Wanaitwa Mabaga Fresh na awali walitamba na kazi zao nyingi
ambazo zilikuwa gumzo si tu kwa washabiki wa muziki wa Hip Hop, bali pia
hata kwa watu wa kawaida wasio na mapenzi na aina hiyo ya muziki.
Wimbo kama Ngangari, Tunataabika, Mtulize, Mtu
bee, Mauzauza, Fagio la chuma na zingine ambazo ziliwatambulisha vyema
katika ulimwengu wa muziki na kuwaweka kileleni katika chati mbalimbali
za Hip Hop.
Hali hiyo ilikuwa inajitokeza huku kukiwa na
ushindani mkali wa makundi ambao ulinadhifishwa na majibizano ya wasanii
kwa wasanii na kundi kwa lingine hali ambayo ilichochea utamu wa muziki
huo na kuzoa halaiki ya washabiki.
Makundi yaliyokuwa yakitamba siku hizo ikiacha
Mabaga Fresh ni pamoja na Gang Star With Matatizo G(WM), TMK Wanaume,
BDP, Gangwe Mob, Watengwa, Walume Ndago na East Coast Team.
Mengine ni Unique Sisters, Wateule na makundi
mengine ambayo yalikuwa gumzo kubwa kutokana na kazi zao achilia mbali
wasanii binafsi ‘solo artist’ ambao hata hivyo walilazimika kuibukia
katika moja ya makundi hayo ingawa hawakuwa wanachama wa kudumu.
Mmoja kati ya wasanii hao ni Zay B aliyeimba na
Mabaga Fresh wimbo ‘Nipo Gado’ ambapo alijitambulisha kama mwanadada
gaidi akiwaponda Gangwe Mob ambao walikuwa chini ya Inspekta Haroun.
Muziki wa makundi hayo ulivutia wengi na kufanya
hata wale waliokuwa wakiuchukulia kuwa ni wa kihuni kutafakari mara
mbili na kubadili mwelekeo.
Kundi hilo ambalo lilikuwa linaundwa na Christoms
Mwingira ‘Dj Snox’ na Jumanne Omary ‘Mkuu wa Majeshi’, hivi sasa
limejipanga na tayari lina nyimbo 30 na kati ya hizo ambazo zimerekodiwa
kwa ajili ya kuwepo katika albamu hiyo ni 14. “Tumejipanga na mashabiki
wa muziki wa Hip Hop wajipange” anasema Dj Snox na kuongeza kuwa albamu
moja kuwa na nyimbo 14 ni jambo geni bongo lakini la kawaida nchi za
Marekani na Ulaya” anasema Mwingira.
Anasema albamu itaitwa 770 na wataisimamia wenyewe
kimauzo ili kuona jinsi gani itawalipa tofauti na siku za nyuma ambapo
waliwatumia mawakala ambao walikuwa wanachangia kupotea kwa mapato yao.
Snox anasema ukimya wao haukuwa wa bure na
walikuwa wanafanya kazi ingawa hawakupata muda wa kurekodi au kuzifanya
ziwe hewani na baada ya kujiweka sawa sasa wanakuja.
“Tulikuwa chimbo (kambini) kiaina ingawa kila
mmoja kwa wakati wake alikuwa anapata fursa ya kushiriki na makundi
tofauti na muziki,” anasema na kuongeza kuwa madai kuwa kinachokuja sasa
ni tofauti.
Msanii huyo alikataa kuzielezea kwa undani nyimbo
zao na kudai kuwa hakuna ambayo itamlenga mtu na kama ikitokea basi
itakuwa ni mtazamo wake lakini sicho walicholenga wao.
Anasema kundi hilo ambalo lina sifa kubwa ya kuwakabili
wapinzani wao majukwaani kwa kutumia mashairi ya nyimbo zao hivi sasa
linakuja tofauti.
“Wakati wa bifu umekwisha kaka hivi sasa ni kazi
na kuiamsha jamii kwani inasongwa na mambo mengi” anasema Mwingira na
kuongeza kuwa ufadhili ma sasapoti ya wadau inahitajika kwani pamoja na
yote pekee yao hawawezi.
Post a Comment