Mwenyekiti wa Kamati Nambari 10 wa Bunge Maalumu la Katiba, Salmin Awadh
Salmin akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana. Picha na
Emmanuel Herman
Dodoma. Mapendekezo mapya yanayopelekwa kwenye
Kamati za Bunge Maalumu kwa ajili ya kurekebisha baadhi ya Ibara za
Rasimu ya Katiba, yamezua mivutano mikali kiasi cha baadhi ya sura
kuwekwa kiporo au kurukwa na kamati husika.
Habari zilizolifikia gazeti hili zinasema
mapendekezo hayo ni yale yanayozigusa taasisi kubwa za nchi, zikiwamo
Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama, pamoja na nafasi za Makamu wa
Rais.
Katika baadhi ya kamati yamepelekwa mapendekezo
ambayo yanataka Bunge liwe na sehemu tatu ili kutoa fursa kwa mambo ya
Tanzania Bara kujadiliwa bila wabunge kutoka Zanzibar kuwapo.
“Mapendekezo yaliyopo ni kwamba wanataka Bunge
liwe na sehemu tatu ambazo ni Bunge la Muungano kwa masuala ya muungano
na humohumo linakuwa na sehemu mbili ambazo ni wabunge wa Zanzibar kwa
ajili ya masuala ya Wazanzibari na sehemu ya Tanganyika kwa ajili ya
mambo ya bara,” kilisema chanzo chetu kutoka katika kamati moja ya Bunge
hilo.
Hata hivyo, habari zinasema baadhi ya wajumbe wa
kamati walikosoa pendekezo hilo kwa maelezo kwamba linashabihiana na
muundo wa muungano wa serikali tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba lakini ukapingwa na baadhi ya wajumbe wakiongozwa
na walio wanachama wa CCM.
Jana Mwenyekiti wa Kamati Namba 8, Job Ndugai
aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati yake imeshindwa kuafikiana
kuhusu muundo wa Bunge la Muungano hivyo kulazimika kuliacha suala hilo
ili kulifanyia uchunguzi kwanza.
“Mbali na sura ya 5 inayozungumzia uraia pacha
ambayo ilitusumbua, lakini pia suala la Muundo wa Bunge la Muungano na
Mahakama ya Muungano vilikuwa tatizo katika kamati yangu,” alisema
Ndugai.
Licha ya kwamba Ndugai hakuzungumzia suala hilo
kwa undani, lakini taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema muundo wa
kuwa na sehemu tatu katika Bunge moja ndio uliozua mtafaruku kiasi cha
kamati hiyo kuliahirisha.
Katika kamati namba 5, sura ya 10 inayozungumzia
suala la Bunge na Mahakama imerukwa. Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo
alisema: “Tumeamua kuendelea na mambo mengine kwanza maana hilo
limeonekana kuwa ni gumu kwa sasa.”
Habari zaidi zinasema katika kamati hiyo namba
tano, mapendekezo ya kuwapo kwa makamu wa rais watatu yalizua mjadala
mkali kiasi cha kusababisha kuwapo kwa wajumbe walioamua kuandaa maoni
ya wachache.
“Wamekuja na mapendekezo kwamba awepo Makamu wa
Kwanza wa Rais ambaye atakuwa mgombea mwenza, Makamu wa Pili wa Rais
ambaye atakuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Tatu wa Rais ambaye ni
Waziri Mkuu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kamati hiyo na
kuongeza:
“Lakini wapo waliokataa kama watano au sita hivi
na wameamua kwamba wataandika maoni ya wachache kwa mujibu wa Kanuni ya
32 (10)”.
Hoja hiyo inafanana kabisa na ile iliyowasilishwa katika Kamati
namba 10 na kusababisha mgawanyiko uliozalisha kuwapo kwa maoni ya
wachache ambayo kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili
yataandaliwa na Mbunge wa Mpanda Mjini (Chadema), Said Arfi na mwenzake
kutoka kundi la 201 Adil Mohamed Ali.
Katika Kamati Namba 11, habari zinasema suala hilo
pia lilizua mvutano baina ya wajumbe wanaounga mkono mfumo wa Serikali
mbili na wale wanaotaka Serikali tatu na kwamba aliyeokoa jahazi ni
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ambaye alitoa
mapendekezo kuhusu mifumo yote miwili.
“Katika kamati yetu wanasema eti tayari mfumo wa
Serikali mbili umepitishwa maana ndiyo unaungwa mkono na wengi, lakini
wengine wamekataa, kwa hiyo ndiyo maana masuala kama haya yanatupa shida
kwelikweli,” kilisema chanzo chetu.
