Katika makubaliano hayo, Kampuni ya Mantra
Tanzania itawekeza Dola za Marekani 800,000 kwa mwaka 2014 katika
kampeni dhidi ya ujangili nchini.
Makubaliano hayo yalisainiwa na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Uranium One Inc, Chris Sattler kwa niaba ya Mantra Tanzania, kampuni
dada ya Uranium One inayosimamia Mradi wa Mto Mkuju, mgodi mkubwa
duniani wa urani katika ukanda wa kusini wa nchi.
Akizungumzia hali ya ujangili nchini, ofisa
mtendaji huyo alisema, “Ujangili wa ndovu umefikia hatua mbaya katika
Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous na Kampuni ya Mantra imejipanga
kikamilifu kuchukua hatua madhubuti ili kukabiliana na tatizo hili,”
alisema Sattler na kuongeza:
“Makubaliano haya yanaturuhusu kushirikiana na
Idara ya Wanyamapori, kuandaa na kuutekeleza mpango wa kupiga vita
ujangili ili kuwaokoa ndovu waliopo katika Hifadhi ya Selous. Napenda
kumshukuru Waziri Nyalandu kwa uongozi wake katika suala hili la msingi.
Najua wote tuna matumaini kuwa mpango huu utasaidia kuonyesha njia kwa
kampuni binafsi na za umma kushirikiana katika kuhifadhi wanyamapori.”
Waziri Nyalandu alisema Serikali ya Tanzania
ambayo inaunga mkono mradi huo, itahakikisha masuala mengine yaliyosalia
yatasainiwa kabla ya Juni.
Post a Comment