Wanafunzi wa moja ya shule zilizopo katika Wilayani Bukombe, kama walivyokutwa na mpigapicha wetu
Bukombe: Wakati Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ikizindua Mpango wa Kuleta Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) katika Sekta ya Elimu Tanzania leo, maelfu ya watoto wenye umri wa kwenda shule katika vitongoji kadhaa vya Kijiji cha Namalandula, mkoani Geita wanasoma katika mazingira duni kutokana na shule walizozianzisha kutosajiliwa hadi sasa.
Waziri wa Elimu, Dk Shukuru Kawambwa ndiye
atakayezindua mpango huo leo sambamba na maonyesho yenye lengo la
kuelimisha na kupata maoni ya wadau katika utekelezaji wa vipaumbele vya
sekta ya elimu.
Wakati hayo yakiedelea, katika vitongoji vya
Ilyamchele na Mutukula vilivyopo Wilaya ya Bukombe zimejengwa shule za
msingi ambazo kwa muda wote wa uhai wake unaokaribia miaka 10, zimekuwa
zikitoa ‘elimu ya awali’ tu, licha ya kwamba zina madarasa kadhaa.
Maisha ya kielimu katika shule hizi ni ya
kuhuzunisha kutokana na kwamba hazijasajiliwa hali ambayo ina athari
kubwa kwa maelfu ya watoto wanaosoma hapo sasa na wale ambao wamewahi
kusoma hapo.
Mazingira ya shule zote mbili ni duni na hazina
miundombinu kwani madarasa yamejengwa kwa miti na baadhi yake yameezekwa
kwa nyasi. Idadi kubwa ya watoto inawafanya walimu wa kujitolea katika
shule hizi kuchanganya madarasa.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Namalandula,
Jackson Bwire anasema shule hizo zilianzishwa na wananchi kutokana na
kutokuwapo kwa huduma za elimu katika maeneo yao ambayo yana kaya zaidi
ya 3,500 hivi sasa, zenye watoto wapatao 7,000 na kwamba nusu yao
wanapaswa kuwapo shuleni wakisoma.
Mwananchi lilishuhudia katika Shule ya Ilyamchele
wanafunzi wakisoma kwa zamu (wengine asubuhi na wengine mchana) wakati
katika Shule ya Mutukula, darasa la kwanza wanasoma peke yao kutokana na
wingi wao wakati darasa la pili wanachangamana na la tatu na darasa la
nne wanachanganyika na darasa la tano.
Awali wanafunzi katika shule hizo walikuwa
wakisoma mpaka ‘darasa la sita’ lakini sasa wengi wanaishia darasa la
nne, kisha kupelekwa katika Shule ya Msingi ya Namalandula ambako
hufanya mtihani wa darasa la nne na wenzao kwa lengo la kuendelea na
darasa la tano baadaye.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji (VEO) cha Namalandula,
Jackson Bwire aliliambia gazeti kuwa baadhi ya watoto ambao walifaulu
darasa nne wameshindwa kuendelea darasa la tano kutokana na umbali
uliopo kutoka katika vitongoji wanakotoka na ilipo shule iliyosajiliwa.
Wingi wa wanafunzi
Hivi sasa shule hizi kwa pamoja zina wanafunzi
954; Ilyamchele ambayo pia inajulikana kama Kashishi ikiwa na wanafunzi
600 na walimu watatu wakati shule ya Mutukula ina wanafunzi 354 na
walimu watano.
Mwezi Mei mwaka huu Shule ya Ilyamchele ambayo
ilianzishwa mwaka 2004 ilikuwa na na wanafunzi 783; wavulana 402 na
wasichana 381 wakati Shule ya Mutukula ambayo ilianzishwa 2008, ilikuwa
na wanafunzi 410; wavulana 183 na wasichana 327.
Post a Comment