UNAMKUMBUKA yule beki wa Prisons aliyemkaba Amissi Tambwe mwanzo mwisho hadi wakapasuka vichwa wote wawili?
Simba imefanya naye mazungumzo na inataka kumsajili awasaidie Joseph Owino na Donald Mosoti.
Huyo si mwingine bali ni beki wa kati wa Prisons,
Nurdin Chona ambaye alimkaba ipasavyo Tambwe katika mechi ya Ligi Kuu
Bara ya raundi ya pili iliyochezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya na timu hizo
kutoka suluhu.
Simba haina beki wa uhakika wa kati inayeweza
kumtumia endapo mmoja kati ya Owino au Mosoti akiumia, hivyo haraka
ikafanya mazungumzo ya siri na Chona ili iweze kumsajili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chona alisema:
“Viongozi wa Simba walinifuata na kufanya mazungumzo nami, sikutaka
kuwadanganya niliwaambia ukweli kwamba bado nina mkataba na Prisons na
kama wananihitaji wawasiliane na uongozi ili kujua tunafanyaje.”
Chona ambaye ni askari magereza, alisema anapenda
kujiunga na Simba ili apate changamoto mpya lakini hawezi kukubaliana na
njia zilizotaka kutumiwa na wana Msimbazi kwani anaheshimu mkataba
wake.
“Wasiogope wafuate taratibu kwa kuzungumza na uongozi na mambo yataenda vizuri,” alisema Chona.
Kwa sasa, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, Zacharia Hans Poppe hayupo nchini, lakini Katibu Mkuu wa timu
hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema: “Kila kitu cha usajili wa Simba kitawekwa
wazi wiki ijayo.”
Post a Comment