“Nipo fiti kwa ajili ya kuitumikia timu yangu kipenzi, Yanga, uamuzi wa
kucheza au kutokucheza ni wa benchi la ufundi, mawazo ya nje kwa sasa
sinayo,”
Ngassa
Klabu moja ya Qatar inataka kumsajili Mrisho Ngassa kwa mkataba wa miaka miwili.
Dar es Salaam. Mabingwa wa soka
wa Tanzania Bara, Yanga wanaweza kumkosa mshambuliaji wao mahiri Mrisho
Ngassa baada ya klabu moja ya Qatar kuonyesha nia ya kumsajili huku
mchezaji huyo akikiri kwamba dau walilomuahidi linamshawishi.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi ilizipata jana
zilisema kuwa, tayari Ngassa amekwishafanya mazungumzo na klabu hiyo
ambayo ipo tayari kuilipa Simba SC milioni 45 anazodaiwa na kuifidia
Yanga kwa kumuuza mchezaji huyo.
Taarifa hizo zimesema kuwa klabu hiyo inataka
kumtumia Ngassa baada ya usajili wa dirisha dogo.Ngassa alithibitisha
hilo huku akikataa kutaja jina la timu hiyo kwa sababu za kisheria za
usajili wa wachezaji na kuogopa adhabu ya Shirikisho la Soka Kimataifa
(Fifa).
Mchezaji huyo alikiri kuwa timu hiyo ipo tayari kumpa mkataba wa miaka miwili na kuzilipa Simba SC na timu yake ya sasa, Yanga.
Alisema kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuona
suala lake la kuitumikia Yanga katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara
linashika sura mpya kutokana na mvutano wa malipo.
Alifafanua kuwa klabu hiyo imemuahidi donge nono
na kuamua kufuta msimamo wake wa zamani wa kutaka kucheza soka hapa
nchini kutokana na maslahi anayopata.
“Maslahi yao mazuri na mazingira waliyoniahidi
kimkataba, nimevutiwa nao kutokana na ukweli kuwa suala langu la
kuichezea Yanga limekumbwa na vipingamizi vingi,” alisema Ngassa.
Alisema kuwa baadhi ya wadau wa Yanga na marafiki
zake wana nia njema ya kutaka kumlipia fedha anazodaiwa na Simba, lakini
uongozi wa Yanga bado haujatoa jibu la sakata hilo.
“Nimemaliza kifungo cha mechi sita, sasa suala lililobaki ni malipo, viongozi hawajatoa jibu mpaka sasa, ” alisema Ngassa.
Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Clement Sanga
alikiri kuwa bado hawajailipa Simba fedha wanazomdai Ngassa kutokana na
majadiliano waliyokuwa nayo.
Sanga alisema kuwa wana uhakika kuwa Ngassa ambaye
anafanya mazoezi ya nguvu na Yanga, atacheza Jumamosi dhidi ya timu
ngumu ya Ruvu Shooting.
Post a Comment