Stephen Wassira. PICHA|MAKTABA
Moshi/Dar. Mawaziri Stephen Wassira na Mwigulu
Nchemba wamesema kuwa japo Bunge Maalumu la Katiba litaendelea na vikao
vyake kuanzia kesho mjini Dodoma, halitakuwa na uhalali wa kisiasa.
“Tunakwenda bungeni kuendelea na vikao kwa sababu
hatuvunji sheria. Kumbukeni hata walipotoka (Ukawa) wakati ule
tuliendelea na vikao kwa sababu akidi inaruhusu, japo hatutakuwa na
uhalali wa kisiasa lakini kisheria tuna uhalali,” alisema Wasira ambaye
ni Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais, Uratibu na Uhusiano).
Hoja hiyo ilisisitizwa na Nchemba ambaye ni Naibu
Waziri wa Fedha kuwa vikao hivyo havitakuwa na uhalali wa kisiasa japo
kisheria vina uhalali.
“Unajua kilichosababisha mkwamo huu ni kila kundi
kushikilia upande wake, kama kila kundi lingeweka masilahi ya Taifa
tusingefika huko. Tunakwenda bungeni, ingawa hakutakuwa na uhalali wa
kisiasa lakini tutaendelea kujadili mambo ya kitaifa,” alisema Mwigulu.
Viongozi hao walisema hayo baada ya mdahalo wa
Katiba uliofanyika Dar es Salam jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akisema wanakwenda bungeni
kuendelea na mijadala japo katiba haitakuwa na afya... “Nawaomba Ukawa
warejee bungeni, ikishindikana sisi tutakwenda, tutajadiliana,
tutawaletea Katiba bora ila haitakuwa na afya bila Ukawa.”
Wengi waendelea kupinga Bunge
Mbali na mawaziri hao, idadi ya wajumbe wa Bunge
hilo wanaopinga vikao hivyo kuendelea bila kushirikisha wenzao wa Umoja
wa Bunge la Wananchi (Ukawa) inazidi kuongezeka.
Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba
kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki
vikao hivyo.
Maoni ya wajumbe hao, baadhi yao wakiwa wabunge wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano kutoka CCM, yanatokana na Bunge la Katiba
kugubikwa na giza nene baada ya Ukawa, kusisitiza kuwa hawatashiriki
vikao hivyo.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema
jana kuwa haungi mkono mpango wa wabunge wenzake wa CCM kuendelea na
Bunge la Katiba bila maridhiano.
“Pengine niwakumbushe wabunge wenzangu wa CCM kuwa
kinachoandaliwa kwenye Bunge la Katiba ni Katiba ya Watanzania wote na
si Katiba ya CCM. Hatua tuliyofikia siiungi mkono, kitendo cha wabunge
wenzangu wa CCM kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu suala la
Katiba halina mshindi ni jambo la maridhiano.
“Kitendo cha sisi wabunge wa CCM kuendelea na
mchakato wa Katiba Mpya ni matumizi mabaya ya wingi wetu mle bungeni. Ni
kweli CCM ina wabunge wengi na ni kweli kwenye demokrasia wengi wape,
lakini pia demokrasia pevu na yenye tija ni ile inayoheshimu na
kuyafanyia kazi maoni ya wachache.”
Hata hivyo, mbunge huyo alisema wajumbe wa Ukawa walipaswa kubaki ndani ya chombo hicho na kujenga hoja zao.
“Ni lazima (Ukawa) watambue sisi wajumbe siyo
waamuzi wa mwisho. Tutafanya yote lakini waamuzi wa mwisho ni wananchi
kwani ndiyo wanaoweza kupiga kura ya kuikataa au kuikubali,” alisema.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, Maria Sarungi
alisema Katiba inapaswa kuwa mkataba wa pamoja lakini bila maridhiano
inakuwa ni waraka unayokosa uhalali wa kukubalika kwa jamii.
Mbunge wa Kahama (CCM), James Lembeli alimsihi
Rais Jakaya Kikwete kuangalia njia bora ya kunusuru fedha za walipa kodi
maskini zinazotumika katika mchakato wa Katiba Mpya.
“Kama Katiba ni ya wananchi tulipaswa kuwa kitu
kimoja, kwamba tunaingia mle ndani kwa masilahi ya Watanzania lakini
kama hakuna mwafaka hadi sasa huko mbele ni giza nene.
“Kwa maoni yangu hekima itumike. Ni busara tu
imebaki kwa wakubwa kuona fedha za Watanzania zinatumika vizuri. Rais
Kikwete awatazame Watanzania kwa macho ya huruma,” alisema.
