Kocha Hans Pluijm
SI utani, Kocha Hans Pluijm ameihakikishia kuiletea timu yake ya
zamani ya Yanga kocha mpya atakayefuata na kuiendeleza misingi
aliyoiacha ili timu hiyo iendelee kutisha ndani na nje ya nchi kwa soka
la uhakika.
Kabla hajapeana mkono wa kwaheri na Yanga, Pluijm
aliyeifundisha timu hiyo kwa siku 107, aliwaambia viongozi wa timu hiyo
kwamba atahakikisha anawaletea bonge la kocha atakayeifanya timu hiyo
iwe tishio.
Pluijm raia wa Uholanzi aliyejiunga na Al- Shoalah
ya Saudi Arabia, kabla ya kuondoka nchini juzi Alhamisi, aliliambia
Mwanaspoti kuwa: “Nimewaambia Yanga watulie, nawaletea bonge la kocha
atakayewapa mafanikio kama waliyotaka kutoka kwangu.”
“Kuna kocha naendelea kuzungumza naye na tupo
katika hatua nzuri, mambo yakikaa vizuri ndiye nitakayempeleka Yanga
akaendelee nilipoishia mimi, naipenda Yanga na sitaki kuona inaangukia
katika mikono ya kocha mwenye kiwango cha chini yangu au asiyeweza
kazi.”
Yanga imeshika nafasi ya pili katika msimu
uliopita wa Ligi Kuu Bara chini ya Pluijm hivyo mwakani itacheza Kombe
la Shirikisho Afrika, pia ligi kuu.
Pluijm anasisitiza vitu ambavyo atahakikisha kocha
mpya anakuwa navyo: “Kwanza nataka ambaye atasimamia nidhamu kwa karibu
ili timu iweze kuongozwa, si mchezaji anafanya mambo atakavyo na muda
anaotaka. Lazima wawe kitu kimoja hivyo kocha mpya lazima aendelee
kuifuatilia nidhamu maana wachezaji wa Kiafrika bila kuwa makini na
nidhamu huwezi kufanikiwa.
“Pili, ni kuifanya timu iendelee kucheza soka la
kuvutia na kufunga mabao ambayo yataonekana na kila mtu kuanzia
linavyoanza kutafutwa hadi linafungwa.
“Tatu, kocha mpya anatakiwa kuwa na hamu ya
kuhakikisha wanafikia malengo ya kufika mbali katika ligi pamoja na
michuano ya Caf (Kombe la Shirikisho), maana hiyo ni nafasi adimu kwa
kocha,” alisema Pluijm anayetarajiwa kuwasili nchini kuanzia kesho
Jumapili.
Kiboko ya Kavumbagu
Baada ya kumaliza kusaini mkataba Saudi Arabia,
Pluijm ataelekea Ghana ilipo familia yake na atafanya mazungumzo na
straika mpya aliyepanga kumleta Yanga kuchukua nafasi ya Didier
Kavumbagu aliyejiunga na Azam FC.
“Nataka kuiacha Yanga ikiwa na straika anayefunga
kwa njia yoyote akiwa katika mazingira yoyote, yupo mmoja wa Ghana
ambaye nilianza mazungumzo naye na nikifika huko namalizana naye,”
alisema.
Pluijm pia atazungumza na kiungo mshambuliaji
mmoja wa Ghana ambaye amependekeza asajiliwe Yanga ili kuimarisha kikosi
cha timu hiyo na kukifanya kitishe.
Wagana kumfukuza HamisKiiza
Kama Yanga ikifanikiwa kuwasajili wachezaji hao
wawili sambamba na Mbuyu Twite, itakuwa imetimiza idadi ya wachezaji
sita wa kigeni, wengine ni Haruna Niyonzima, Hamis Kiiza na Emmanuel
Okwi.
Kanuni za TFF zinaruhusu wachezaji watano tu wa kigeni katika timu, hivyo Yanga italazimika kupunguza mmoja.
Pluijm alimtaja Kiiza kuwa ndiye atakayepunguzwa kwani anamfanya Okwi kutowajibika uwanjani.
Uongozi wa Yanga
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah
Bin Kleb alisema: “Tusingeweza kumzuia Pluijm kuondoka, kwa sasa ni
vigumu kuzungumzia kwa undani kuhusu kocha mpya kwani tunaweza kuwanyima
fursa makocha wengine kutuma maombi ya kutaka kuifundisha timu yetu.
Lengo letu ni kuwa na mtu atakayeendelea pale alipoachia Pluijm na
tufanikiwe.
Post a Comment