Dar es Salaam. Bodi ya Taifa ya Uhasibu na
Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), imesema watahiniwa wa shahada ya juu ya
ukaguzi nchini CPA-(T) imeongezeka kutoka 478 mwaka 1975 na kufikia
5,646, mwaka huu.
Ongezeko hilo linatokana na matokeo ya mitihani ya
NBAA iliyofanyika Mei, mwaka huu, kwa watahiniwa 1,327 kati ya 4,395
sawa na asilimia 30.2 kufaulu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, Profesa
Mussa Assad akitangaza matokeo hayo jana Dar es Salaam, alisema
watahiniwa 1,674 sawa na asilimia 40.8 watarudia somo au masomo
waliyoshindwa na watahiniwa 1,394 sawa na asilimia 31.7 hawakufaulu
mitihani.
Alisema katika ngazi ya mwisho (Final Stage Module
F), watahiniwa 467 sawa na asilimia 28.7 kati ya 1,625 waliofanya
mtihani huo wamefaulu na wengine 790 sawa na asilimia 48.7 watarudia
somo moja na watahiniwa 368 sawa na asilimia 22.6 hawakufaulu.
“Watahiniwa 644 sawa na asilimia 30.5 kati ya
watahiniwa 2,109 wamefaulu mtihani wa taaluma ngazi ya Module E na
wengine 595 sawa na asilimia 33.5 watarudia somo moja na 870 sawa na
asilimia 41.3 hawakufaulu,” alisema Assad ambaye pia ni Profesa wa Shule
ya Bishara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Tunafurahi kuona kuna ongezeko la ufaulu
ukilinganisha na miaka minne iliyopita, lakini pia wanawake wameendelea
kuongezeka, mwaka huu walikuwa asilimia 31 kati ya watahimiwa wote
4,395.”
Kuhusu mabadiliko ya mitalaa, Profesa Assad
alisema NBAA imeibadili tangu mwezi uliopita na itaanza kutumika kwa
mara ya kwanza Novemba, mwaka huu.
“Wanafunzi walioko katika mitalaa iliyofutwa
wanatakiwa kusoma na kuelewa mfumo wa uhamaji iliyowekwa kwenye tovuti
ya Bodi ili waweze kufahamu ni masomo gani wanatakiwa kujisajili katika
mitalaa hiyo,” alisema.
Post a Comment