0

Hamza Kalala,  

Kuna wanamuziki ambao wamejipatia umaarufu mkubwa kupitia tasnia ya muziki, kwa kuufanya uvutie ndani na nje ya nchi.
Vile vile wanamuziki hao wamedumu kwenye tasnia hiyo kwa zaidi ya miaka 40, miongoni mwa wanamuziki hao ni pamoja na Hamza Kalala, ambaye amewahi kupewa majina kadhaa kama vile mzee wa Madongo na Komandoo.
Historia ya Kalala kwa ufupi
Alizaliwa mkoani Tanga na kusoma shule za msingi na sekondari mkoani humo.
Baba yake Komando alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Reli, katika Stesheni ya Mpanda, ambaye baadaye alihamishiwa mkoani Tanga ambako alibahatika kuoa mke wa kabila la Kizigua, ambaye ndiye mama wa Komando Kalala.
Mara baada ya Komando kuzaliwa alipewa jina la ‘Kapesula,’ akiwa ni mchanganyiko ‘chotara’ wa makabila ya Kinyamwezi na Kizigua.
Komando Kalala alianza kuhamasika katika mambo ya muziki mwaka 1966 akiwa darasa la nne, wakati alipokuwa akimshuhudia baba yake akiimba na kucheza ngoma ya Kinyamwezi ya ‘Manyanga’ ambayo ilitokana na ngoma ya ‘Hiyari ya Moyo’, huko huko Tanga.
Wakati huo wakata mkonge walikuwa wakifanya mashindano ya ngoma kati ya Wanyamwezi na ngoma za makabila mengine waliokuwa katika mashamba tofauti ya mkonge ya Kibaranga, Amboni na mengine mengi.
Lakini ngoma ya ‘Manyanga’ ya Wanyamwezi na ile ya ‘Sindimba’ ya Wamakonde ndizo zilizokuwa zikitia fora katika mashindano hayo kila mara. Kalala anaeleza, hakufundishwa muziki na mtu bali ni kutokana na ngoma hizo alizokuwa akicheza na kuimba baba yake, na kumuiga kupiga gitaa mjomba wake ambaye alikuwa na gitaa nyumbani.
Anasema alipima uwezo wake wa muziki alipokuwa kwenye bendi zilizokuwapo kwenye mashamba ya Mkonge kama Kwanduru Jazz Band, na Amboni Jazz.
Hakuvutiwa na maisha ya mashambani hivyo alirudi Tanga Mjini, ambako aliendelea na mazoezi ya kupiga gitaa nyumbani kwao, siku moja alipita Mkongo mmoja aliyekuwa akijulikana kwa jina moja la Chivosha, akavutiwa kwa jinsi alivyokuwa akipiga gitaa na kumuomba ajiunge na bendi yao ya Villa Negro Successes.
Anasimulia huku kote alikuwa anatoroka na baba yake hakuwahi kufahamu kama anaimba, alichelea kumwambia kwa kuogopa kukatishwa tamaa.
Anaeleza kuwa baba yake aliposikia kuwa mwanaye ni mwanamuziki na anaimba na kupiga katika ukumbi wa Mwananchi, ulikuwa ukumbi maarufu Mkoani Tanga, akaenda kumtafuta, lakini hakumtambua licha ya yeye kumuona.
Kalala anasema, haikuwa rahisi kumfahamu kutokana na alivyojiremba, kutokana na kuwapo katika bendi ya Wakongo ambao wanapenda kujiremba.
Anasema wanawake wa viongozi wa bendi hiyo, kazi yao kubwa ilikuwa ni kumremba, ambapo siku hiyo aliyokuja baba yake alikuwa amechoma nywele, na alivaa nadhifu kama wanamuziki wa Kikongo wanavyovaa.
“Moja ya sifa za mwanamuziki kufanya kazi na wanamuziki wa Kikongo ilikuwa ni kuwa nadhifu, na wakiridhishwa na kazi yako wapo radhi kukugharamia, wanawake wao walikuwa wanachukua karibu nusu siku kunipendezesha, na kwa kweli nilikuwa nabadilika kabisa, “anasema Kalala.
Anaendelea kueleza kabla ya kukutana na baba yake ili kulitolea ufafanuzi suala hilo walipata safari ya Nairobi nchini Kenya, akatoroka na aliporudi alimletea zawadi ya fulana ya kisasa wakati huo, na kumueleza wazi kuwa alikuwa Nairobi, kimuziki na ndiyo kazi anayofanya kwa wakati huo.
“Aliipenda sana zawadi niliyomletea, na alinisifia kwa kujiheshimu kipindi chote kiasi cha yeye kushindwa kubaini kuwa mimi ni mwanamuziki, na kunitaka niendelee kuwa na heshima katika kazi yangu hiyo, “anasema Kalala.
Anasema anakumbuka fedha ya kwanza kulipwa katika muziki ni Sh saba kwa mwezi ambayo yote aliimaliza kwa kununua nguo, kama suruali pekosi, viatu raizoni na Itali vilivyokuwa vimechongoka mbele kama mkuki, na mashati ya slimu fiti ambayo yalikuwa yanashika mwili, ‘ukimkumbatia mtu limechanika’.
