>Wachezaji wa Manchester City wakishangilia ubingwa wa Ligi Kuu England jana Jumapili. PICHA NA AFP
MANCHESTER City imenyakua ubingwa wa Ligi
Kuu England katika staili ya aina yake baada ya kuichapa West Ham
United uwanjani Etihad na kuwaacha Liverpool kwenye mataa wakishangaa
licha ya ushindi wao dhidi ya Newcastle United kwenye Uwanja wa Anfield
jana Jumapili.
Mabao ya Samir Nasri na Vincent Kompany yalitosha
kuipa ushindi wa 2-0 Man City na hivyo kunyakua ubingwa huo kwa mara ya
pili katika kipindi cha miaka mitatu, huku Liverpool waliokuwa na
matumaini ya kumaliza ukame wa taji hilo msimu huu wakiishia kushika
nafasi ya pili baada ya kutokea nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Newcastle
United.
Daniel Agger na Daniel Sturridge walifunga mabao
ya haraka ndani ya dakika mbili na kuifanya Liverpool kujikomboa kwenye
bao la kujifunga Martin Skrtel ambalo ni la nne kwa msimu huu. Man City
imenyakua ubingwa baada ya kufikisha pointi 86, pointi mbili zaidi ya
Liverpool.
Chelsea imeshika nafasi ya tatu kwa kufikisha
pointi 82 baada ya kuishinda Cardiff City 2-1, wakati Arsenal
imekamilisha timu nne za juu zitakazocheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu
ujao kwa kushika nafasi ya nne baada ya kuichapa Norwich City mabao 2-0.
Tottenham Hotspur na Everton zimefanikiwa kupata nafasi ya kucheza Ligi
ya Europa msimu ujao baada ya kushinda mechi zao, wakati Spurs
waliikung’uta Aston Villa 3-0 na Everton ilishinda 2-0 ugenini kwa Hull
City.
Matokeo ya mechi nyingi za mwisho za ligi hiyo
zilizochezwa jana, Manchester United ilichomoa na kutoka sare ya 1-1 na
Southampton, Fulham wakitoka sare ya 2-2 na Crystal Palace na Stoke City
ikiishinda ugenini kwa West Bromwich Albion mabao 2-1 na Sunderland
ikichapwa nyumbani na Swansea City mabao 3 -1.
Post a Comment