“Kama hawakumbuki rekodi, hilo ndilo CCM ilitakiwa wakumbuke. Kwamba
sisi sera yetu tuliyokubaliana ilikuwa siyo Serikali mbili. Ni Serikali
mbili kwenda Serikali Moja..
Joseph Butiku
Dar es Salaam. Makada wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Joseph Butiku na Njelu Kasaka wamesema kuwa msimamo wa chama
hicho uliotokana na vikao vyake ni kuelekea Serikali moja na siyo kama
kinavyoshikilia sasa kuendelea na Muundo wa Serikali Mbili.
Makada hao walitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti
jijini Dar es Salaam hivi karibuni katika mahojiano na gazeti hili,
ikiwa ni siku tatu kabla ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza vikao vyake.
Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake
hivi karibuni, Butiku alisema kuwa uamuzi na msimamo huo wa CCM
ulitolewa mwaka 1993 baada ya kuibuka kwa hoja ya Muungano wa Serikali
tatu, iliyotolewa na wabunge waliounda kundi la G55.
“...Katika mazungumzo kwenye chama (CCM), baada ya
kuwapo mawazo ya kuwapo mfumo wa Serikali tatu, ikawa Serikali mbili,
lakini tukielekea Serikali moja. Huo ndiyo msimamo wa CCM ‘on record’,
Serikali mbili kwenda moja,”alisema Butiku na kuongeza:
Kwa mujibu wa Butiku, mgogoro uliofanya CCM
kukubali Serikali tatu uliojadiliwa kwenye vikao vya chama hicho mwaka
1992/93 awali ulikuwa kwa siri na hawakutaka Mwalimu Julius Nyerere
ahudhurie.
“Yeye alishastaafu, lakini alijitahidi kujua kinachotokea ndani ya CCM, hawakupenda kumwambia,” alisema Butiku na kuongeza:
“Nyerere alikaa nao (CCM) na kuwauliza, lakini
walimpinga. Alilia mbele yao akiuliza ili kujua sababu za kutaka
Serikali Tatu, walimpinga.”
Akieleza namna Nyerere alivyopata wakati mgumu
mbele ya wanaCCM, Butiku alisema: “Alipingwa kila kona, si mwenyekiti wa
CCM wakati huo, si rais, makamu wake, rais wa Zanzibar hata waziri mkuu
wakati huo na Spika wa Bunge wote walishakubali Serikali Tatu.
Mwishoni walikuwa kina Njelu Kasaka wakataka kwenda bungeni na kuiidhinisha. Ndiyo wakamwita Nyerere Dodoma.”
Butiku alikumbusha kuwa hoja ya sera ya Serikali
mbili ndani ya CCM ni hoja ya Nyerere na ndiyo iliyowatoa CCM kwenye
mpango wao wa kutaka Serikali tatu kwa wakati huo.
“Hoja ya Nyerere ndiyo iliwatoa CCM kwenye sera
yao mpya ya Serikali tatu. Nyerere ndiyo alikuja akasema sera yetu
(CCM), bado Serikali mbili. Ilimchukua siku mbili kuwashawishi
kukubaliana naye,”alisema Butiku.
Alifafanua kuwa Nyerere hakuwapinga waliotaka
Serikali tatu, lakini alihoji aliyewatuma na utaratibu walioufuata
kuwasilisha hoja yao.
“Hakusema wasibadili, alisema kama wanataka CCM kuwa na sera ya
kuwa na Serikali Tatu, irejeshwe kwanza kwenye chama, izungumzwe na
kuwekwa kwenye sera na ilani ya uchaguzi. Alisema kama wananchi watapiga
kura kuwachagua (CCM), watakuwa wameikubali,”alisema Butiku aliyefanya
kazi na Nyerere kwa kipindi kirefu.
Alisema kuwa katika maisha yake, Nyerere alipinga
kuvurugwa kwa utaratibu na uvunjaji wa Katiba, akionyesha hilo katika
mambo mbalimbali ikiwamo suala hilo hata lililomwondoa madarakani
aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe.
