0
Kaze na Tambwe waliumia Jumamosi iliyopita wakati Simba ilipoikabiri Mbeya City na kutoka sare ya 2-2.
Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Simba limeshusha pumzi kufuatia wachezaji wake wawili wa kimataifa raia wa Burundi, Gilbert Kaze na Hamis Tambwe kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha waliyopata Jumamosi iliyopita wakati wakiitumikia timu hiyo ilipokuwa ikipambana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika michezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, timu hizo zilitoka sare ya 2-2, mabao yote ya Simba yalipachikwa wavuni na Hamis Tambwe ambaye hadi sasa ameshazifumania nyavu mara sita katika  mechi tatu za Ligi Kuu alizoitumikia klabu hiyo.
Kwa mujibu wa Daktari wa Simba, Yassin Gembe alisema kuwa wachezaji hao walipatwa na matatizo hayo katika mechi hiyo ambapo Kaze alishtuka Nyonga na Tambwe aliumia nyama za paja.
Alisema hivi sasa wanendelea vizuri na jana wameanza mazoezi mepesi hivyo ana imani kuwa hadi kufikia Jumamosi watakuwa wapo fiti tayari kwa kukalinana na vijana wa JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Hata hivyo mbali na wachezaji hao kurejea uwanjani, Gembe alisema kuwa kuna uwezekano mkubwa kwa timu hiyo kumkosa kiungo Henry Joseph ambaye anasumbuliwa na maumivu ya goti.
“Hali ya Henry bado kidogo hajakaa sawa, lakini kuanzia kesho (leo) tunaweza kujua anaweza kuanza lini mazoezi ila Tambe na Kaze wao wapo vizuri na leo jioni (jana) watanza mazoezi,”alisema Gembe.
Timu ya Simba imepiga kambi yake katika hoteli ya Bamba Beach  iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam ikijifua kwa ajili ya mchezo wake wa Jumamosi wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Ruvu, ambapo inahitaji ushindi ili izidi kujikita juu kabisa ya msimamo wa ligi hiyo.

Post a Comment

 
Top