Joseph Kapinga
Fainali za Kombe la Dunia zimekwisha. Ujerumani wametwaa ubingwa
wa kuifunga Argentina bao 1-0 katika mchezo wa fainali wiki moja
iliyopita nchini Brazil.
Ule mwezi mzima wa mashabiki wa soka kuelekeza
masikio na macho nchini Brazil, umepita, hakuna tena stori. Imebaki
kumbukumbu na maisha yanaendelea.
Tunarudi nyumbani kwenye soka letu la nyumbani. Soka lenye changamoto za migogoro, majungu, fitina, chuki na visasi.
Ukiona soka limemezwa na mambo hayo, usitarajie
hata siku moja mafanikio yakapatikana. Itoshe kusema kwamba, soka letu
linahitaji mapinduzi makubwa.
Inasikitisha, siku zinakwenda na hakuna
mabadiliko, siyo kwenye klabu wala vyama vya michezo. Migogoro kila
kukicha. Yanga wameuongezea uongozi wao muda wa kukaa madarakani. Siyo
wote waliopenda uamuzi huo. Hali hiyo tayari inaweza kuzaa mgogoro.
Simba walifanya uchaguzi mkuu hivi karibu. Sote
tumeshuhudia yaliyotokea, uchaguzi ulifanyika baada mvutano mkali kiasi
cha hata baadhi ya wanachama kwenda mahakamani kutaka kuusimamisha.
Tunamlaumu nani wakati sisi wenyewe ndiyo chanzo
cha migogoro? Wenzetu wanalilia kuweka rekodi za mafanikio kwenye
mashindano makubwa ya soka, sisi tunapigania kuweka rekodi za kuzalisha
migogoro.
Kinachotokea kwenye soka letu, ni sawa na mtu
asiyependa kuona watu wanaishi kwa amani, atafanya kila njia
kuwagombanisha. Soka letu liko hivyo. Hatuwapi nafasi viongozi, tukiona
viongozi wametulia, hakuna migogoro, hakuna chuki, fitina, majungu
tunaumia. Tunataka migogoro.
Unajua kwa nini yote haya? Kwa sababu, migogoro
kwenye klabu zetu haipendwi, lakini siyo wote wasiyoipenda. Kwenye
migogoro, kuna watu wanafaidika nayo. Fikiria, shabiki anayeishi mjini
kwa sababu ya kufaidika na migogoro, leo anawezaje kuwa na furaha kama
hakuna migogoro? Atakubali vipi kufa njaa wakati ana taaluma ya
kulazimisha migogoro kutokea?
Haya ndiyo maisha ya soka letu. Kama vile fainali
za Kombe la Dunia zilivyomalizika na maisha yanaendelea kama kawaida,
ndivyo hivyo kwetu.
Tumerudi kwenye maisha ya kawaida ya soka letu.
Soka ambalo tunatumia muda mwingi kuwekeza migogoro badala ya maendeleo.
Alaumiwe nani?
Viongozi wetu wamepitwa na wakati, bado wapofu.
Hawana kiu ya maendeleo kupitia kujifunza kwa wenzetu walioachana na
uwekezaji kwenye migogoro na kuangalia mbele.
Nchi hii ina vijana wenye vipaji vya hali ya juu. Hatuwaangalii
kabisa. Tutaonaje vipaji vyao wakati macho na fikra zetu zimejaa utumwa
wa migogoro?.
Tukipenda tunaweza kuleta mageuzi, lakini kamwe
hayatapatikana kama tutaendelea kuwa viongozi walewale, wanachama wa
migogoro walewale. Tujifunze kutoka kwa wenzetu!
Post a Comment