Ni jambo la kawaida kabisa kwetu sisi wazazi wa sasa kufanya
kazi nyingi kwa wakati mmoja. Wala si jambo la ajabu kumkuta mwanamke
anapika huku anaosha vyombo pembeni yake kuna gazeti na upande mwingine
ana simu ya mkononi.
Katika kipindi kama hiki, mama huyu huwa hapendi kabisa usumbufu iwe ni kwa wageni au hata watu wengine katika familia.
Kwa mkubwa jambo kama hili linakuwa rahisi
kueleweka, lakini kwa mtoto mambo huwa ni tofauti kidogo. Kwani kutokana
na umri wake inakuwa ni vigumu kupambanua mambo.
Sasa unajua ni nini kinachoweza kutokea kwa mtoto huyu ikiwa atamvamia mama yake akiwa kwenye shughuli zake hizo?
Hebu ondoka bwana! Usinichanganye nitakupiga! Aaaah toka!
Pata picha unapomwambia maneno haya mtoto wa miaka
mitatu au minne. Kitakachotokea kwanza sura yake itasawajika. Atachukua
kidole chake ataweka mdomoni. Au kwa wengine walio wepesi kulia anaweza
akaangusha kilio cha nguvu. Unaweza kabisa kuyasoma mawazo yake kupitia
muonekano wa sura yake kwa wakati huo.
Tumekuwa tukiyafanya haya mara nyingi. Na kwa
kiasi kikubwa yanatajwa kuwa mambo yanayowakwaza watoto na hata
kuwasababishia kuwa na vitabia fulani fulani visivyoendana na maadili
mema.
“ Niache!”
Inawezekana kwa wakati huo ukawa huitaji
kuingiliwa kwa aina yeyote. Lakini unachopaswa kufahamu mtoto ana nafasi
yake kwako. Na huwezi kujua anapokuita anataka kukwambia nini. Pengine
ana jambo linalohitaji maelezo kwa wakati huo. Kitendo cha kumwambia
“niache” kinaweza kuwa chanzo cha kuharibika kwa maisha yake. Hata kama
una kazi nyingi kiasi gani, hakikisha unampa nafasi mwanao ya
kumsikiliza.
“Wewe ni …..”
Watoto wetu huwa wanaamini kile tunachokisema
kutoka midomoni mwetu hivyo tunatakiwa kuwa waangalifu na maneno
tunayotamka dhidi yao.
“Hivi ni kwa nini unamsikiliza Anna kwa kila kitu,
we mjinga sana” au “Hivi kwa nini unakuwa mjinga namna hiyo?” au
anakusikia unamwambia mwenzako “ Mwanangu ana aibu sana”
Kwa kuwa watoto wanaamini yale yanayosemwa na wazazi wao, kama
mzazi unatakiwa kuwa makini na kauli zako. Epuka kuwa mtabiri wa tabia
za mwanao.
Waswahili husema “maneno huumba” hivyo usipokuwa makini unaweza kuwa chanzo cha mwanao kuwa na tabia mbaya.
Unapomwambia mtoto kuwa ni mjinga, hujidharau na
mwisho hupoteza hali ya kujiamini na mwisho wa siku huangukia kwenye ule
ujinga uliokuwa ukimaanisha.
“Usilie kama …..”
“Nyamaza mwanangu usilie kama mtoto” au “Usilie kama mwanamke we mwanaume bwana!”
Mara nyingi tumekuwa tukitumia kauli hizi kuwabembeleza watoto wetu. Lakini umeshawahi kufikiria athari ya kauli kama hizi?
Kulia ni sehemu ya maisha ya mtoto. Mara nyingi
hutumika kama njia moja wapo ya kujifariji. Hivyo unapomwambia asilie
kwa sababu atakuwa kama fulani, unamtengenezea utaratibu mwingine wa
kukabiliana na hasira zake. Si hivyo tu pia unakuwa unamjengea mazingira
ya kuamini kuwa hisia zake hazina maana tena.
Kwa mantiki hiyo, mtoto atajitengenezea utaratibu
mpya, utakuta badala ya kulia anapopata hasira, anaamua kupambana kwa
kurusha mawe au wakati mwingine hata kutumia lugha za matusi.
Mtoto huyu ataogopa kulia ili asifananishwe na mwanamke au mtoto. Hii ni mbaya zaidi
“ Kwa nini huwezi kuwa kama dada yako?”
Ni jambo la kawaida kwetu sisi wazazi kulinganisha
tabia za watoto wetu na wengine hasa pale wanapokuwa wamekosea. “Kwa
nini huwi mtoto mzuri kama Anna?” au utamsikia akisema “ “Mwenzio
akirudi shule tu anaosha vyombo wewe unafikia kwenye TV”.
Tuonane wiki ijayo!
Post a Comment