Mbegu dhaifu zinahitaji uangalizi wa hali ya juu kwa sababu mkulima asipokuwa makini, zitazaa matunda yasiyo bora.
Wakulima wengi nchini wamekuwa na mazoea ya
kutayarisha mashamba yao bila kufuata msingi sahihi inayozingatia kilimo
bora na kusababisha wakulima hao kupata hasara.
Mara nyingi hali hiyo inatokana na wakulima kutokuzingatia ushauri wa kitaalamu, kwa mfano, kilimo bora chenye tija.
Mbali na hayo ili kujua changamoto zinazoikabili
sekta ya pamba kupitia kilimo cha mkataba sambamba na umuhimu wa Mfuko
wa Maendeleo ya Pamba (CDTF), Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba nchini
(TCB), Gabriel Mwallo na Meneja wa CDTF, Essau Mwalukasa, wanazungumzia
mambo mbalimbali yanayohusu kilimo hicho cha mkataba.
Mwalukasa anasema kazi ya mfuko huo unaojumuisha
wakulima, wafanyabiashara na Serikali ni kununua pembejeo za kilimo
kutoka nje kwa manufaa ya wakulima.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wakulima
kupitia kilimo cha mkataba, Mwallo anasema kilimo cha mkataba
kinawasaidia wakulima kupata dawa za mimea na mbolea, mazao bora
kutokana mbegu bora wanazopewa wakulima.
Mwallo anaeleza kwamba mbegu dhaifu inahitaji uaangalizi wa hali ya juu kwani inazaa matunda yasiyo na ubora.
“Gharama za utunzaji wa mbegu dhaifu ni kubwa kwa kuwa mkulima atalazimika kununua dawa nyingi ili kupata mbegu bora,” anasema.
Ameongeza kuwa iwapo mmea dhaifu utakosa dawa hizo
mara kwa mara pamba itakayotoka itakuwa na weupe hafifu. Anasema
kutokana na kuwapo wa dawa zenye kiwango cha chini, itamlazimu mkulima
kuingia gharama zaidi kununua dawa.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa TCB, anasema ili kupata
mmea bora wataalamu wanashauri mkulima kupanda kiasi cha mbegu takribani
22,200 kwa ekari moja. “Kwa mbegu bora mkulima anaweza kurudia mara
mbili kuweka dawa ya kuzuia wadudu, lakini kwa mbegu dhaifu itamlazimu
mkulima kurudia mara kwa mara kwa kiwango cha asilimia 85,” anasema.
Kuhusu changamoto ya uhaba wa mvua, Mwallo
anasema: “Kilimo chetu nchini Tanzania kinategemea mvua kwa asilimia
100, lakini kwa bahati nzuri zao la pamba ni kati ya mazao yanayohimili
ukame.”
Mwallo anasema CDTF imelenga kusimamia maendeleo
ya pamba sambamba na kuitangaza kwa ushirikiano na TCB na Kampuni ya
Usambazaji wa Pembejeo nchini (MUKPAR).
Post a Comment