Bahi. Mwenyekiti wa Kijiji cha Chonde Kata ya
Makanda wilayani hapa, Daud Nhiti ameuagiza uongozi wa kijiji kumweka
mahabusu Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ng’ambo, Zebedayo Hemezi kwa kosa
la kutohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa zahanati.
Amri hiyo ilitolewa juzi baada ya mwenyekiti huyo
wa kijiji kutoa agizo kwa wenyeviti wote wa vitongoji kujitokeza katika
harambee hiyo na mwenyekiti huyo wa Ng’ambo kutofika bila ya taarifa.
Nhiti ambaye ni kiongozi katika kijiji hicho
aliwaamuru wenyeviti hao kuhakikisha wanachangisha fedha kwa ajili ya
ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Chonde kutokana na kijiji hicho
kutokuwa na kituo cha huduma za afya tangu Uhuru.
Wazo la ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho lilitolewa na Diwani wa Kata ya Makanda, Antoni Lyamunda.
Hata hivyo ,wazo hilo limedaiwa kugeuka mwiba kwa wananchi na sasa wanalalamikia kulazimishwa kuchangia ujenzi huo.
Baadhi ya wananchi walisema wamekuwa
wakichangishwa michango kwa nguvu na wakati mwingine hulazimika kuuza
mifugo yao kwa hasara.
Walisema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa na tabia
ya kuahidi kutoa michango kwa ajili ya shughuli za maendeleo lakini
hawatimizi na matokeo yake hulazimisha wananchi ambao vipato vyao ni
vidogo.
Diwani Lyamunda alisema kutokana na wakazi hao
kutokuwa na huduma ya zahanati au kituo cha afya aliamua kuibua wazo
hilo la ujenzi wa zahanati kwa kushirikisha wananchi ili kuishinikiza
Serikali kutoa hela kwa ajili ya kuiendeleza.
Alisema pamoja na juhudi mbalimbali za kuanzisha
ujenzi huo pia aliibua wazo la kufanya harambee kwa ajili ya kuchangia
ujenzi wa zahanati ya Chonde.
Katika harambehe hiyo iliyohudhuriwa na Mbunge wa
Jimbo la Bahi, Omar Badwel (CCM), mwakilishi wa Mganga Mkuu wa hospitali
ya rufaa, Ally Nyange, madiwani pamoja na wananchi wa kada mbalimbali
Sh1.8 milioni ziliweza kupatikana na ahadi ilikuwa Sh9.8 milioni na
kufanya jumla kuu kuwa Sh11.1 milion.
Katika harambee hiyo pia baadhi ya wananchi wa jamii ya wafugaji walichangia ng’ombe wawili na mbuzi wawili.
Post a Comment