Dar es Salaam. Shirikisho la Jumuiya ya Madola
(CGF) limetoa vibali vya wanamichezo watatu wa Tanzania katika mchezo
wa judo kushiriki kwenye Michezo ya Madola itakayofunguliwa kesho jijini
Glasgow, Scotland.
Wachezaji, Gervas Chilipweli, Ahmed Magogo na
Amour Kombo waliachwa kwenye msafara wa Tanzania ulioondoka nchini
Jumatano iliyopita kwenda Scotland kwa kile kilichoelezwa na Katibu Mkuu
wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi kuwa majina yao
hayakuonekana CGF.
Mapema jana, Bayi ambaye yuko Scotland kwenye
mkutano mkuu wa CGF ulioanza jana aliliambia gazeti hili kuwa shirikisho
hilo limeridhia wanajudo hao kujumuishwa kwenye timu ya Tanzania.
“Tayari wamefanyiwa usajili ili kupokelewa
kijijini na nimeshatuma taarifa wizarani, hivyo nadhani sasa wizara
itashughulikia utaratibu wa safari ili kujumuika na wenzao kwenye
michezo hii,” alisema Bayi.
Naibu Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini,
Juliana Yasoda alisema tayari wamepata taarifa hiyo na sasa wako kwenye
mchakato wa kuangalia wachezaji hao watafikaje Glasgow inapofanyika
michezo hiyo.
“Tunaendelea na mchakato wa kuwasafirisha
wachezaji wa judo, sambamba na kushughulikia visa ya Ikangaa (Dotto)
ambayo tukifanikiwa wataondoka pamoja wakati wowote,” alisema Yasoda.
Akizungumzia hali ya wanamichezo wa Tanzania, Bayi
alisema wote wako katika hali nzuri ya ushindani na wanaendelea na
mazoezi chini ya makocha wao tayari kwa mashindano hayo.
Post a Comment