0

Hussein Jumbe akiwa kazini  

Ni huzuni. Kumbi za muziki wa dansi ziko tupu. Bendi maarufu karibu zote zilizotamba miaka ya 70 na 90 zimebaki kuwa historia. Chache zilizokuwapo tunashuhudia wanamuziki wake wakipigia viti vitupu katika baa za kawaida kabisa, zilizopo pembezoni mwa jiji la Dar es salaam.
Nini kimetokea kwa muziki huu ambao unabakia kuwa alama pekee na miongoni mwa burudani ambazo Watanzania wana kila sababu ya kujivunia, kutokana na historia kuonyesha kuwa muziki huo uliasisiwa nchini Tanzania na ulianzishwa katika Jiji la Dar es Salaam zaidi ya miaka 80 iliyopita.
Kati ya wanamuziki wakongwe nchini, Hussein Jumbe aliyewahi kupigia bendi za Msondo Ngoma na DDC Mlimani Park anapingana na wanamuziki wenzake wanaoamini kuwa muziki huo unaangushwa na vyombo vya habari.
Mfano wa kuigwa kuonyesha kuwa muziki huo bado unakubalika, ni kile alichokifanya Jumbe, akiwa na bendi yake ya Talent wiki iliyopita katika Ukumbi wa Kisumba zamani Sugar Ray uliopo maeneo ya Temeke.
Jumbe alifanya uzinduzi wa albamu ya ‘Kiapo Mara Tatu’, lakini akafanya maandalizi kama ambavyo wanafanya wanamuziki wa sasa kama vile Jahazi Modern Taarabu, Twanga Pepete, Linah Sanga, Diamond Plutnamz kwa kualika watu wengine wenye mvuto wanapokuwa wanazindua albamu zao.
Kama ilivyo kawaida yake, Jumbe licha ya kuwa ni mwanamuziki wa zamani aliachana na uzamani na kuonyesha kuwa kulialia kwamba wanamuziki wa zamani hawasaidiwi siyo dawa.
Lakini kitu kilichofanya shoo hiyo ivutie zaidi na kujiweka katika soko la muziki kama wafanyavyo wanamuziki wengine, aliweka burudani tofauti tofauti ikiwamo kikundi cha muziki wa asili cha Hayahaya Ngoma Afrika kutoka Kijiji cha Makumbusho, jijini Dar es Salaam. Kama hiyo haitoshi katika kuwavutia mashabiki wa muziki wa aina zote, hakuwatenga wadau wa taarabu kwani mwanamuziki wa miondoko hiyo Isha Mashauzi alikuwapo kuwakilisha.
Cha kufurahisha ni kwamba Isha Mashauzi, akiwa na kundi zima la Mashauzi Classic hakumuangusha kwani walifanya kile mashabiki walichokuwa wanakikusudia, ikiwamo kuimba muziki wa taarabu kwa ustadi mkubwa na kuimba nyimbo za wanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ikiwamo wimbo ‘Maneno maneno’, wa mwanamuziki Ben Pol na kuuimba kwa ustadi mkubwa. Pia wimbo wa Injili wa mwanamuziki Bahati Bukuku‘ uitwao ‘Waraka wa Amani’ na nyimbo mbili za mwanamuziki Jumbe ambazo ni ‘nachechemea na ‘siri ya nini’.
Jumbe anena
Mwanamuziki huyo mkongwe alisema kuwa alichokifanya ni kusoma mahitaji ya soko la muziki wa sasa na kujua mahitaji ya wadau wa burudani na hatimaye hadi leo anapiga muziki na ana mashabiki vijana kwa wazee. “Niliwahi kusema kulalamika siyo dawa, tulijisahau miaka ya 80-90, tulijisahau na vijana wamechukua nafasi wanaifanyia kazi. Tunachotakiwa kufanya sasa ni kuhakikisha tunaurudisha muziki wa dansi kwenye chati ingawa kazi kubwa inatakiwa kufanyika, ”anasema Jumbe.
Jumbe anafafanua kuwa licha ya vyombo vya habari kuusahau muziki huo na wanamuziki wenyewe wanataka ujiuze kwa umaarufu wa zamani bila kujali dunia inazunguka na inakwenda sambamba na mabadiliko.“Hata Serikali imefanya mabadiliko, kulikuwa na Chama kimoja na sasa ni vyama vingi na muziki vivyo hivyo unatakiwa uende na kasi ya mabadiliko, ”anasisitiza Jumbe.
Jumbe ambaye wimbo wake wa ‘Kiapo Mara Tatu, ambao ndiyo umebeba jina la albamu hiyo, uliingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za Kilimanjaro Music, katika kipengele cha Wimbo bora wa Kiswahili, ingawa haukufanikiwa kupata tuzo hiyo.
Wadau wanasemaje?
Mohamed Kambangwa, anasema miongoni mwa vitu vinavyomsikitisha ni wanamuziki wa muziki huo, kutaka watukuzwe kwa yale waliyoyafanya zamani bila kufanya kipya ilihali uwezo wa kufanya hivyo wanao.
