0

Kijana Gerard Mwambungu mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam,  

Ugonjwa wa saratani unazidi kushika kasi kila kukicha hapa nchini. Pia umegharimu maisha ya watu wengi kutokana na huo ugonjwa bado haujapatiwa tiba madhubuti.
Mbali na kugharimu maisha ya watu wengi, ugonjwa huu umekuwa tishio kutokana na gharama kubwa za matibabu zinazowagharimu wagonjwa.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Februari wakati wa maadhimisho ya Siku ya Saratani Dunia, takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, zenye ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani.
Takwimu hizo zinaeleza kuwa kila mwaka wagonjwa wapya 21,180 hugundulika. Aidha zaidi ya watu 16,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na ugonjwa huo. Kati ya wagonjwa 40,000 wanaokwenda kutibiwa kwenye hospitali maalumu, asilimia 80 ya wagonjwa hao wanafariki dunia kutokana na maradhi ya saratani.
Licha ya ugonjwa huo kugharimu maisha ya watu wengi, baadhi ya wagonjwa wanaogundulika mapema, wataalamu wa afya huwashauri wafayiwe upasuaji kwa lengo la kuondoa sehemu iliyoathirika na kuzuia usienee sehemu zingine za mwili na kuleta madhara zaidi.
Hali hiyo imemkuta kijana Gerard Mwambungu mkazi wa Manzese jijini Dar es Salaam, ambaye ameamua kupiga magoti mbele ya Watanzania akiwaomba msaada wa fedha ili aweze kupata matibabu na kunusuru maisha yake.
Mwambungu ambaye hakuwahi kutegemea kama siku moja angekumbwa na maradhi hayo, sasa nusura ya maisha yake iko mikononi kwa Watanzania.
Kijana huyo amekuwa akisumbuliwa na saratani ya ngozi kwa muda wa takriban miezi saba. Licha ya kwamba baada ya kuanza kuumwa hakufahamu kuwa ingefika hatua ya kufanyiwa upasuaji.
Mwambungu aliyekuwa mfanyabiashara wa viatu katika eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani cha Ubungo, baada ya kufanyiwa vipimo na wataalamu wa afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kugundulika na ugonjwa huo kwenye mguu wake wa kulia sasa anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Chimbuko la ugonjwa huo
Mwambungu anasema siku moja jioni baada ya mizunguko yake ya kutafuta riziki alikuwa amejipumzisha sebuleni kwake. Akiwa hana hili wala lile, akajisikia muwasho sehemu ya mguuni. Anasema kwanza aliinama na kuangalia ule muwasho kama ni mkwaruzo alioupata akiwa kwenye mizunguko ya siku ile au la.
Hata hivyo Mwambungu anasema haukuwa mkwaruzo kama alivyodhania bali kilikuwa ni kipele, kitu ambacho hakikumtia hofu, kwani haikuwa mara ya kwanza kutokewa na kipele mwilini mwake, basi akajikuna usiku ukapita
Kesho yake anasema aliamka mapema kama ilivyo kawaida yake kwenda kwenye biashara ya kuuza viatu kama ilivyokawaida. Lakini siku hiyo kile kipele kilimnyima raha kabisa. “Nilivyoanza kukikuna ule usiku ilikuwa kama nimekichokoza…Siku iliyofuatia kilikuwa kinawasha sana, ilikuwa kero kwangu,” anasema Mwambungu na kuongeza kuwa hali hiyo iliendelea kwa muda wa siku kadhaa na kadiri kilivyoendelea kukikuna kilizidi kukua.
“Mimi nilikuwa nashaangaa siku zilivyozidi kusonga, muwasho ukawa unazidi kuongezeka kwenye kipele halafu kikawa kinaendelea kuwa kikubwa mithili ya jibu,” anasema kijana huyo na kuongeza kuwa hali ilivyobadilika ilimsababishia maumivu makali kwenye mguu.
Kutokana maumivu hayo kwenye mguu anasema wakati mwingine alilazimika kushinda nyumbani tu bila kufanya kazi yoyote kutokana. Baada ya mwezi kupita alivyoona hali inazidi kuwa mbaya bila ya unafuu anasema aliona ni vyema akitumia dawa za maumivu angalau aweze kuendelea na shughuli zake za kujiingizia kipato.
“Panadol na diclopar zilikuwa kama sehemu ya chakula changu…Nilikuwa bora nisile chakula lakini ni hakikishe nina pesa kwa ajili ya hivyo vidonge kwa ajili ya kutuliza maumivu makali niliyokuwa nanyasikia kwenye mguu.” Anasema na kuongeza kuwa dawa hizo hazikuwa na msaada sana.”Wakati huo na kipele, kimekuwa jipu, jipu likazaa kidonda.”