Hata hivyo, kwa mujibu wa habari hizo, kamati hiyo
namba 11 iliunda kamati ndogo ya watu watatu akiwamo Naibu Waziri wa
Kilimo, Godfrey Zambi ili kupitia mapendekezo ya Othman kabla ya
kuyarejesha kwenye kamati nzima kwa ajili ya kufanya uamuzi.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Christina
Mnzava alipotafutwa jana kutoa ufafanuzi wa suala hilo alisema
asingeweza kuzungumza kwani alikuwa kwenye kikao. Othman kwa upande wake
naye alisema hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo kwani lipo
kwenye mamlaka ya kamati.
Habari zaidi zinasema pia kumekuwa na mvutano
pale kunapokuwa na mapendekezo ya kufutwa kwa maneno Tanganyika na
Shirikisho, kwani baadhi ya wajumbe wamekuwa wakitaka yaendelee kuwapo
kama yalivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hadi pale Bunge
zima litakapofanya uamuzi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati Namba 10, Salmin
Awadh Salmin, alikiri kwamba katika maeneo mengi ambako kulikuwa na
maneno hayo wameyaondoa kwa kuzingatia kuwa ndiyo yalikuwa makubaliano
ya wengi.
“Ingawa bado tuna watu ambao ni sehemu ya Ukawa,
lakini ni wachache na pamoja na hoja zao za msingi, lakini zinaonekana
kumezwa na wajumbe walio wengi ambao ndio wanaounga mkono Serikali
mbili,” alisema.
Akizungumzia changamoto zilizowapata ndani ya
kamati yake, alitaja kuwa ni suala la kutenganisha madaraka ya mawaziri
na wabunge.
Kwa maelezo ya kiongozi huyo, jambo hilo lilitoa
mvutano mkali ndani ya kamati yake na kuwa litaamuliwa Jumatatu ingawa
wao kwenye uraia walipitisha uraia pacha.
Frederick Sumaye
Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye ameshauri
kusimamishwa kwa Mchakato wa Katiba kutokana na mvutano kati ya wajumbe
wa Chama Cha Mapinduzi na wale wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) akionya kuwa bila ya maridhiano hakuna katiba bora.
Akifungua Kongamano la Kuombea Katiba Mpya na Uchaguzi na Amani
nchini lililoandaliwa na Free Pentecostal Church in Tanzania (FPCT) na
kufanyika mkoani Kigoma, Sumaye amesema kuwa Bunge ni nyumba ya kujenga
hoja na siyo nyumba ya mapambano wala ubabe.
“Pamoja na umuhimu huu wa kupata Katiba Mpya,
Watanzania tungependa katiba itakayopatikana kwa maelewano na maridhiano
ya pande zote husika. Bunge ni nyumba ya kujenga hoja na siyo nyumba ya
mapambano wala ubabe. Kinachotakiwa wabunge wote washiriki na hatima ya
yote ni wengi wape na wachache wasikilizwe,” alisema Sumaye na
kuongeza:
“Kama inaonekana dhahiri kuwa hatutapata katiba
nzuri kwa wakati uliopo, ni busara mchakato huu ukasimama, Watanzania
tukajipa muda zaidi tukayatafakari haya ili tuje tupate katiba mwafaka
kwa muda mwafaka. Itakuwa ni ushindi batili kama tutang’ang’ania
kutengeneza katiba ambayo siyo ya manufaa kwa Watanzania wote.
Sumaye ambaye ni mmoja wa makada wa CCM
waliojipambanua kutaka kuwania urais mwakani, alisema mchakato huo
umetumia fedha nyingi za walipakodi ambazo zingetumika katika kuboresha
huduma mbalimbali za jamii kama vile afya, elimu, maji na miundombinu.
Alisema licha ya sura nyingi katika Rasimu ya
Katiba, sura zinazozungumzia Muungano ndizo zimekuwa ngumu licha ya kila
upande kutoonyesha nia ya kuuvunja.
Hata hivyo, Sumaye alipendekeza muundo wa serikali mbili, kwani kuongezwa kwa idadi ya Serikali hakutakuwa suluhisho.
Huku akionyesha kutoamini kama mchakato huo kuwa
suluhisho la mwisho la maendeleo ya Watanzania, Sumaye alionya kuhusu
ulafi wa madaraka:
“Kama tumefika hapa kwa sababu kuna matatizo ya
madaraka au utawala kwa vyovyote jawabu lake siyo Serikali tatu kwa
sababu kufanya hivyo kutafanya tatizo liwe kubwa zaidi. Kama tumefika
hapa kwa sababu ya mivutano ya rasilimali, basi kuwa na mfumo wa
Serikali tatu kutafanya hali iwe ngumu zaidi,” alisema na kuongeza:
“Kwa maoni yangu kama kuna mvutano wowote kati ya
Serikali ya Jamhuri na Serikali ya Zanzibar katika muundo wa Serikali
mbili, na tukaanzisha Serikali ya Tanganyika kabla hatujatatua mivutano
iliyopo, hiyo mivutano itaendelea kuwapo na tutazalisha mivutano mingine
mipya.”
Imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Elias Msuya Dar es Salaam.
Post a Comment