“Wanataka redio ambazo nyingi ni za biashara zipige nyimbo zao za zamani na kuacha kupiga mpya, badala ya kufanya kitu kipya ili kifufue ya zamani, “anasema Kambangwa. Mwanaidi Juma, anasema kuwa anaamini muziki wa dansi wa zamani ni bora kuliko wa sasa, lakini akiwataka wanamuziki wa muziki huo kuacha kubweteka na kulia wasaidiwe na Serikali bila kujibidisha kuhakikisha muziki wa dansi hasa usiokuwa na masebene ya Kikongo unapanda chati.
Raymond Ayoub, anasema wadau wa muziki wanachanganya muziki wa zamani na dansi, huku akifafanua kuwa muziki wa zamani ni wa bendi kama za Cuban Marimba, Moro Jazz, Kiko Kids, lakini muziki wa dansi unatakiwa uendelee kuwapo.
“Wanamuziki wa zamani wanataka kuendelea kufanya vizuri wakitumia nyimbo zile zile za zamani kama Jojina, Rangi ya Chungwa, Mama Bembeleza Mwana, Kitambaa Cheupe, nyimbo ambazo kwa sasa wanaozifahamu na kutambua thamani yake ni wachache, wanatakiwa kutunga nyimbo mpya,” anaongeza Ayoub.
Wanamuziki wa enzi za Jumbe na wanaopiga muziki wa dansi
Mwanamuziki mkongwe wa bendi ya Msondo, Saidi Mabera, anasema kuwa licha ya kufanya juhudi binafsi kama ambazo wao kama Msondo wamekuwa wakifanya, bado kuna haja ya vyombo vya habari kuwaunga mkono. Anafafanua kuwa Jumbe anafanya vizuri, lakini kwa siku ni mara ngapi nyimbo zake zinapigwa redioni, kibaya zaidi redio nyingi katika vipindi vyao wanataja nyimbo ambazo wanataka ziombwe.
“Katika kipindi mtangazaji anasema nyimbo ambazo ni ruhusa kuziomba kwa siku hiyo na ukiomba nyingine kati ya hizo haitakuwapo. Sasa kwa watangazaji wa sasa unafikiri kuna ambaye atataja nyimbo ya Msondo, Sikinde, kama siyo za kizazi kipya anazozifahamu, ”anasema na kuhoji Mabera ambaye amefanya kazi na bendi hiyo kwa miaka zaidi ya 40. Hassan Rehani Bichuka kiongozi wa bendi ya Sikinde, anaanza kwa kumlaani aliyeanzisha mpango maalumu wa kuua muziki wa dansi nchini.
Anasema aliyeanzisha mpango huo alihakikisha vyombo vya habari vinausahau na kufanikiwa hatua yake ya kwanza ambayo ilikuwa muhimu sana kwenye mpango huo.
“Nipo kwenye tasnia hii siku nyingi, niamini nakwambia hata tufanye nini, kuna mtu au watu hawataki muziki wa dansi uendelee na wana nguvu za kuua na kama hakutakuwa na juhudi za kuhakikisha haufi utakufa. Sisi bado tunapambana na ndiyo maana unaona hizi bendi bado zipo licha ya kuwa nyimbo zetu hazipigwi redioni, ”anafafanua Bichuka.
Mwanamuziki kinda kutoka katika bendi ya Msondo, Hassani Moshi Junior anasema; atahakikisha muziki wa dansi haufi na ndiyo maana hakufikiria kujiunga na muziki wa kizazi kipya ambao una fedha kwa sasa, kutokana na kuutakia mema muziki huo.
Anafafanua anaziunga mkono juhudi zinazofanywa na baba zake kwa kufanya vitu vipya kila siku ili kuhakikisha wale mashabiki wao wa asili wanapata burudani.
“Mimi sikubaliani na wazo la kwamba redio hazipigi muziki huu hivyo unakufa. Kila siku kumbi zinajaa mashabiki na kila muziki ninaamini una mashabiki wake, hata hao wanaocheza Bongofleva mwisho wa siku wanakuja kusikiliza muziki na kupata burudani ya kweli kwenye muziki wa dansi, “anasema Moshi Junior ambaye ni mtoto wa marehemu Tx Moshi William aliyekuwa ni mwanamuziki wa bendi hiyo hadi anafikwa na umauti.
Salim Zahoro kiongozi wa bendi ya Shikamoo anazitupia lawama redio kwa kusema kuwa zimeupotezea muziki wa dansi ndiyo maana umekuwa kimya.
“Muziki huu uliwahi kutamba lakini kuna mtu anauua na siyo mwingine bali ni redio”anasema kwa kifupi Zahoro, aliyeanza kuimba muziki huo zaidi ya miaka 50 iliyopita akiwa na bendi ya Kiko Kids.

Post a Comment

 
Top