“Haikuwa kama jipu tena…Kilizidi kukuwa kidonda kikubwa kikawa kinasambaa kwenye sehemu ya goti kwenda juu,” anasema Mwamungu huku akionyesha jinsi kipele kilivyokuwa siyo kipele tena bali kidonda kikubwa. Mbali na kuwa hivyo sehemu ya goti hadi kuelekea katikati ya paja kumepata uvimbe uliosababisha mishipa ya goti kutuna ambayo pia inamsababishia maumivu makali. Kijana huyo ambaye hivi sasa anaishi kwa kutegemea msaada wa chakula kutoka kwa wasamaria wema, anasema alipoona kuwa hali inazidi kuwa mbaya licha ya kutumia dawa za maumivu aliamua kwenda hospitali kuonana na wataalamu wa afya kwa ajili ya matibabu zaidi.
Anasema Desemba 2013 alikwenda Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu zaidi ikiwa ndiyo hospitali ya kwanza kuhudhuria kwa ajili kuonana na wataalamu wa afya.
“Nilivyofika hospitalini nilimwelezea daktari jinsi kidonda kilivyoanza hadi kufikia hapo…Baada kuchukua maelezo yote akaniandikia dawa na sindano,” anasema Mwambungu. Anasema kuwa daktari alimpa maelezo kuwa dawa hizo atatuma kwa wiki moja kwa ajili ya kutuliza maumivu na sindano itasaidia kukausha kidonda.
“Nilipomaliza dozi nilirejea hospitalini hapo lakini hali bado ilikuwa siyo yakuridhisha…Maumivu yaliendelea na kidonda kikazidi kuwa kikubwa,” anasema.
Kutokana na hali ile daktari wake alimshauri aende katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu na uchunguzi zaidi.
Anasema kuwa licha ya kuwa alitamani sana kuendelea na matibabu haraka hakuweza kwenda Muhimbili kwa wakati uleule.
“Kwa kipindi chote kile nilichokuwa sifanyi chochote, hivyo daktari alivyonishauri niende Muhimbili nililazimika kusubiri kwa muda huku nikiomba msaada kwa wasamariawema kwa ajili ya kwenda kupata matibabu Muhimbili,” anasema kijana huyo ambaye anaishi peke yake bila ndugu wa kumsaidia. Mwambungu anasema uvumilivu wake ulimsaidia kupata kiasi kidogo cha fedha. Ilipofika Februari 2014 alifanikiwa kwenda kumwona daktari mwingine huko Muhimbili.
“Nilimwelezea pia chimbuko la tatizo hili…Moja kwa moja akasema watanifanyia uchunguzi wa kina lakini akanishauri niendelee na zile dawa za maumivi na sindano kwa sababu nilimwambia bado ninapata maumivu makali sana,” anasema Mwambungu.
Uchunguzi huo ulifanywa kwa kukatwa nyama kidogo kutoka kwenye sehemu ya mguu yenye kidonga hicho.
“Siku ya kurejeshewa majibu ilipowadia daktari aliniita akaniambia kuwa kwa mujibu wa uchunguzi waliofanya kutokana na ile nyama waliokata wamebaini kuwa nina saratani ya ngozi ambayo ipo kwenye hatua za awali,” anasema na kuongeza,
“Ninahitajika kufanyiwa upasuaji ili waweze kuondoa hiyo sehemu ambayo imeanza kuharibika.”
Mwambungu anasema daktari alimwambia kuwa upasuaji utagharimu Sh700,000 fedha ambayo kwa hali aliyonayo hajaweza kuipata hivyo anaomba Watanzania wamsaidie.
Mtaalamu wa Afya alonga
Mganga wa Hospitali ya Nansio, Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, Dk. Michael Kamili anafafanua kuwa kuna aina zaidi ya nne ya kansa ya ngozi. Moja ikiwa ni hiyo ambayo huanza kama kipele na hadi kufikia hatua ya kuondolewa sehemu ya ngozi au kiungo.
Dk Kamili anasema kuwa kipele hicho hukua kwa haraka sana tofauti na ilivyo kwa vipele vya kawaida, lakini kuna mara nyingi kipele hicho huwa hakina maumivu.
Anaendelea kufafanua kuwa njia pekee ya kubaini kansa ni kwamba mgonjwa anapoenda kuonana na wataalamu wa afya huwa wanafanya vipimo kwa kuchukua sehemu ndogo (sample) ya eneo lililo athirika na kulifanyia vipimo.
“Wataalamu wa afya wakibaini kuwa ni kansa baada ya kupata majibu ya vipimo hivyo huwa wanatoa matibabu kulingana na hatua ilipofikia na aina ya kansa hiyo ya ngozi,” anabainisha Kamili.
Kamili anasema kuwa ikiwa kansa imefikia hatua ya mwanzo madaktari wanaweza kushauri sehemu yenye uvimbe ilioambatana na ngozi ikatwe, kukinga athari za ugonjwa huo kuenea zaidi.
Hata hivyo ikiwa ugonjwa huo umefikia kwenye hatua za mwisho mgonjwa atalazimika kukatwa kama ni mguu au mkono, vikiwa ndiyo viungo vinavyoelezwa kushambuliwa na kansa ya ngozi mara kwa mara tofauti na viungo vingine.
Pia, matibabu mengine yanaweza kuwa dawa na kufanyiwa matibabu kwa njia ya mionzi.

Post a Comment

 
Top