Bariadi. Watu wasiojulikana mkoani Simiyu
wamemuua kwa kumkatakata mapanga mlemavu wa ngozi (albino), Mughu Lugata
(40) huku wakitoweka na baadhi ya viungo vyake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo
alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12:00 usiku nyumbani kwa Lugata
katika Kitongoji cha Chalala, Kijiji cha Gasuma, Kata ya Nkololo
wilayani Bariadi, mkoani hapa.
“Wauaji hao baada ya kumuua Lugata walimkata mguu
wa kushoto na kuchukulia sehemu ya goti, vidole viwili vya mkono wa
kushoto na kucha ya kidole gumba cha mkono wa kushoto na kuondoka
navyo,” alisema Mkumbo.
Mkumbo alisema Lugata akiwa amelala peke yake
nyumbani kwake, alivamiwa na watu wasiojulikana na kuanza kumkatakata
mapanga na kuchukua baadhi ya viungo vyake vya mwili na kutokomea navyo
kusikojulikana. Alisema tayari wanawashikilia watu wawili, mmoja
akidaiwa kuwa ni mganga wa kinyeji mkulima wa kijiji hicho.
Mkumbo alisema mtuhumiwa mwingine alikuwa kwa
mganga huyo wakiwa na vifaa vya kupigia ramli na kwamba chanzo cha tukio
hilo ni imani za ushirikina.
Aliwataka wananchi wenye taarifa ya wahusika wa
tukio hilo kuisaidia polisi ikiwamo kuacha kudanganyika kuwa utajiri
unakuja kwa imani za ushirikina bali kufanya kazi kwa bidii.
Alisema kuna baadhi ya waganga wanawadanganya
wateja wao kuwa, viungo vya walemavu wa ngozi vinaleta utajiri hali
ambayo inawasababisha kuamini na kuendeleza mauaji hayo kwa albino.
Kasi ya mauaji dhidi ya albino lilikuwa limepungua
baada ya Serikali na mashirika ya ndani na nje kupiga vita mauaji hayo,
lakini tukio hili linaanza kutonesha vidonda na kuhatarisha usalama wa
walemavu hao.
Post a Comment