Morogoro. Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Datomax Selanyika amesema wameanza ujenzi wa barabara itakayounganisha Pori la Akiba la Selous na hifadhi hiyo lengo likiwa ni kuwarahisishia watalii wanaotaka kufika katika hifadhi hizo kutumia muda mfupi zaidi.
Alisema barabara hiyo itakuwa na umbali wa
kilomita 143 ukilinganisha na mzunguko uliopo sasa wa kutoka Selous
kupitia Kisaki, Mvuha, Matombo hadi Morogoro mjini ndipo ufike Mikumi
umbali wa kilomita zisizopungua 248.
Selanyika alisema hayo jana wakati akizungumza
mjini Morogoro ambapo alisema kuwa ujenzi huo unatarajiwa kukamilika
Oktoba mwaka huu.
Alisema kuwa lengo la kufungua barabara hiyo ni
kuwaunganisha watalii waweze kufika katika Hifadhi ya Mikumi kupitia
upande wa Kusini mwa hifadhi hiyo maeneo ambayo hayajawahi kutumika kwa
utalii pamoja na kuwa na vivutio vingi adimu.
“Asilimia 30 ya Hifadhi ya Mikumi ndiyo inatumika
kwa utalii kwa sasa, asilimia 70 ilikuwa bado haijafunguka bado ni
mapori mazito, kufunguliwa kwa barabara hiyo kutasaidia watalii kuona
vivutio vingi,” alisema.
Mhifadhi huyo alisema kujengwa kwa barabara hiyo
kutahamasisha watalii wengi wa ndani na nje ya nchi kufurahia kutembelea
maeneo hayo na kwamba wamejipanga kutoa huduma zitakazohitajika wakati
wote.
Post a Comment