Anakumbuka jinsi alivyokuwa anapata taabu na kina dada ambao walikuwa wanampapatikia kutokana na kuwa nadhifu, hadi kuna kipindi alilazimika kujificha ili kuepuka usumbufu.
Anasema kifo cha bendi hiyo kilitokana na kugombania fedha, kuna baadhi walisema hawalipwi vizuri, “ siku hiyo walipigana sana, na walikuwa na miili mikubwa, sikuingilia ugomvi wao, hivyo baada ya hapo bendi ilikufa kutokana na baadhi yao kuamua kurundi kwao Kongo usiku huo huo.
Safari ya kwanza kutafuta bendi nje ya Tanga
Mwaka 1969, aliamua kumfuata mwanamuziki Abel Bartazar ambaye alikuwa anaishi na kufanya kazi za muziki katika Mji mdogo wa Kilosa Mkoani Morogoro, lakini kwa bahati mbaya hakumkuta.
Anasema aliamua kurudi Tanga kujipanga upya kabla ya kuamua kwenda Moro kwa lengo la kutafuta kazi katika bendi za Moro Jazz na Cuban Marimba.
Anasema hakuwa na ndugu wala jamaa Mkoani humo, hivyo alilazimika kuuliza zilipo kumbi za starehe ambazo zilikuwa zinapiga muziki wa dansi baada ya kushuka kituo cha mabasi.
Anaeleza kwa bahati mbaya akafahamishwa kuwa bendi maarufu za muziki wakati huo Cuban Marimba na Moro Jazz, zilikuwa ziarani mikoani ambapo Moro Jazz ilikuwa Zanzibar na Cuban Marimba ilikuwa Songea, lakini kwa bahati nzuri alibakia mwanamuziki mmoja wa Cuban Marimba, mpiga gitaa la solo anaitwa Waziri Nyange, akaelekezwa alipo.
“Nilipofika nyumbani kwake alinipokea, nikajieleza kuwa mimi ni mgeni nimetoka Tanga na nimekuja kwa ajili ya kutafuta bendi ya kupigia muziki, akanikaribisha na kuniambia nitaishi kwake, hadi bendi itakaporudi, ”anasema Kalala.
Kalala anasema, baada ya wiki moja bendi ya kwanza kurudi ilikuwa ni Moro Jazz, hivyo akaenda kujieleza kwa Mbaraka Mwishehe, ambaye alikuwa na taarifa ya uwapo wake, na kumkubali akanza kupiga katika bendi hiyo.
Anasimulia aliporudi Juma Kilaza, kiongozi wa Cuban Marimba hali ilikuwa tofauti, alimwita na kumueleza kwa nini amejiunga na bendi hiyo wakati alipokelewa na mtu wao, kulingana na ukweli alioambiwa ikabidi aondoke Moro na kujiunga na Cuban Marimba.
“Kilaza alikua mbabe kidogo, hivyo alikuja kunichukua kwa nguvu Moro Jazz na mimi sikuwa na budi kukubali, kutokana na ukweli walioniambia na hadi wakati huo nilikuwa naishi kwa Nyange, ”anasema Kalala.
Anaendelea kusimulia kuwa, licha ya kukubali kujiunga na Cuban Marimba kutokana na hisani aliyofanyiwa na Nyange, alikuwa anatamani sana kubaki Moro kutokana na ucheshi wa Mbaraka Mwishehe na unadhifu waliokuwa nao wanamuziki wa Moro Jazz ukilinganisha na Cuban Marimba.
Anasema kama kulikuwa na bendi zina upinzani wa kweli wa muziki, ilikuwa ni hizi mbili, zilikuwa zinashindana na kupiga muziki wa kweli, anazitaja nyimbo za majibizano zilizokuwa zinaonyesha upinzani wao ni ule wa Moro Jazz, uliokuwa unaitwa ‘Moto wako washa nje hapa maji yatazima’, na Cuban wakawa na mtindo kila baada ya kumaliza wimbo wanasema ‘Dawa ya moto ni moto siyo maji’, ikiwa ni kama kuwajibu Moro.
Anawataja wanamuziki aliowakuta Moro Jazz kuwa ni pamoja na Mbaraka Mwishehe , Issa Khalfani aliyekuwa anatumia shoto na alikuwa anapiga gitaa zote, Athumani Milingiti, Maneno, alikuwa anapiga drums, Kokobile alikuwa mwimbaji, ambaye ndiyo aliyeimbiwa wimbo na Baraka Mwishehe uitwao ‘kwa heri rafiki yangu mpenzi’, alipokuwa anaondoka kwenda kwao Zaire.
Anayakumbuka mashairi ya wimbo huo kuwa ni ‘Kwa heri, kwa heri rafiki yangu mpenzi, utapofika Zaire wasalimie mabingwa wote wa muziki wa huko Zaire......Wasalime Franco na Ok Jazz’.
Anawataja wanamuziki waliokuwa wanaunda Cuban Marimba wakati huo kuwa ni Juma Kilaza, mpiga solo Ufuta, Ally analikuwa anapiga Rythm, mpiga bezi gitaa Juma Sangula, na mwimbaji Maselina.

Post a Comment

 
Top