“Ugomvi wake ni kutofuata utaratibu na kuvunja
Katiba, hata ukimuuliza kama angekuwapo leo (Nyerere), angekujibu,
sababu za kumfukuza Jumbe haikuwa mawazo ya kutaka Serikali Tatu, bali
hakufuata Katiba katika kutaka Serikali Tatu, alivunja Katiba. Ugomvi wa
Nyerere ulikuwa kuivunja Katiba ya nchi.”
Kuhusu madai ya CCM kwamba zinahitajika Serikali
mbili zilizoboreshwa na siyo Serikali tatu zilizopendekezwa kwenye
Rasimu ya Pili ya Katiba, Butiku alisema:
“Serikali mbili nani alikubali, waulize hao CCM,
Serikali mbili za Nyerere zipo wapi. Serikali mbili za CCM
zilizoboreshwa zipo wapi, mbona hawaelezi wanaficha, hawaweki wazi au
wametoa kwenye gazeti maboresho ya Serikali mbili, sijaona? Wanayaficha,
huu ni wakati wa kuficha?”
Aliongeza: “CCM walikuwa na muda, wakati wa
rasimu ya kwanza kuyatoa maboresho ya Serikali mbili, lakini wameshindwa
hata sasa. Wanasiasa wanacheza na akili za Watanzania. Tume imewaambia
rekebisheni haya, hawafanyi, kelele tu. Kazi kusema tatu mbaya, mbili
zilizoboreshwa zipo wapi?”
Njelu Kasaka
Akiunga mkono kauli ya Butiku, mbunge wa zamani wa
CCM, Njelu Kasaka aliyeendesha harakati za wabunge waliounda kundi la
G55 kushinikiza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Muungano
wa Serikali tatu, mwaka 1993, alisema baada ya kuona Zanzibar wana
Serikali yao ndipo wabunge hao wakaamua kuidai Tanganyika na yeye ndiye
aliyewasilisha hoja binafsi akilitaka Bunge kuridhia hoja yake.
“Bunge nalo lilikubali Serikali tatu, lakini
Mwalimu Nyerere alipoona hivyo akazuia utekelezaji wa agizo hilo la
Bunge hadi pale CCM watapokubaliana nalo kwa kuwa Sera ya CCM ilikuwa ni
Serikali mbili kwenda moja,”alisema akiongeza:
“Nilipeleka mwenyewe hoja hiyo binafsi kwa Spika
wakati huo akiwa Pius Msekwa na wabunge wengi waliniunga mkono na hoja
yangu ya kuitaka Serikali tatu badala ya mbili ilipita.
“Mwanzo nakumbuka walipinga-pinga na wananchi
waliunga mkono. Ingekuwa wanavyounga mkono sasa, nina hakika hoja hiyo
ingepita bila wasiwasi.”
Kasaka alisema kuwa Mwalimu Nyerere alimuuliza
Malecela aliyekuwa Waziri Mkuu: “Kwa nini mmeshindwa kumshauri Rais
Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi) hadi hoja hiyo ikapita? Kama ni hivyo basi
mimi nitajitoa CCM.”
“Nyerere alisema agizo hilo litatekelezeka ila hadi akawaulize
CCM kama wanataka pendekezo hilo lipite huku sera ya CCM ikiwa ni
serikali mbili na wakikubali basi utekelezaji utaanza kutumika,” alisema
Kasaka.
Aliongeza: “Katika ngazi ya kata CCM walikubali
serikali tatu, lakini Kamati Kuu ilivyokaa ikapendekeza serikali mbili
kuelekea serikali moja na uamuzi huo ulitolewa nakumbuka ilikuwa Agosti
mwaka 1994.”
Kuhusu mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba, Kasaka
alisema yako sahihi na wananchi wanatakiwa kuyaunga mkono kama ambavyo
walivyowaunga mwaka 1993.
Post a Comment