamke huyu anajulikana kwa ujeuri wa kutokubali kuyazungumzia maisha yake binafsi.
Labda kwa sababu hili limeonekana wazi, huenda akakubali kufunguka kutoa sababu za kusimama pembeni wakati mdogo wake akimshambulia baba watoto wake.

Post a Comment

 
Top