Mgombea wa nafasi ya Urais,katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba,Evans
Aveva (juu ya gari) akisindikizwa na mashabiki na wanachama wa klabu
hiyo akielekea makao Makuu ya klabu hiyo,Mtaa wa Msimbazi,Kariakoo,Dar
es salaam kwenda kuchukua fomu ya kuwania nafasi iyo.Picha na Michael
Matemanga
GUMZO la Dar es Salaam jana Jumapili ilikuwa ni Evans Aveva na
Sued Nkwabi waliochukua fomu za kuwania uongozi wa Simba kwa kishindo.
Vigogo hao wenye ushawishi mkubwa ndani ya Simba walisindikizwa na kundi
kubwa la mashabiki na wanachama wa Simba na kusababisha mitaa ya
Msimbazi kufurika kwa mbwembwe za kila aina.
Aveva anagombea nafasi ya Urais wa Simba na Nkwabi
Makamu wa Rais. Hata hivyo Aveva ndiye aliyekuwa na umati mkubwa zaidi
na wengi walipania kutaka kusikia atazungumza nini huku ikielezwa kwamba
mpinzani wake wa karibu zaidi Michael Wambura atachukua fomu mchana
huu.
Wapambe hao walikuwa wakiimba wimbo; “Tumechoka
kukaa eda kwa miaka minne sasa Simba tunataka tutoke kiushindani zaidi.”
Wakimaanisha kwamba wamechoka kuteseka kuwa vibonde kwa muda huo sasa
wanataka Simba ya ushindani.
Maandamano yalianzia mtaa wa Lumumba ambapo Aveva
alifika hapo akiwa ndani ya gari aina ya Mercedes Benz yenye namba za
usajili T840 BHQ akifika kuungana na mashabiki wanaomuunga mkono kabla
ya kushuka na kupakia katika gari maalum aina ya Mitsubishi Chariot
iliyompa fursa ya kuonekana kwa juu ambako aliweza kuwapungia mkono watu
wote wakati akipita barabarani akielekea yalipo makao makuu ya Simba.
Msafara huo ulipitia barabara ya Uhuru na kukamata
ile ya Msimbazi ambako mbele kulikuwa na pikipiki zisizopungua 30
ambapo alipofika makao makuu ya Simba alikutana na mamia ya mashabiki
wa timu hiyo waliokuwa wakimsubiri ambako shangwe iliongezeka na kufanya
zoezi hilo kufana.
Akiwa katika makao makuu ya Simba, Aveva
aliongozana na wagombea wengine wa nafasi za ujumbe akiwemo Said Tully,
Idd Kajuna, Ramson Rutiginga. “Umati huu ulionisindikiza ni kiashiria
tosha kwamba nakubalika na nina deni kubwa kwa Wanasimba endapo nitapata
nafasi hii,”alisema Aveva
Kwa upande wa Nkwabi ambaye alikuwa mjumbe kwenye
kamati ya utendaji alisema; “Ninawania Umakamu wa Rais ili kuitumikia
timu kwa nguvu zaidi nikishirikiana na wanachama wengine na viongozi
watakaokuwepo. Najua wanachama na mashabiki wengi wangependa kuiona
Simba ikiwa kwenye makali yake ya awali kwa kusajili wachezaji makini na
wenye uwezo, hivyo nitahakikisha hilo linasimamiwa.”
Nkwabi amepanga kurejesha fomu hiyo kwenye ofisi
za klabu ya Simba hii leo Jumatatu na kusubiri taratibu nyingine za
uchaguzi kuendelea hadi hapo Juni 24 yatakapotolewa rasmi majina ya
wagombea watakaowania nafasi mbalimbali za klabu hiyo na kuruhusiwa
kuanza kampeni. Mwanachama mwingine aliyechukua fomu ya makamu wa rais
ni Wilbard Mayage.
Post a Comment