Uingereza, London
Gazeti la Uingereza la Daily Mail toleo la jana, liliripoti kuwa watu walioonekana kukata tamaa wakati wa kutoa msaada kwa wasichana hao, kwa nia njema walitumia maji machafu kumsafisha mmoja wa majeruhi.
Taarifa zaidi kuhusiana na tukio la kihalifu pia
zilieleza kuwa wasichana, Katie Gee na Kirstie Trup, wote wakiwa na umri
wa miaka 18, waliwaona waliowamwagia tindikali ambapo kabla ya kutenda
uhalifu huo, walitazamana, wakatabasamu na kupeana ishara kwa kichwa.
Wasichana hao waliokuwa wakifanya kazi ya
kujitolea katika Shule ya St Monica mjini Unguja, Zanzibar,
wamehamishiwa kwenye Hospitali ya Chelsea and Westminster, London
wanakotibiwa majeraha ya tindikali.
Mtalii aliyeshuhudia
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Sam Jones,
ambaye ni mtalii kutoka Uingereza aliyekuwa Zanzibar kwa mapumziko akiwa
na mpenzi wake Nadine, aliliambia gazeti la The Sun la Uingereza namna
alivyomsaidia Katie Gee baada ya kumwagiwa tindikali.
Jones alisema akiwa na mpenzi wake kwenye mitaa ya
Mji Mkongwe, Unguja, walisikia sauti ya msichana anayeugulia maumivu
makali, ikitoka katika choo cha mkahawa uliokuwa jirani.
Alisema walipoingia ndani ya choo walimkuta
msichana raia wa Uingereza akiwa ameungua vibaya mwilini, huku wasamalia
wema wakijitahidi kumfuta kwa maji yaliyokuwemo ndani ya choo hicho.
Jones alisema dakika mbili baadaye aliingia
msichana mwingine ambaye naye alikuwa ameungua, ambapo waliwapa msaada
wa kuwasaifisha kwa maji.
“Tulihisi kuna kitu kinawasumbua na kinahitaji
kutolewa,” alisema Jones na kuongeza kuwa waliwapeleka wasichana hao
kwenye zahanati ya jirani, ambapo Nadine na wanafunzi wa uuguzi walianza
kuwamwagia maji yaliyowekwa chumvi.
Alisema kutokana na kuwepo daktari mmoja tu,
waliamua kuwapeleka hotelini wasichana hao na kuwatumbukiza ndani ya
bwawa la kuogolea, katika jitihada za kuwasaidia kuondokana na maumivu
waliyokuwa nayo.
“Maji ya bahari yalionekana kusaidia kwa sababu
msichana mmoja aliungua vibaya kwa sababu mwanzo tulitumia maji ya bomba
na mengine yalichukuliwa kutoka kwenye ndoo,” alisema.
Post a Comment