0

Baadhi ya wachezaji wa kikosi kipya cha klabu ya Simba.  

WACHEZAJI wa Simba raia wa Burundi, beki Gilbert Kaze na straika Tambwe Amis walitua Dar es Salaam jana Jumatatu saa sita usiku, lakini Tambwe amerusha kombora na amewatamkia mashabiki wa Simba kwamba atafanya zaidi ya straika.
Tambwe anaongoza kwenye chati ya ufungaji bora katika ligi ya Burundi akiwa na mabao 22 huku anayemfuata akiwa na mabao 13 na kila timu imebakiza mechi mbili kumaliza msimu.
Mchezaji huyo alizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu jioni kwa simu akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Bujumbura na kusema; “Nimefanya mazoezi ya kutosha na Vital’O kwenye siku ambazo nilikuwa Burundi, ndio maana nakwambia kwamba niko fiti kimazoezi.
“Tulikuwa na mechi ya ligi Jumapili dhidi ya Academie Tchite tukashinda mabao 3-0, lakini mimi sikucheza kwa vile nilitaka mwili upumzike kwa kuwa nina kazi nzito sana naianza na Simba wiki hii, natakiwa mwili upumzike kidogo.
“Ila Kaze yeye alicheza hiyo mechi na yuko vizuri vilevile. Najua Simba wamenigharimia ndio maana nataka nije nitulie nifanye kazi zaidi ya hii niliyokuwa nafanya hapa Vital’O. Nazijua timu za Tanzania kama Azam, Yanga, Kagera, Mtibwa na Coastal Union ndio maana sina wasiwasi sana na ligi ya Tanzania.
“Nakuja kucheza kama straika namba 9 kazi yangu ni kufunga mabao tu, naomba Mungu anisaidie tu nisiumie. Ila nitakuja kuonyesha utofauti kwa vile najua Simba wameninunua wakanitoa Burundi kuja kufanya kazi, nahitaji kuonyesha utofauti. Naomba tu Mungu aisimamie miguu yangu na akili yangu,”alisema straika huyo.
Akizungumzia utata wa uhamisho wao alisema: “Kuna malipo kidogo ya kumalizia mkataba ambayo Simba wanatakiwa kuwalipa viongozi wa Vital’O lakini si kiasi kikubwa. Viongozi wametwambia kwamba tusiwe na wasiwasi tuje Dar es Salaam ndani ya kipindi kifupi watamalizana na tutacheza.
“Tukishafika tutakwenda moja kwa moja Tabora kuanza mazoezi na timu kujiandaa na mechi ya Jumamosi (dhidi ya Rhino Rangers) najua mambo yatakwenda sawa na tutajitahidi kufanya kwa nguvu ili kutafuta namba na kuhakikisha Simba itafanya vizuri, huo ndio mkakati,”alisisitiza kwa kujiamini huku akilalamikia hali ya hewa ya sasa ya mvua mjini Bujumbura, Burundi.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala aliliambia Mwanaspoti jana Jumatatu kwamba; “Wakiamka tu leo Jumanne watasafiri kwenda Tabora kujiunga na timu tayari kwa maandalizi ya msimu. Ni wachezaji wazoefu ambao haitawachukua muda mrefu sana kuelewana na wenzao.”
Ujio wa wachezaji hao unafanya Simba iwe na wachezaji wanne wa kigeni huku ikiacha nafasi moja ya straika wa Uganda, Moses Oloya ambaye wamepanga kumsajili kwenye dirisha dogo. Wachezaji wengine wa kigeni walioko Simba ni raia wawili wa Uganda, Abel Dhaira na Joseph Owino.
Kama hesabu za benchi la ufundi zikienda sawa kikosi cha kwanza cha Simba msimu ujao kitakuwa hivi; Dhaira, Nassor Chollo, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Abdulhalim Humoud, Betram Mwombeki, Tambwe Amis na Ramadhani Chombo ‘Redondo’.

Post a Comment

 
Top