Wafanyakazi wa kiwanda cha maziwa wakiwajibika kazini
Kwa muda mrefu sasa, wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa
wakilalamika kwamba kanuni lukuki na kodi kubwa zimekuwa zikichangia
kudumaa kwa biashara na kuwavunja moyo wajasirimali.
Malalamiko yao yanatokana na ukweli kuwa ili mtu
asajili biashara yake anatakiwa kupitia kwa mamlaka zaidi ya 11 ambazo
zinatoa vibali na leseni za biashara na mchakato huo unaweza kuchukua
mwezi mzima bila usajili kukamilika.
Kutokana na mlolongo huo mrefu, wadau
wanapendekeza kwamba iwepo mamlaka moja ambayo itashughulikia utoaji wa
vibali ili kuokoa muda na kupunguza au kuondoa usumbufu usiokuwa wa
lazima.
Hivi karibuni malalamiko mengine yalitolewa na
wasindikaji wa maziwa ambao nao wanaamini mamlaka zaidi ya 11 kwa mfano,
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS)
katika sekta ya maziwa zinasababisha gharama za biashara kuwa kubwa.
“Hatusemi kwamba kusiwapo na wadhibiti la,
tunachohitaji ni wadhibiti wachache ambao watawasaidia wafanyabiashara
wadogo kujiimarisha pia kusajili biashara zao,” anasema Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha Wasindika Maziwa nchini (TAMPA), Edmund Malick.
Kanuni zinatubana
Malick anasema kuwapo kwa kanuni nyingi zinazuia wajasiriamali wapya na kukwamisha juhudi za kuimarisha sekta ya maziwa nchini.
Endapo mjasiriamali anapenda kuwekeza au kuanzisha
kiwanda cha kusindika maziwa cha lita 6,000, anapaswa kuwa na mtaji wa
wa Sh45 milioni kabla hakijaanza kufanya kazi.
Kwa mujibu wa Malick, fedha hizo ni nyingi na wengi wa wafanyabiashara hawajui namna ya kupata fedha hizo.
Malick anasema zaidi ya lita milioni 6 za maziwa
zinazalishwa nchini na wafugaji kila siku, lakini kwa sasa wasindikaji
wana uwezo kutengeneza lita 300,000 kwa siku sawa na asilimia tatu ya
maziwa yote yanayozaslishwa nchini.
“Badala ya kuondokana na kanuni zisizokuwa na
maana ili kuwavutia wajasiriamali zaidi wenye mitaji midogo katika sekta
ya maziwa, Serikali imekuwa ikiweka vikwazo vingi zaidi vya udhibiti
wajasiriamali kuingia katika sekta hiyo,” anasema Malick.
Taarifa ya hivi karibuni ya Shirikisho la Wenye
Viwanda nchini (CTI), inaonyesha kwamba wasindika maziwa wana mzigo
mkubwa wa kulipa tozo mbalimbali za kupata ruksa ya kufanya kazi hiyo
kutoka kwa wadhibiti mbalimbali wa kisekta.
Post a Comment