Wananchi hao kutoka Tanzania Bara na Zanzibar walisema kwa nyakati
tofauti kuwa, Rais Kikwete anatakiwa kutumia busara ya kushauriana na
kupata maoni ya watu wa kada mbalimbali ili kujua nini kifanyike, kabla
ya kuamua kusaini muswada huo.
Mjadala wa muswada huo uliopitishwa Ijumaa iliyopita na wabunge wengi
wakiwa wa CCM, ulizua tafrani bungeni iliyosababisha Kiongozi wa
Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi (Chadema) kutolewa nje na askari. Katika tafrani hiyo, baadhi
ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku
wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine
Mrema, wakiususia.
Wapinzani walisema Serikali iliubadili kwa nguvu muswada huo kwa kuondoa
maoni muhimu ya wadau, pia walilalamikia kitendo cha wajumbe wa Kamati
ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kutokwenda Zanzibar kuchukua maoni
ya upande huo wa muungano.
Wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gaudence Mpangala
alisema mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya ulikuwa ukienda vizuri...
“Lakini umebadilika vibaya, tena katika kipindi muhimu. Kupitishwa kwa
muswada na kusubiri saini ya Rais kunaweza kuleta Katiba Mpya, ikawa
siyo ile ambayo Watanzania wanaitarajia.” Alishauri busara itumike kabla
ya kusainiwa kuwa sheria kamili.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tunguu Zanzibar, Ali Uki alisema hakuna haja
ya muswada kukimbiliwa kusainiwa kwani katiba ni mali ya wananchi na
kuupitisha ili uwe sheria bila kuyashirikisha makundi mengine,
kutaendeleza malalamiko na kurudisha nyuma malengo ya kupatikana kwake.
Uki alisema upo wasiwasi kwamba Katiba Mpya itatokana na utashi wa
kisiasa badala ya matakwa ya wananchi, jambo ambalo alisema linaweza
kuathiri malengo ya kuandikwa kwake.
“Utashi wa vyama umeanza kujitokeza, huku chama kimoja kikiwa na
uwakilishi mkubwa kwenye Bunge hilo, chama kimoja kina uwakilishi wa
asilimia 72 katika Bunge la Katiba,” alisema Uki.
Alikosoa Kifungu cha 8 na Kifungu kidogo cha 4 na 5 cha muswada huo
kwamba vina kasoro kwa kuruhusu wabunge wa Bunge la Katiba kufanya
uamuzi kwa wingi wa kura badala ya kutumika utaratibu wa theluthi mbili
kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.
Profesa mwingine wa UDSM, Chris Peter Maina alisema ikiwa kuna nia njema
ya kupata Katiba bora, lazima suala la uwiano wa idadi ya wabunge
katika Bunge la Katiba litazamwe upya.
“Rasimu ya pili ikishatolewa na kukabidhiwa kwa Bunge la Katiba, kazi ya
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndiyo itakuwa imekwisha. Sasa inakuwaje
Bunge linajadili Rasimu ya Katiba huku waliyoiandaa hawapo, hiki kitu
kinashangaza,” alisema Profesa Maina.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Dk Frank Tilly alisema hakuna umuhimu
wa kukimbiza muswada kutiwa saini wakati kuna mambo mengi ya msingi
ambayo hayajapatiwa ufumbuzi... “Watanzania hawajakubaliana kwa pamoja,
ili jambo liwe zuri ni lazima pande mbili au zaidi zenye masilahi na
kitu husika zikubaliane, sasa hilo halijafanyika tunakimbilia wapi?”
alihoji
Post a Comment