Choo maalumu cha kuhamishwa
Uchafu wa hali ya juu…usiofaa kwa kutazama, wala kuutumia
kufanya kazi fulani, umegundulika kuwa na manufaa lukuki kwa matumizi ya
binadamu. Uchafu huo si mwingine bali ni kinyesi cha binadamu pamoja na
mkojo.
Mfumo wa usafi wa mazingira ya kiikolojia
hautiliwi maanani hapa nchini, pamoja na kufafanuliwa kwa kina na
wataalamu mbalimbali, lakini bado imekuwa ni vigumu kwa Watanzania
kuitilia maanani na kuitumia kwa tija.
Barani Asia, taka mwili zimekuwa zikihifadhiwa na
kufanyiwa utafiti kwa miaka zaidi ya 1,000, huku mfumo huo ukilindwa
katika vifungu vya sheria ya kutunza taka ya mwaka 1988, Korea ya
Kusini.
Kitaalamu mfumo huo unajulikana kama Ecological
Sanitation System, ambao unatumia taka mwili za binadamu na kuzirejesha
katika matumizi yenye thamani huku ukitunza mazingira.
‘Taka mwili’ zinafaa kwa nishati
Mtaalamu wa Mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Fredrick Mwanuzi anasema kama usimamizi wa mazingira
utazingatiwa basi ipo haja ya kufanyia utafiti taka mwili kwa ajili ya
matumizi mbalimbali kwa sababu zina manufaa makubwa katika nyanja
mbalimbali.
Mwanuzi anasema wakati umefika sasa kinyesi cha
binadamu kichukuliwe kama malighafi badala ya uchafu na kutumia mbolea
hiyo kwa ajili virutubisho vya kilimo, nishati, pamoja na dawa za
binadamu.
“Kilo 25 hadi 50 za kinyesi huzalishwa na mtu
mmoja kwa mwaka, hii ni sawa na kilo 0.55 nitrogen, 0.18 phosphorus na
0.37 potassium, vilevile binadamu huzalisha kiasi cha lita 400 za mkojo
kwa mwaka ambazo huwa na kg 4.0 nitrogen, 0.4 phosphorus na 0.9 za
potassium,” anasema.
Wataalamu wa mazingira nchini Tanzania walijaribu
‘taka mwili’ kuzifantia mchakato wa kitaalamu ili kuwa malighafi,
walichagua eneo la Majumba Sita jijini Dar es Salaam lengo kubwa likiwa
ni kuzuia kinyesi kinachotoka chooni kuchafua maji ambayo yapo ardhini.
Mtaalamu wa mazingira Esnati Chaggu alifanya
utafiti na kugundua kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Jiji la Dar
es Salaam wanatumia vyoo vya shimo ambavyo vinachafua maji yaliyomo
ardhini huku watu wengi wanategemea maji ya visima vyenye urefu zaidi ya
meta 6.75 pamoja na mabomba ambayo huathiriwa na kinyesi kinachofukiwa
ardhini. “Maji yaliyoko ardhini yanaathiriwa na aina ya vyoo ambavyo
Watanzania wanavitumia, asilimia 90 hutumia vyoo vya shimo.
“Tulichagua eneo la Majumba Sita ambalo lina
asilimia kubwa ya visima vyenye kina kifupi na wakazi wengi wanatumia
vyoo vya shimo na wengine hawana kabisa na wanajisaidia vichakani,”
anasema.
Kutokana na mazingira hayo walibuni namna ya
kuhifadhi kinyesi cha binadamu kwa manufaa na pia kutunza mazingira hasa
maji ambayo yalisababisha mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kama
kipindupindu na kuharisha.
Post a Comment