0


 Wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza vyombo vya nyumbani wakiwa kazini wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro. Picha na Zacharia Osanga. 
Kutokana na juhudi za kiwanda hicho, Serikali inapaswa kukipatia ruzuku. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha vikombe kati ya 1,500 mpaka  2,000 kwa siku.
Kama unatabia ya kupenda kukagua bidhaa kwa lengo la kujua zinatengenezwa wapi, basi ni rahisi kwa kuwa vikombe vingi vinavyotumika kunywea chai, vimetengenezwa China.
Ukifika wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro utakuta kiwanda cha kutengenezea bidhaa hizo zinazotumika kunywea chai pamoja na matumizi mengine.
Tununue bidhaa zetu
Kiwanda cha Kilimanjaro Industries Development Trust (KIDT) ambacho ni tawi la Kiwanda kikuu kilichopo Moshi kimekuwapo wilayani hapo kwa takribani miaka 30, kikizalisha vikombe, sahani, bakuli, birika, majagi na vifaa vya kuwekea maua.
Bidhaa hizo zinazozalishwa kutokana na malighafi zinazopatikana wilayani humo, wilaya jirani ya Mwanga na malighafi nyingine kutoka Pugu Dar es Salaam.
Msimamizi wa Kiwanda hicho, Loveness Mhina anasema vikombe hivyo vya udongo na bidhaa nyingine wanazotengeneza wanatumia mawe wanayoyatoa eneo la Kavambughu,  nje kidogo ya wilaya hiyo, udongo maalum wanaochimba eneo la Kifula wilayani Mwanga na Kaolini inayopatikana Pugu Dar es Salaam. Mhina anasema kiwanda hicho kwa siku kina uwezo wa kuzalisha vikombe kati ya 1,500 hadi 2,000 kwa siku.
Mbali na kutengeneza vyombo hivyo vya mezani pia kiwanda hicho kinatengeneza vifaa visivyopitisha umeme (insulators), vinavyotumiwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambavyo navyo hutengenezwa kwa malighafi hizo.
Miaka 30 kiwanda kimefanya nini?
Meneja Mkuu wa KIDT, Mhandisi Frank Elisa, anasema kiwanda hicho kilipaoanzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1980, hakikuanzishwa kwa lengo la biashara.
“Wajapan ndiyo walioanzisha viwanda hivi na lengo lao lilikuwa kuanzisha viwanda vidovidogo kwa kutumia raslimali zinazopatikana maeneo husika.Kwa mfano,  malighafi za kiwanda hiki, nyingi zinatoka Same,” anasema.
Anasema fursa za biashara zipo nyingi, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni mtaji wa kukipanua kiwanda hicho.
“Mtaji ni changamoto kubwa kwa sasa tunafanya kazi kwa kutegemea  fedha za wateja, lakini tunachukua jitihada za kuwa na uhusiano mzuri na benki ili tupate mkopo,” anasema.
Elisa anasema mbali na uzalishaji unaoendela pia wanafanya tafiti za bidhaa na masoko jambo ambalo wakati mwingine linawagharimu kwani inakuwa vigumu kufanya uzalishaji na utafiti kwa wakati mmoja.
Pamoja na hayo Mhandisi wa Kiwanda hicho Abtwalibe Maghembe anasema mashine wanazotumia ni za zamani na kusababisha kuzalisha bidhaa chache ambazo hazikidhi mahitaji ya wateja.
 “Mashine zetu zinategemea zaidi usimamizi wa mtu (manually) tofauti na wenzetu ambao wanatumia ‘Automatic Machine’ ambazo zinafanya kazi kubwa na kwa kasi,”anaeleza.
Anaongeza kuwa kwa sasa zipo mashine za kisasa zinazoendeshwa kwa mfumo wa Kompyuta (Computer Numerical Control-CNC) ambazo utendaji wake uko juu kuliko mashine wanazotumia wao.
Maghembe anasema ili uzalishaji uwe mkubwa wanahitaji kuzalisha bidhaa bora zaidi na nyingi ambazo zitapunguza gharama za mauzo.
Mhina anabainisha changamoto zinazokabili kiwanda hicho ni tatizo la maji ambalo ni la muda mrefu wilayani Same.
Changamoto hiyo inazorotesha kwa kiasi fulani uzalishaji mali kiwandani hapo.
“Kazi      zetu zote zinahitaji maji, kwa kawaida tunatumia lita 8,000 kila baada ya siku mbili, yanapokosekana uzalishaji unarudi nyuma, lakini pia umeme unapokatika ni tatizo lingine, lakini tupo kwenye mpango wa kununua jenereta,” anasema.
Naye Mhandisi wa  KIDT, Maghembe anasema kuna wakati wanaenda maeneo ya mbali kama Kirinjiko kwa ajili ya kutafuta maji na hivyo kupoteza muda mrefu badala ya kutumia muda huo kuzalisha.
Anasema wanatengeneza mfumo wa kutumia maji yaliyokwisha tumika ili yatumike tena kwa lengo la kukabiliana na tatizo la maji.
Maghembe anasema mpango mwingine wa kutatua changamoto ya umeme,  kuanza kutumia gesi.
Utengenezaji wa vikombe
Kwanza, mtengenezaji anapaswa kuchanganya udongo na baada ya kufanya hivyo hatua ya pili anatengeneza umbo la kikombe,  hatua ya tatu,  ni kuvichoma kwenye matanuru, hatua ambayo inahitaji umeme mkubwa na baada ya kukaushwa kinafaa kwa matumizi.
Kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 20 na 13 kati yao wameajiriwa. Wafanyakazi katika kiwanda hicho ni wanawake kwa kuwa kiwanda kimetoa kipaumbele kwa kinamama na wengine waliobaki ni wanaume watatu.
Waajiriwa wengine ni wa muda na huajiriwa kutokana na mahitaji ya kiwanda.
Kutoka na uchache wa viwanda nchini, serikali inapaswa kutazama kwa jicho la tatu viwanda kama hivi ambavyo vinaweza kupunguza tatizo la ajira kwa vijana, lakini changamoto ya mitambo ya kisasa haina budi kutatuliwa.

Post a Comment

 
Top