Mbunge wa Mchinga (CCM), Said Mtanda alisema
wajumbe kutoka CCM wanaweza kuendelea na vikao vya Bunge la Katiba,
lakini lingekuwa jambo muhimu iwapo yangefanyika maridhiano ya pande
mbili zinazovutana.
“Kama akidi itatimia vikao vitaendelea kama
kawaida. Lakini hata kama itatimia nadhani si busara vikao vya Bunge
kuendelea kwa mtindo huo, binafsi naona turidhiane ili kunusuru hali
hii,” alisema.
Hata hivyo, Mtanda aliwataka Ukawa kutambua kuwa
si lazima kila jambo wanalolitaka litakubaliwa na kuwa iwapo
watashikilia msimamo huo ipo siku wananchi watawahukumu.
Mbunge wa Longido (CCM), Lekule Laizer alisema
lingekuwa jambo la busara kama vikao vya Bunge hilo vingeitishwa baada
ya pande mbili zinazovutana kukubaliana.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla
alisema, “Yangefanyika maridhiano kwanza na kama hilo litashindikana ni
vyema viongozi wa vyama vya siasa wangeondolewa kuwa sehemu ya Bunge
hili, ili kuondoa hali ya kila upande kuvutia kwake.”
Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango
alisema hata bila Ukawa vikao vya Bunge hilo vitaendelea kwa sababu
wajumbe wa kundi hilo walisusia kikao cha maridhiano kilichoitishwa na
Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta.
“Bunge la Katiba lina wajumbe 629 na kama Ukawa wasipokuja
sidhani kama watazuia vikao kuendelea kwa sababu hata watu 100 hawafiki.
Kikao cha Sitta ndicho kilikuwa kizuri kwa maridhiano,” alisema Kilango
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ali Keissy alisema, “Katiba ni ya wananchi wote ni vyema tungekubaliana kwanza.”
Tangu wajumbe wa Ukawa kususia Bunge, baadhi ya
wajumbe, wakiwamo wabunge wa CCM wamekuwa wakitoa maoni yanayoonyesha
kuwa bila wenzao hao, katiba itakayopatikana haitakuwa ya kidemokrasia.
Miongoni mwa wabunge hao ni Ridhiwani Kikwete wa
Chalinze alisema katika mahojiano maalumu na gazeti hili kuwa iwapo
wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka CCM watalazimisha mambo bila ushiriki
wa wenzao wa Ukawa, kuna hatari ya kupata Katiba isiyokuwa na misingi ya
kidemokrasia.
“Kwa mazingira tuliyonayo wabunge wa CCM wanaweza
kuamua kwamba walazimishe vitu, lakini ile misingi ya demokrasia
haitakuwapo,” alisema Ridhiwani na ambaye pia ni mtoto wa Rais Kikwete
na kuongeza: “Kwa sababu kupata Katiba ya kidemokrasia ni lazima
taratibu zifuatwe na Ukawa washiriki, lakini bila wao kushiriki huwezi
kusema Katiba tuliyopata ni ya kidemokrasia, tutakuwa tunajiongopea.
“Wao (Ukawa) wasipokuja na kama busara ya viongozi
wetu wa chama, busara za Bunge letu na busara ya Rais itatuonyesha
kwamba tukutane tu na tujadili, sisi tutakuja, tutajadili na
tutaipitisha lakini mwisho wa siku, ule uhalali wa document
(kilichopitishwa) hautakuwepo.”
Wiki iliyopita gazeti hili liliwanukuu wabunge
wengine wa CCM wakipendekeza kusitishwa kwa Bunge hilo ili kutafuta
maridhiano kwanza.
Miongoni mwao ni Charles Mwijage (Muleba
Kaskazini) ambaye alisema, “Kukosekana kwa Ukawa bungeni kutaathiri
upatikanaji wa Katiba Mpya...Ningekuwa na uwezo, ningeamua mchakato huu
usitishwe na tuendelee kutumia Katiba iliyopo kwa sababu suala hili
linahitaji zaidi maridhiano,” alisema.
Mjumbe mwingine, Ezekiah Oluoch (Kundi la 201)
alisema: “Katiba haipatikani kwa ubabe au wengi wape, bali inapatikana
kwa maridhiano na mwafaka bila kujali wingi wa wajumbe.”
Mbunge wa Mbeya Vijijini, Lackson Mwanjali alisema
kitendo cha Ukawa kukataa kurejea bungeni ni pigo katika mchakato wa
Katiba Mpya kwa sababu Katiba inatengenezwa kwa majadiliano na kufikia
mwafaka.
Post a Comment